NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema eneo la Mangapwani kwa sasa litakuwa kituo kikuu cha biashara ya mafuta nchini.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amezitaka wizara zinazohusika kuzielekeza kampuni zote za mafuta kuelekeza shughuli zote za mafuta kwenye eneo hilo.
“Serikali imekusudia kampuni zote za mafuta kushushia mafuta yao hapa Mangapwani,"amesema Rais Dkt.Mwinyi.
Dkt.Mwinyi amesema, bandari jumushi ya Mangapwani itahusisha bandari ya makontena itakayokuwa na gati ya urefu wa kilomita moja itakayohudumia sio Zanzibar pekee bali ukanda mzima wa Afrika Mashariki na makontena yatakayoshushwa bandarini hapo yaende hadi Dar es Salaam, Mombasa, Beira hadi Durban Afrika Kusini yakitokea Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mhe.Dkt.Amani Abeid Karume alipowasili katika viwanja vya Kampuni ya Mafuta ya United Petroleum (UP) Mangapwani kwa ajili ya uzinduzi wa Bohari ya Mafuta ya kampuni hiyo. (Picha na Ikulu).
“Tunataka bandari hii isihudumie Zanzibar pekee, tunataka Dar es Salaam, Mombasa, Beira hadi Durban Afika Kusini waitumie bandari hii,"ameeleza Rais Dkt.Mwinyi.
Bandari nyingine inayotarajiwa kujengwa eneo hilo, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameeleza ni bandari ya nafaka itakayohusisha ushushwaji wa bidhaa zote za vyakula ikiwemo mchele, maharage, mahindi, unga wa ngano na vyakula vingine ambavyo vitashushwa kwa muda mchache ili viwafikie wananchi kwa wakati, ujenzi mwingine ni wa bandari ya mafuta itakayohifadhi lita milioni 21.
Vilevile Dkt.Mwinyi alieleza Serikali inatarajia kuwa na mafuta ya kutosha na kuweka akiba ili Zanzibar iuze mafuta hadi nchi nyingine zisizokuwa na bahari na ujenzi wa bandari jumushi ya Mangapwani ni ufumbuzi wa changamoto zizilizopo kwenye bandari ya Malindi ambako meli hutumia siku 5, 7 hadi 10 kushusha mizigo hiyo, hali inayosababisha kupunguza uchumi wa nchi.
Pia amesema katika jitihada za Serikali kupunguza kero hizo, inatarajia kuzindua tenki kubwa la maji safi na salama Chakechake Pemba, lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni moja ambalo litakuwa la kwanza kwa ukubwa kwa Zanzibar nzima.
Ameihakikishia Serikali kwamba kampuni za Bakhresa zitaendelea kushirikiana na taasisi za Serikali zinazohusika na usimamizi wa majukumu yao ya kila siku na kuahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja wao.