Rais Dkt.Mwinyi:Msikubali kupotoshwa kuhusu Mji Mkongwe

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi waelewe dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Mji Mkongwe unabaki kama ulivyokuwa miaka mia mbili iliyopita na si kuubadilisha.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Machi 22, 2023 katika hafla fupi ya ufunguzi wa Jengo jipya la Hoteli ya Tembo, iliyofanyika Ukumbi wa Tembo House Hoteli,Shangani huko Mkoa wa Mjini Magharibi jijini Zanzibar.

Amesema, wapo wanaojaribu kupotosha kuwa Serikali ina lengo la kuubadilisha Mji Mkongwe kwa kuugawa na kubinafsishana akaeleza lengo ni kuwapa watu wenye uwezo kuyajenga majengo hayo, kuyatunza ili yaweze kudumu miaka mia mbili ijayo.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ametolea mfano Jengo la sasa la Tembo Hoteli lilikuwa Ubalozi wa Marekani mwaka 1831 na jengo lililozinduliwa leo kwa marekebisho ilikuwa ni Skuli mwaka 1944.

Pia, Rais Dkt.Mwinyi amewakaribisha wawekezaji waje kushirikiana na Serikali kurudisha hadhi ya Mji Mkongwe na kuujenga huku akitoa miezi mitatu kwa waliopewa majengo mbalimbali kwa ajili ya kuyarekebisha na kuyaendeleza wakishindwa Serikali itayachukua.

Ameeleza Serikali imeamua kutenga fedha kuhakikisha inaleta mfumo bora wa maji, mfumo wa kisasa wa umeme, huduma ya intaneti, ujenzi wa barabara katika Mji Mkongwe ili kuwa kivutio kwa utalii.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amemshukuru Mfalme wa Oman Sultan Haitham Bin Tariq M Said na Serikali yake kwa msaada wa dola za Kimarekani milioni 21 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Beit-al-Ajaib na kulirudisha katika hadhi yake na mkandarasi ameshapatikana na ujenzi utaanza hivi karibuni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news