Rais Dkt.Nabiijoshua:Mapenzi ya jinsia moja, dawa za kulevya na uhalifu havikubaliki nchini

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania (UMMT), Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala amesema, wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanayakemea matendo yote maovu ikiwemo vitendo vya uhalifu, mapenzi ya jinsia moja na dawa za kulevya.

Amesema,licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kuhakikisha inahimiza na kusisitiza maadili ya Mtanzania ambayo yanagusa moja kwa moja katika upande wa mavazi, lugha, kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano, kudumisha mila na desturi, ukarimu, upendo, heshima, na nidhamu,bado nafasi ya viongozi wa kidini ni muhimu sana ili kuyafikia hayo.

Dkt.Nabiijoshu ambaye pia ni Kiongozi wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania iliyopo mjini Morogoro amebainisha kuwa,viongozi wa kidini wakifanikiwa kushirikiana na Serikali bega kwa bega Taifa litazidi kuwa na watu wema ambao hawatayatamani mambo maovu.

Amesema, ukisoma Biblia Takatifu kitabu cha Tito 2:12-14, neno linasema, "12 Neema hiyo inatufundisha kukataa uovu na tamaa za dhambi, tupate kuishi maisha ya kiasi, ya haki na ya kumcha Mungu, katika ulimwengu huu.

"Wakati huo huo. 13 Tukingojea tumaini letu lenye baraka-kuja kwa utukufu wa Mungu wetu Mkuu na Mwokozi wetu, Yesu Kristo. 14 Yeye alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili atukomboe katika uasi wote, na kutufanya tuwe safi kwa ajili yake; na tuwe watu wake kabisa, ambao wana juhudi katika kutenda mema."

Pia amewataka viongozi wenzake wa dini nchini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kueneza habari njema kuhusu umuhimu wa wazazi na walezi kulea watoto kimaadili ili kuepusha vitendo viovu na visivyompendeza Mungu na katika jamii.

Katika hatua nyingine, Dkt.Nabiijosha amewaasa wazazi wote nchini kujitahidi kufuatilia maendeleo ya watoto wao wawapo nyumbani, shuleni pamoja na kuzungumza nao ili kuweza kutatua changamoto wanazopitia na kuwasaidia kutumia maarifa, ujuzi na vipaji walivyonavyo kwa maendeleo ya familia, jamii na Taifa.

Aidha, amesema viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika kuhimiza malezi bora ndani ya jamii kwa sababu wanasikilizwa na watu wengi, hivyo ni muhimu kutilia mkazo jambo hilo ili kujenga jamii salama na yenye maadili.

“Sisi viongozi wa dini nchini tunapaswa kushiriki kikamilifu katika kusaidia malezi ya watoto wetu, kwani iwapo watoto wetu wataandaliwa vyema kwenye misingi bora ya dini watakuwa ni tegemeo bora la taifa la leo na kesho.

"Tukishindwa kufanya hivyo leo basi tutalia kesho. Kwa sababu, Dunia hii ya utandawazi imekuwa na mapokeo mengi yenye tija na yasiyokuwa na tija, mapokeo yasiyokuwa na tija yameendelea kuwa na nguvu kubwa kwa sababu shetani anataka kila lililo baya liwe ndiyo kipaumbele cha kwanza kwa mwanadamu, lakini kwa uweza tuliyopewa na Yesu Kristo hakuna litakaloshindikana, yupo Mungu anayejibu maombi."

Rais Dkt.Nabiijoshua amewaomba wazazi na walezi ndani ya jamii zetu kuacha ukimya, "badala yake tuzungumze na watoto wetu na tuwafundishe kuhusu maadili, kwani kuporomoka kwake ndiyo imekuwa sababu ya vitendo viovu. Jukumu la malezi ni shirikishi, hivyo niwasihi wazazi, walezi, walimu na jamii kwa ujumla kushirikiana pamoja katika malezi ya watoto ili kujenga familia, jamii na Taifa bora na salama,"amefafanua Dkt.Nabiijoshua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news