NA DIRAMAKINI
MKURUGENZI Mtendaji wa Redio Penuel ya Marangu mkoani Kilimanjaro ambaye pia ni Muhubiri wna Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba amesema, ndani ya miaka miwili ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa ambayo kwa kawaida yangeweza kuchukua miaka na miaka kuyatekeleza ikiwemo kurejesha kwa asilimia kubwa uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Temba amesema,mwaka juzi baada ya Rais Dkt.Samia kuingia madarakani aliuthibitishia umma na ulimwengu kuwa, vyombo vya habari ni mdau muhimu katika kuisadia Serikali yake kulisukuma gurudumu la maendeleo mbele.
"Mama yetu, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ni msikivu, mnyenyekevu na ni kiongozi asiyependa kuona mwingine anaumia kwa sababu ya jambo fulani, yupo tayari kusikiliza, kushauri na kutoa uamuzi panapostahili kwa mustakabali mwema.
"Na hayo ndiyo tuliyoyaona baada ya kutoa maagizo na maelekezo siku zile kuwa, wasaidizi wake wakashirikiane na wadau wa habari ili kupokea mapendekezo kuhusu marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, na nyingine ambazo zimeelezwa kuwa kandamizi.
"Hakika, tumeona mwezi uliopita hatua iliyofikiwa ni kusomwa kwa mara ya kwanza kwa mswada wa marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, hilo si jambo dogo kwa Taifa letu, ni jambo kubwa ambalo kwetu sisi wadau wa habari tunamshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt.Samia na Serikali yake.
"Tunatarajia maboresho mema yakifanyika, ustawi wa vyombo vya habari kuanzia mijini hadi vijijini utakuwa mkubwa. Vyombo vya habari vitazidi kuwa mdau muhimu wa kushirikiana na Serikali katika kuupasha umma taarifa mbalimbali za maendeleo,"amefafanua Temba.
Mwinjilisti Temba amesema, vyombo huru vya habari vina wajibu mkubwa wa kuripoti taarifa zinazohusiana na malengo mapya 17 ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa ambayo yamepangwa utekelezaji wake kukamilika ifikapo mwaka 2030.
Amesema, malengo hayo ambayo yanagusa kila Taifa mwanachama wa umoja huo ikiwemo Tanzania yanagusa kila nyanja, hivyo panapokosekana mfumo mzuri wa mawasiliano na kutoa taarifa kwa ajili ya kuupasha umma, itakuwa vigumu hayo yote kufikiwa.
Ikumbukwe kuwa,baada ya miaka kadhaa ya kupitishwa na kuridhiwa na mataifa zaidi ya 160, malengo mapya 17 ya Maendeleo Endelevu yanatajwa kugusa kila sekta ikiwemo kuutokomeza umaskini na njaa, usawa wa kijinsia na masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Temba amesema, maendeleo endelevu yanatoa fursa kwa nchi na Dunia kwa ujumla kutokomeza umaskini na kuhakikisha kwamba haki za binadamu zinaheshimiwa, mfano haki ya kupata elimu, afya, maji safi na salama, kazi nzuri, na amani.
Mwinjilisti huyo amefafanua kuwa, malengo haya ni mwendelezo wa hatua na mafanikio yaliyokwishapatikana, hivyo kukiwa na vyombo huru vya habari vitaendelea kutimiza wajibu mkubwa katika kuibua na kushirikisha mamlaka husika changamoto ambazo zimekuwa zikichangia baadhi ya mikwamo.
Wakati huo huo, Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba amempongeza Rais Dkt.Samia kwa kufanikisha maridhiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo siasa.
Amesema, miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt.Samia umedhirisha kuwa, ni kiongozi mpatanishi na mwenye shauku ya kuona kila Mtanzania bila kujali itikadi yake anaendelea kushiriki katika harakati za kulijenga Taifa letu.
Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka 2021 aliudhirishia ulimwengu kuwa, tasnia ya habari ni muhimu kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa.
Aidha, alianza kwa kuitaka Wizara ya Habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa huko nyuma huku akisisitiza wahusika wafuate sheria, jambo ambalo lilifanyiwa kazi hatua kwa hatua.
Pia, alitaka kanuni ziweke wazi makosa na adhabu zake ili kusiwe na ubabe kwa kuwa Serikali inaamini katika uhuru wa vyombo vya habari nchini.
“Nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni, lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, wafungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa vyombo vya habari, na kanuni ziwe wazi tusifungie vyombo vya habari kibabe,” Rais Samia aliagiza Aprili, mwaka jana katika hafla ya kuwaapisha makatibu na manaibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.
Aidha, miezi kadhaa baadaye Rais Samia alitoa maelekezo ya kufanyiwa marekebisho sheria za habari ambazo zinaonekana kuwa kikwazo katika taaluma hiyo.
Mheshimiwa Rais Samia aliyasema hayo Mei 3, mwaka jana wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti' katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.
“Nimeelekeza sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,"alielekeza Mheshimiwa Rais Samia.
Tags
Habari
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita
Miaka Miwili ya Rais Samia