MPC yabaini matokeo chanya kupitia Uchumi wa Buluu,sera imara Zanzibar

NA GODFREY NNKO

JITIHADA mbalimbali zinazozoendelezwa na Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi zimetajwa kuwa na matokeo chanya katika uchumi.

"Kwa upande wa Zanzibar, uchumi unakadiriwa kukua kwa asilimia 5.4 mwaka 2022, kutokana na jitihada zinazoendelea katika kuimarisha uchumi wa buluu, kuimarika kwa shughuli za utalii, pamoja na sera madhubuti za fedha na kibajeti;

Hayo yamebainishwa leo Machi 14, 2023 na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tututba kupitia tamko la MPC ambayo ilikutana leo kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha katika miezi Januari na Februari 2023.

Sambamba na mwenendo wa uchumi, na kufanya maamuzi ya mwelekeo wa utekelezaji wa sera ya fedha kwa miezi miwili ijayo.

"Kamati inatarajia ukuaji wa uchumi kuendelea kuimarika zaidi ndani ya mwaka 2023 kutokana na ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, jitihada mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, kuimarika kwa shughuli za utalii, na utekelezaji wa sera madhubuti za fedha na kibajeti,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Mwenyekiti wa kamati.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, hali hiyo itachagizwa pia na matarajio ya kupungua kwa shinikizo la mfumuko wa bei na kuimarika kwa mnyororo ya ugavi duniani.

MPC imebainisha kuwa, mfumuko wa bei umeendelea kuongezeka katika miezi ya hivi karibuni, kutokana na athari ya vita inayoendelea nchini Ukraine, ambayo imesababisha ongezeko la bei za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.

"Mfumuko wa bei kwa Tanzania bara uliongezeka na kufikia asilimia 4.9 mwezi Januari 2023, kutoka asilimia 4.8 mwezi uliotangulia, kiwango ambacho kimeendelea kubakia ndani ya lengo la nchi la asilimia 5.4 kwa mwaka 2022/23, na vigezo vya mtangamano vya nchi wanachama wa EAC na SADC vya asilimia 8 na asilimia 3 hadi 7, mtawalia.

"Kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei uliongezeka na kufikia asilimia 8.4, kutokana na ongezeko la bei za chakula na bidhaa zisizo za chakula.

"Aidha, Kamati inatarajia mfumuko wa bei nchini kubaki ndani ya lengo katika nusu ya pili ya mwaka 2022/23 kutokana na matarajio ya kuendelea kupungua kwa bei za bidhaa na mfumuko wa bei katika nchi washirika wa biashara, pamoja na matarajio ya kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula nchini,"imebainisha sehemu ya taarifa hiyo.

Wakati huo huo, MPC imebainisha kuwa, kupungua huku kutachagizwa pia na utekelezaji thabiti wa sera ya fedha inayolenga kupunguza kiwango cha ongezeko la ukwasi kwenye uchumi unaofanywa na Benki Kuu.

"Ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) ulikua kwa asilimia 12.8 katika mwaka ulioshia Januari 2023, sanjari na lengo la asilimia 10.3 kwa mwaka 2022/23.Hali hii ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na ukuaji mzuri wa mikopo kwa sekta binafsi uliofikia takribani asilimia 23,"imebainisha.

Pia, katika miezi saba ya kwanza ya mwaka 2022/23,MPC imebainisha kuwa, utekelezaji wa bajeti za Serikali umeendelea kufanyika kuendana na malengo. Mapato ya ndani yalifikia asilimia 97.1 na asilimia 96.1 ya malengo kwa Tanzania Bara na Zanzibar, mtawalia.

Mwenendo huu umechangiwa na kuimarika kwa mifumo ya usimamizi wa ukusanyaji mapato na utayari wa walipa kodi.

Aidha, matumizi ya Serikali yalifanyika kulingana na rasilimali zilizopo, sanjari na uhitaji wa kuimarisha miundombinu nchini na jitihada za Serikali za kuunusuru uchumi kutoka katika athari za misukosuko ya kiuchumi duniani kwa lengo la kuhakikisha ukuaji wa uchumi unakuwa shirikishi na endelevu.

"Sekta ya nje imeendelea kuathiriwa na misukosuko inayotokana na vita inayoendelea nchini Ukraine na athari za janga la UVIKO-19.

"Changamoto hizi zilipelekea kuongezeka kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje, kufikia dola za Marekani bilioni 5.2 mwaka ulioishia mwezi Januari 2023, ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani bilioni 2.6 mwezi Januari 2022, kutokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa katika soko la Dunia,"imebainisha sehemu ya taarifa ya kamati hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news