MIWILI YAKE SAMIA-6:Ni mashangilio kote nchini

NA LWAGA MWAMBANDE

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imetoa kipaumbele kikubwa katika Sekta ya Elimu kwa kuhakikisha miundombinu ya shule za msingi na sekondari imeboreshwa ili kila mtoto wa Kitanzania apewe nafasi ya kupatiwa elimu bora na ya uhakika.

Ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt.Samia, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefanya magaeuzi makubwa katika sekta hiyo.

Mageuzi hayo yamechochea msukumo mkubwa wa kuhakikisha kila mtoto anakwenda shule, kitu ambacho kimeongeza idadi ya watoto wanaojiunga na masomo kwa shule za msingi na sekondari.

Pia imekuwa ikihakikisha watoto wote hata wale walioacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo kupata mimba, wanafutiwa mkakati wa namna ya kurudi shule.

Aidha, katika kuhakikisha miundombinu ya shule inaandaliwa kupokea idadi kubwa ya wanafunzi kwa mwaka huu, sekta ya elimu imepokea robo ya mgawanyo wa fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 ambapo zaidi ya madarasa 15,000 yamejengwa kutokana na fedha hizo.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, si hayo tu bali pia hata kwa upande wa elimu ya juu, ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt.Samia, mambo ni mazuri na bila kusahau sekta zingine mashangilio yapo kila eneo nchini. Endelea;

139.Elimu sijagusia,
Inazidi shamiria,
Mengi ametufanyia,
Heko Rais Samia.

140.Wengi tunafurahia,
Haya yanayotukia,
Kutoka na kuingia,
Heko Rais Samia.

141.Elimu bure sikia,
Dola inagharamia,
Wazazi twafurahia,
Heko Rais Samia.

142.Tukitaka kuchangia,
Siyo kulazimishia,
Ni vile twajipangia,
Heko Rais Samia.

143.Miaka miwili pia,
Majengo yameingia,
Ni mengi ninakwambia,
Heko Rais Samia.

144.Madarasa Tanzania,
Ya watoto kutumia,
Ni mengi kukutajia,
Heko Rais Samia.

145.Lengo tuweze fikia,
Mazingira kuvutia,
Kusomea Tanzania,
Heko Rais Samia.

146.Hili uliloanzia,
Ajira kuwapatia,
Walimu twashangilia,
Heko Rais Samia.

147.Tena tumeshasikia,
Wasichana kukazia,
Shule bweni kuzidia,
Heko Rais Samia.

148.Kila mkoa sikia,
Shule moja taingia,
Ei levo shangilia,
Heko Rais Samia.

149.Lingine lituambia,
Wengi tukakusikia,
Sasa limeshatujia,
Heko Rais Samia.

150.Watoto walofulia,
Shule wakazikimbia,
Darasani waingia,
Heko Rais Samia.

151.Utoro kujitakia,
Na ule kufanyizia,
Elimu wafurahia,
Heko Rais Samia.

152.Idadi kubwa sikia,
Mimba zilizoingia,
Shule kuwakatizia,
Heko Rais Samia.

153.Darasani waingia,
Wengi wanafurahia,
Nafasi kujipatia,
Heko Rais Samia.

154.Nguvu kazi nakwambia,
Taifa kutumikia,
Na uchumi kuchangia,
Heko Rais Samia.

155.Hivi anatufanyia,
Si tiketi kuzidia,
Mimba kuchangamkia,
Heko Rais Samia.

156.Wanaume mwasikia,
Watoto kufwatilia,
Jela mtajaingia,
Heko Rais Samia.

157.Wanafunzi angalia,
Acha kuwasarandia,
Heshima mwajivunjia,
Heko Rais Samia.

158.Wanawake Tanzania,
Wengi mkihitajia,
Mila zenu zingatia,
Heko Rais Samia.

159.Umri ukitimia,
Wakishajihitimia,
Ruksa kufwatilia,
Heko Rais Samia.

160.Nanyi wanafunzi pia,
Ni shule kuzingatia,
Mengineyo achilia,
Heko Rais Samia.

161.Umri mkifikia,
Mbele mtayakutia,
Yasijewavurugia,
Heko Rais Samia.

162.Wale waliyavamia,
Na mimba zikaingia,
Si vizuri kurudia,
Heko Rais Samia.

163.Nafasi mejipatia,
Ya kujisahihishia,
Ni vema muda tumia,
Heko Rais Samia.

164.Afya tunajivunia,
Kiwa njema furahia,
Huko ndiko naingia,
Heko Rais Samia.

165.Sekta twafurahia,
Huduma yatupatia,
Walo huko shangilia,
Heko Rais Samia.

166.Tiba twaing’ang’ania,
Tena twaishadidia,
Tusizidi kuumia,
Heko Rais Samia.

167.Huku ndiko kapania,
Yale anatufanyia,
Mengi ya kufurahia,
Heko Rais Samia.

168.Zinajengwa zaingia,
Zahanati nakwambia,
Watu waweze tumia,
Heko Rais Samia.

169.Na dawa kuwafikia,
Bila kawiakawia,
Hilo anaangalia,
Heko Rais Samia.

170.Hata gonjwa la dunia,
Ambalo lilitishia,
Chanjo wanajichanjia,
Heko Rais Samia.

171.Afya atuinulia,
Vifaa kutupatia,
Lengo tuweze fikia,
Kuridhisha Tanzania.

172.Serikali ya Samia,
Jinsi yatuangalia,
Mazuri yanazidia,
Heko Rais Samia.

173.Bima afya nakwambia,
Kwa wote inaingia,
Kusiweko kukimbia,
Heko Rais Samia.

174.Kama ikishaingia,
Watu wote kuingia,
Mashaka yataishia,
Heko Rais Samia.

175.Endapo utaumia,
Au kujiugulia,
Tiba tutakupatia,
Heko Rais Samia.

176.Si kujihangaikia,
Pesa kujitafutia,
Upate kujitibia,
Heko Rais Samia.

177.Ni mipango ya Samia,
Ambayo atupatia,
Nasi tunafurahia,
Heko Rais Samia.

178.Afya akitufanyia,
Pazuri tukafikia,
Wengi tutafurahia,
Heko Rais Samia.

179.Sasa wengi wanalia,
Ugonjwa ukiingia,
Gharama zawazidia,
Heko Rais Samia.

180.Bima kwa wote sikia,
Ndiyo itatutibia,
Mzigo kutushushia,
Heko Rais Samia.

181.Hili la kuangalia,
Na kujaziajazia,
Huduma tafurahia,
Heko Rais Samia.

182.Watumishi nakwambia,
Idadi hajafikia,
Shida tunapitia,
Heko Rais Samia.

183.Ila twakuaminia,
Vema utatufanyia,
Waweze tuhudumia,
Heko Rais Samia.

184.Wengi kama waingia,
Faida inaingia,
PAYE watakupatia,
Heko Rais Samia.

185.Serikali ya Samia,
Afya kwa kuzingatia,
Huduma kutupatia,
Heko Rais Samia.

186.Ambyulensi twasikia,
Dola inatumwagia,
Kote kote kufikia,
Heko Rais Samia.

187.Ni Halmashauri pia,
Zotezote tafikia,
Huduma rahisishia,
Heko Rais Samia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news