NA DIRAMAKINI
HALMASHAURI ya Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe imewekwa chini ya karantini dhidi ya ugonjwa wa homa ya nguruwe (African Swine Fever).
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Machi 15, mwaka huu na Daktari wa Mifugo Wilaya ya Ludewa, Dkt.Festo Mkomba.
Dkt.Mkomba amefafanua kuwa, amefikia uamuzi huo kwa mamlaka aliyopewa na Sheria ya Mifugo namba 16 (2), 17 ya mwaka 2003 ambapo kuanzia Machi 15, mwaka huu wilaya hiyo itakuwa chini ya karantini mpaka hapo itakavyotangazwa vinginevyo.
"Hii ni kutokana na matukio ya ugonjwa wa homa ya nguruwe kujitokeza katika Wilaya ya Ludewa. Kwa tangazo hili hakuna kuingiza aina yoyote ya nguruwe wala kutumia mazao yoyote ya nguruwe kama nyama, damu, samadi, mifupa, nywele katika wilaya hii, isipokuwa kwa idhini ya Daktari wa Mifugo wa Wilaya ya Ludewa. Atakayekiuka masharti ya tangazo hili, ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria,"amefafanua Daktari huyo.