Rais Dkt.Mwinyi atoa maagizo kwa mashirika ya umma

NA DIRAMAKINI

MASHIRIKA ya umma nchini yametakiwa kujitathmini kwa kujipambanua na kufungua ukurasa mpya wa ufanisi na uendeshaji kwa kuacha utendaji wa kusuasua, badala yake kuja na mikakati ya mageuzi na kuleta mabadiliko ya haraka yenye kutoa huduma za uhakika kwa wananchi na tija kwa Serikali.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akizungumza na viongozi wa mashirika ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar leo katika Ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu). 

Hayo yamesemwa leo Machi 8, 2023 Ikulu jijini Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi alipozungumza na watendaji wakuu wa mashirika hayo.

Dkt.Mwinyi amewataka kufanya marekebisho na maboresho ya kiutendaji watakapoona mazingira hayapo sawa kwa mustakabali wa mashirika hayo na Serikali kwa ujumla.

“Tunataka mashirika ya umma yaendane na kasi ya Awamu ya Nane kwa kufungua ukurasa mpya wa nidhamu, ukurasa wa kufanya kazi kwa bidii, ukurasa wa kuleta faida na kubwa kuliko lote ni huduma za uhakika kwa wananchi, wanachotaka kutoka kwetu Serikali ni huduma za uhakika, haitoshi kutetea tu maji na umeme iwe uhakika,”ameagiza Rais Dkt.Mwinyi.

Pia Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyataka mashirika yanayotoa huduma kwa wananchi kutafuta ufumbuzi wa haraka kutatua changamoto zinazowakabili na kuzigeuza kuwa fursa zenye tija kuleta mabadiliko chanya ikiwemo kubadili mifumo ya taasisi zao inapoonekana inafaa kwa maslahi ya umma.

Akiizungumzia Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Rais Dkt.Mwinyi ameeleza ni mashirika yanayotoa huduma na kugusa maisha ya watu moja kwa moja na kueleza haitoshi kutoa huduma pekee bila ya kuingiza faida kwa ajili ya uendeshaji wa mashirika hayo.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amewaelekeza watendaji wa mashirika hayo wajitathmini na huduma wanazowapatia wananchi na kwa nini wakose faida.

Aidha, ameyataka mashirika hayo kubadilika na kuwapatia wananchi huduma za uhakika kwa kuongeza kasi ya utendaji wao na wajiendeshe kwa mikakati ya uwekezaji ili wajiepushe na hasara na huduma zisizokidhi haja za wananchi. 

Hata hivyo, amewashauri kuja na mpango wa utekelezaji kwa kuangalia upya vyanzo vya matatizo waliyonayo na kuyatafutia ufumbuzi wa haraka.

Vile vile amewashauri ZAWA kuacha kutumia pampu zinazotumia umeme wa ZECO badala yake watumie za umeme wa jua ama sola ili kukwepa matatizo ya kuungua kila mara na kuwaondolea wananchi shida ya kukosa maji mara kwa mara.
Kwa mashirika yanayojitegemea,Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyashauri kutafuta mitaji kujiwekeza kwenye uzalishaji wenye faida kwa mustakabali wa mashirika hayo na Serikali kwa ujumla.

Akizungumzia baadhi ya mashirika ya umma yanayosuasua kwenye uzalishaji, Rais Dkt.Mwinyi aliwaeleza uwekezaji zaidi unahitajika ili yajiendeshe kibiashara na kuongeza Serikali inahitaji uwekezaji mkubwa kwa baadhi yao ili kuwapa nafasi ya kufanya vizuri.

“Ukipewa taasisi ukiona mambo hayapo sawa badilisha na kuweka ufanisi wenye tija kwa Serikali na maslahi kwa wananchi kama huna uwezo rudi tukusaidie,”ameshauri Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Amesema, hakuna sababu ya mashirika ya umma kupata hasara, alieleza kuna mambo kama Serikali imeshindwa hayafanya hakuna sababu ya kuendelea kupata hasara badala yake alishauri kupewa sekta binafsi kufanya ili serikali ipate faida na wananchi wapate huduma wanazostahiki kwa wakati unaofaa, akitolea mfano Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA). 

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, awali taasisi hiyo ilikuwa inapata hasara hadi Serikali ilikuwa ikitoa fedha za mishahara, lakini baada ya taasisi hiyo kushirikiana na sekta binafsi imekua ikiingiza faida kubwa.

Akiyazungumzia mashirika ya umma yanayojiendesha yenyewe kama Shirika la Bima, ZMUX na mashirika mengine, Rais Dkt.Mwinyi ameyashauri kutafuta mitaji na kujiendesha kibiashara hususani ZMUX ili kuendana na soko la ushindani.

Kuhusu shirika la nyumba, Dkt.Mwinyi alilielezea shirika hilo kwamba halina kasi ya kujiendesha kwa kukosa mtaji wa kukarabati na kufanya matengenezo ya nyumba tokea zilipojengwa mwaka 1972 hadi sasa.

“Mkisema mna nyumba Michenzani sio nyumba tena, Kilimani hamna nyumba, Kikwajuni zote zinahitaji ukarabati na kujengwa upya, ifike sehemu shirika hili liweze kukarabati, kujenga nyumba mpya na kufanyakazi kibiashara,” ameshauri Dkt.Mwinyi.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amelishauri shirika hilo kuja na mpango utakaoonesha mahitaji ya matengenezo na maboresho ya nyumba hizo ama kujenga mpya na kuonesha marejesho ya uwekezaji ili nyumba hizo zieendelee kuleta tija kwa wananchi na Serikali.

Rais Dkt. Mwinyi aliligeukia Shirika la Biashara la ZSTC na kulitaka kubuni mbinu endelevu za uzalishaji kwa kuhakikisha wananunua karafuu zilizosafishwa ili kukwepa hasara kwa Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news