Makamu wa Rais atoa maagizo ujenzi wa barabara

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Mpango ameitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuwasimamia wakandarasi wanaojenga barabara ya kiwango cha lami ya Kabingo ,Kasulu hadi Manyovu mkoani Kigoma yenye urefu wa kilometa 260 kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Dk Mpango amesema hayo wakati akizungumza na Kamati ya Bunge ya Mitaji na Uwekezaji wa Umma iliyokuwa inatembelea miradi iliyo chini ya kamati hiyo mkoani Kigoma na kusema kuwa barabara hiyo ni mkombozi kwa wananchi wa mkoa huo.

Alisema kuwa, wananchi wa mkoa Kigoma wana imani kubwa na Raisi Samia kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali hivyo imani hiyo lazima ioneshwe kwa vitendo kwa miradi inayotekelezwa kumalizika kwa wakati na kuinua uchumi wa wananchi wa mkoa huo.

Alisema kuwa, Barabara ya Kabingo,Kasulu hadi Manyovu ni tegemeo la uchumi la wananchi wa mkoa Kigoma kwani shughuli zao kuu za uchumi kibiashara kwenye kuuza na kununua inafanyika mikoa ya Mwanza na Mji wa Kahama mkoa Shinyanga hivyo barabara hiyo inakuwa kiunganishi muhimu kiuchumi katika kusafirisha bidhaa na wafanyabiashara wa mkoa huo na mikoa mingine.

Sambamba na hilo alisema kuwa barabara hiyo pia ni kiungo muhimu cha usafirishaji wa mizigo na abiria kwenda mikoa mbalimbali ya nchi ya Burundi na kwamba barabara hiyo ni sehemu wa miradi ya kikanda kwa nchi za Afrika Mashariki ambayo Burundi ni Mwanachama.

“Mkurugenzi Mkuu TANROAS Ningependa kuona mradi huu unaisha kwa wakati wasimamieni wakandarasi watekeleze majukumu yao kulingana na mkataba na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi angalia suala la malipo kwa wakandarasi kama kuna changamoto zozote zileteni mapema tuzifanyie kazi,”alisema Makamu wa Raisi.

Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya uwekezaji na mitaji, Jerry Slaa alimwambia Makamu wa Raisi kuwa wana imani na Raisi Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo inayofanyika nchini.

Slaa alisema kuwa mkoani Kigoma kamati hiyo imetembelea kituo cha kuzalisha umeme uliopo Bangwe mjini Kigoma, Bandari ya Kigoma na Barabara hizo za kiwango cha lami na kuridhishwa na kazi kubwa ambayo imefanywa kwenye miradi hiyo.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa barabara nchini, Rogartus Mativila alisema kuwa jumla ya kilometa 260.6 za kiwango cha lami zitajengwa zenye thamani ya shilingi Bilioni 325 na wakandarasi wanne wanatekeleza mradi huo kwa vipande tofauti tofauti.

Mativila alisema ujenzi wa barabara hiyo itaunganisha mkoa Kigoma na mikoa ya Kagera,Geita, Shinyanga na Mwanza na nchi jirani ya Burundi na kwamba ipo miradi ya kijamii ikiwemo shule mpya ya msingi, masoko, vituo vya afya na stendi za mabasi zitajengwa kama sehemu ya mradi huo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa ujenzi na uchukuzi anayeshughulikia ujenzi, Ludovick Nduhiye alisema kuwa hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 59 na barabara za lami zenye urefu wa kilometa 68 zimekamilika.

Alisema kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa kilometa 260.6 za barabara za kiwango cha lami, daraja kubwa moja, madaraja ya kawaida manane, makaravati makubwa 103 na makaravati madogo 306.

Hadi sasa shilingi bilioni 15 zimelipwa fidia kwa wananchi ambapo hadi kufikia Februari mwaka huu wakandarasi wote wameshalipwa shilingi bilioni 171 na wahandisi washauri wameshalipwa shilingi Bilioni 8.4.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news