MIWILI YAKE SAMIA-5: Nchi kavu,majini na angani

NA LWANGA MWAMBANDE

NDANI ya miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, Watanzania wameendelea kushuhudia Serikali ikianzisha na kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Utekelezaji wa miradi hiyo ni kuanzia ile ya afya, elimu, maji,sekta ya usafirishaji na uchukuzi ambayo inagusa pande zote kwa maana ya usafiri wa anga, majini na nchi kavu.

Bidii na juhudi za Serikali katika kuyaendea mafanikio hayo huku wakiongozwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka 2020 hadi 2025 imewafanya wengi kuguswa na kupongeza.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita ni Serikali ya Kazi Iendelee, haitaki kuona jambo linayumbishwa au kucheleweshwa, kwani yote ni kwa manufaa ya umma na Taifa. Endelea;

116.Kwingine hujatulia,
Miradi kujifanyia,
Barabara zetu pia,
Heko Rais Samia.

117.Dasalamu naanzia,
Twafika twafurahia,
Ni tamu inavutia,
Heko Rais Samia.

118.Pale ulipoanzia,
Hukubaki kusinzia,
Miradi kumalizia,
Heko Rais Samia.

119.Mfano kujitajia,
Jiji Dar nakwambia,
Barabara zavutia,
Heko Rais Samia.

120.Mbezi Luis sikia,
Mbagala kichungulia,
Ni nje ya Tanzania,
Heko Rais Samia.

121.Moto walikowashia,
Wale walitangulia,
Umeukoleza pia,
Heko Rais Samia.

122.Madaraja nakwambia,
Juu juu twatambia,
Chini tunaangalia,
Heko Rais Samia.

123.Waweza jihesabia,
Ni mengi ninakwambia,
Na tena yanazidia,
Heko Rais Samia.

124.Nchi kavu yavutia,
Hata baharini pia,
Dasalamu yavutia,
Heko Rais Samia.

125.Dodoma ninaishia,
Kidogo kuangalia,
Kwani ndiyo Tanzania,
Heko Rais Samia.

126.Wakati lipoingia,
Wengine lifikiria,
Kasi eti tafifia,
Heko Rais Samia.

127.Miaka imetimia,
Miwili twaangalia,
Pazidivyo kuvutia,
Heko Rais Samia.

128.Serikali metulia,
Kazi inajifanyia,
Mji wake wavutia,
Heko Rais Samia.

129.Wale waliosalia,
La mgambo limelia,
Dodoma tushatulia,

Heko Rais Samia.

130.Dodoma kiangalia,
Macho utafurahia,
Inazidi kuvutia,
Heko Rais Samia.

131.Wageni wanaingia,
Miradi inaingia,
Amani kumetulia,
Heko Rais Samia.

132.Miradi mikubwa pia,
Timu imeshaingia,
Ili pazidi vutia,
Heko Rais Samia.

133.Ring road mesikia,
Inavyotuzungukia,
Mradi unavutia,
Heko Rais Samia.

134.Lengo ni kuzungukia,
Pembeni ukipitia,
Foleni tupunguzia,
Heko Rais Samia.

135.Jinsi unavyovutia,
Mradi ninakwambia,
Tutakuja furahia,
Heko Rais Samia.

136.Mradi huo sikia,
Ajira watupatia,
Vijana changamkia,
Heko Rais Samia.

137.Tukimsema Samia,
Serikali Tanzania,
Ndiye aisimamia,
Heko Rais Samia.

138.Mipango nayoingia,
Yeye tiki apatia,
Miwili kashikilia,
Heko Rais Samia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news