"Mungu akiamua kumfanyia mtu msaidizi wake (mke), hawezi kumpa mwanaume mwenzake kama msaidizi wake, hata kama watu wanasema tutadhamini harusi yako na huyo mume mwenzio ndiyo awe mke wako, huo ni msaada unaomvunjia mtu utu wake.”
Pia amesema, kuliko kupokea msaada wa aina hiyo, bora kuukata kabisa na kuendelea kuishi maisha yanayokubaliana na maongozi ya Mungu.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande (KiMPAB) anaeleza kuwa ni jukumu letu sote Watanzania kuendelea kulea watoto na vijana wetu katika malezi bora na yampendezayo Mungu, ambayo hayashabiani na mambo yanayokuzwa kwa kasi kutokana na matamanio ya wanadamu duniani.
Vivyo hivyo kuendelea kukemea na kukataa kwa nguvu zote matendo ambayo yanakwenda kinyume na mila, maadili na tamaduni zetu.
Mwambande anakusisitiza urejee katika neno la Mungu kupitia Biblia Takatifu, Mathayo 19:4-6...Yesu akawajibu, “Je, hamkusoma katika Maandiko Matakatifu kwamba Mungu aliyemuumba mtu tangu mwanzo alimfanya mwanamume na mwanamke, na akasema: ‘Kwa sababu hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake, ataungana na mke wake, nao wawili watakuwa mwili mmoja?’ Kwa hiyo, wao si wawili tena bali mwili mmoja. Basi, alichounganisha Mungu, binadamu asikitenganishe.” Endelea;
1. Mungu hutumia mtu, Mwovu hutumia mtu,
Mungu anajenga utu, Mwovu hubomoa utu,
Jichunguze wewe mtu, wewe kwa nani ni mtu,
Saidia jenga utu, apendavyo Mungu wetu.
2. Saidia jenga utu, apendavyo Mungu wetu,
Msaada wenye utu, huo ndio bora kwetu,
Ule uvunjao utu, katu haufai kwetu,
Bora tuvikose vitu, apendezwe Mungu wetu.
3. Bora tuvikose vitu, apendezwe Mungu wetu,
Hata wachukia watu, twaenda na Mungu wetu,
Zinune nchi za watu, wana kwao tuna kwetu,
Mungu ndiye dira yetu, Neno lake ndilo letu.
4. Mungu ndiye dira yetu, Neno lake ndilo letu,
Alivyotuumba watu, tuanze maisha yetu,
Aliona peke yetu, kwamba hatufai kitu,
Akatufanyia mtu, ni msaidizi wetu.
5. Akatufanyia mtu, ni msaizidi wetu,
Yule Adamu ni mtu, na msaidizi ni mtu,
Si Adamu yule mtu, usijechanganya vitu,
Hawa ndiye mtu wetu, jinsia yao si yetu.
6. Anajua Mungu wetu, yote mahitaji yetu,
Ngetaka tuumba watu, jinsia moja ya kwetu,
Tusingemfanya kitu, hata kujadili kitu,
Lakini liumba mtu, Adamu ni babu yetu.
7. Lakini liumba mtu, Adamu ni babu yetu,
Mwanaume yule mtu, twasoma vitabu vyetu,
Mwanamke kawa mtu, ni msaidizi wetu,
Huyu ndiye Mungu wetu, na sisi tu viumbe tu.
8. Huyu ndiye Mungu wetu, na sisi tu viumbe tu,
Sasa mbona sisi watu, twajifanyia ya kwetu?
Ambayo yajaa kutu, kinyume na Mungu wetu,
Haya yasitajwe kwetu, Sodoma Gomora katu.
9. Haya yasitajwe kwetu, Sodoma Gomora katu,
Kwamba kuna ndoa kwetu, jinsia moja ya watu?
Huo ni uovu kwetu, usikae kati yetu,
Tusijekubali katu, tumfwate Mungu wetu.
10. Tusijekubali katu, tumfwate Mungu wetu,
Wakate misada kwetu, acha tuishi kivyetu,
Watujue utu wetu, msingi ni Mungu wetu,
Tusidhalilishe utu, kinyume na Mungu wetu.
11. Tusidhalilishe utu, kinyume na Mungu wetu,
Na tusikubali katu, ushawishi wao kwetu,
Waache na mambo butu, hukumu yao si yetu,
Ndoa za kibali kwetu, jinsia bilia za watu.
12. Ndoa za kibali kwetu, jinsia mbili za watu,
Mwanaume huyo mtu, kuoa mke ni utu,
Mume kwa mume si utu, mke kwa mke si utu,
Kamwe yasifike kwetu, yasikubalike kwetu.
13. Kamwe yasifike kwetu, yasikubalike kwetu.
Na endapo kuna watu, wanaunga hayo kwetu,
Hukumu yao si yetu, kutoka kwa Mungu wetu,
Tumweshimu Mungu wetu, na zawadi kubwa kwetu.
14. Tumweshimu Mungu wetu, na zawadi kubwa kwetu,
Aliona huyu mtu, peke hatabaki mtu,
Kwa huo ubavu wetu, tukapata Hawa wetu,
Tuzidi mweshimu Mungu, Neno lake liwe letu.
(Warumi 1:17-32)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602