NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema lengo la Serikali ni kuimarisha na kuweka mazingira mazuri wezeshi ya kibiashara katika uwekezaji hapa nchini.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Machi 10, 2023 katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Airport jijini Zanzibar wakati akizindua Muongozo wa Uwekezaji na Mfumo wa Kieletroniki wa Uwekezaji (ZIPA).
Dhumuni ni kurahisisha utoaji wa huduma kwa wawekezaji ikiwemo usajili na upatikanaji wa cheti cha uwekezaji wenye jina la"ZANZIBAR INVESTMENT ELECTRONIC WINDOW" (ZieW).
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema kukuza uwekezaji ni moja ya malengo makuu ya Serikali na kuleta Maendeleo.
Amesema, Serikali imedhamiria kuondoa vikwazo vyote vya kisheria na kimfumo vinavyozuia kuwapo kwa mazingira mazuri ya biashara kwa ajili ya uwekezaji nchini.
“Kwa kuanzia tayari tumeanza kufanya mabadiliko makubwa ZIPA (Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar) kwa kuimarisha zaidi kituo cha pamoja kutoa huduma za wawekezaji.
"Na jitihada hizo zimeanza kuzaa matunda ambapo kwa kipindi cha miaka miwili tayari miradi ya 226 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 3.5 ambazo zitatoa ajira 13500 imeanzishwa,”amesema.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema,muongozo wa uwekezaji Zanzibar unaelekeza taratibu zote muhimu za uwekezaji kwa wawekezaji kwa lengo la kukamilisha na kuharakisha usajili wa miradi ya uwekezaji.