LAAC yatoa maelekezo wanufaika mikopo ya asilimia 10 za halmashauri

NA ASILA TWAHA

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imetoa wito kwa vikundi vinavyopatiwa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kurejesha mikopo waliyokopeshwa ili kutoa nafasi kwa vikundi vingine kuweza kukopa.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara walipotembelea Kikundi cha Vijana cha Kimbilio kinachojishughulisha na uzalishaji wa chaki.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Halima Mdee (Mb) amesema, fedha zilizotolewa na Serikali sio kwa ajili ya kutolewa bure bali ni kuwezesha jamii kujiendeleza kichumi katika kujitafutia riski na kujikwamua kimaisha, hivyo ni jukumu la kila kikundi kilichopatiwa mkopo kuweza kurejesha ili kuwapa nafasi vikundi/jamii nyingine kuweza kukopeshwa.

“Tumekuja kujiridhisha kama kweli mlipewa mkopo na mnajishughulisha na biashara mliohitaji,”amesema Mhe.Mdee.

Akielezea lengo la ziara hiyo ni kutaka kujua maendeleo ya shughuli zinazofanywa na vikundi hivyo na kuwataka kuhakikisha wanarejesha mkopo kwa wakati ili wengine waweze kupatiwa mikopo hiyo.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kikundi Katibu wa Kikundi cha Vijana cha Kimbilio, Bw. Shaibu Gobosi amesema, wanaishukuru Serikali kwa kuwapa nafasi na kuwaamini kuwakopesha shilingi milioni 38 ambapo wemeweza kuanzisha kiwanda cha uzalishaji wa chaki na kununua mashine na malighafi.

Gobosi ameeleza kuwa, pamoja na mkopo huo ameiomba Serikali kuisapoti biashara yao iwe ni yenye kuleta tija na maendeleo kwa familia yao lakini jamii kwa ujumla.

Aidha, amesema Serikali ikiendelea kuunga mkono jutihada zao italeta chachu kuimarisha vikundi vingine vya vijana wajasiriamali ndani na nje ya Halmashauri ya Mji Nanyamba.

Pia ameiomba Serikali kuwekeza kwenye ununuzi wa chaki hizo katika kiwanda hicho ili kuwapa ari ya kufanya kazi na kuongezeka kipato.

“Tupo wanachama 10 na hii imetusaidia kufanya kazi na tunaamini baadae tutapata manufaa, lakini pia kwa sasa tunayo ajira sababu tunakuja hapa tunajishughulisha,”alisema.

Alifafanua mikakati ya kikundi kuwa ni kujiwekeza zaidi kwa kutafuta masoko ndani ya Mkoa wa Mtwara na nje ya Mkoa wa Mtwara kwa sababu chaki wanazozalisha katika kiwanda hicho ni zenye ubora na zimethibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

“Tunashukuru Mkoa wa Mtwara zipo shule ambazo wanatumia chaki tunazozalisha, tunaiomba Serikali, kupitia kwa ninyi viongozi wetu mtusaidie kututangazia chaki tunazozalisha ziweze kutumika katika shule zote ndani ya mkoa wetu na nje,” amesema Gobosi.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa imekipongeza kikundi hicho kwa uthubutu wa kuwa na wazo kujishughulisha na uzalishaji wa kutengeza chaki pia imewataka kuweka jitihada za pamoja kwa kushirikiana ili waweze kufikia malengo yao bila kukatishwa tamaa na kuondokana na tamaa za kuweka faida kwanza.

“Jitahidini kufanya kazi kwa bidii ili muweze kurejesha mikopo na wwenzetu waweze kupatiwa endeleeni kuwa wabunifu kwa kufanya kazi yenye ubora zaidi,”alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news