Rais Dkt.Nabiijoshua:Rais Dkt.Samia ameleta mashangilio Sekta ya Habari

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania (UMMT), Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusababisha mashangilio katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya habari.

Amesema, ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt.Samia amefanya mambo makubwa ambayo yamerejesha imani, furaha na tabasamu kwa wengi ikiwemo Sekta ya Habari baada ya kuridhia mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

Februari 10, mwaka huu katika Mkutano wa Kumi wa Bunge jijini Dodoma, Serikali ilisoma kwa mara ya kwanza mswada huo.

"Kwa umuhimu kabisa,nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwani chini ya uongozi wa Serikali yake kila tabaka la jamii yetu kubwa ya Watanzania zaidi ya milioni sitini kote nchini wana mashangilio ya namna yao.

"Tumeona namna ambavyo anaunga mkono uhuru wa vyombo vya habari, na tayari ameridhia maboresho ya sheria ambazo huko nyuma zilionekana kuwa kikwazo katika sekta ya habari, hii ni hatua njema na Mungu ambariki sana,"amefafanua.

Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka 2021 aliudhirishia ulimwengu kuwa, tasnia ya habari ni muhimu kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa.

Aidha, alianza kwa kuitaka Wizara ya Habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa huko nyuma huku akisisitiza wahusika wafuate sheria, jambo ambalo lilifanyiwa kazi hatua kwa hatua.

Pia, alitaka kanuni ziweke wazi makosa na adhabu zake ili kusiwe na ubabe kwa kuwa Serikali inaamini katika uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni, lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, wafungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa vyombo vya habari, na kanuni ziwe wazi tusifungie vyombo vya habari kibabe,” Rais Samia aliagiza Aprili, mwaka jana katika hafla ya kuwaapisha makatibu na manaibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.

Aidha, miezi kadhaa baadaye Rais Samia alitoa maelekezo ya kufanyiwa marekebisho sheria za habari ambazo zinaonekana kuwa kikwazo katika taaluma hiyo.

Mheshimiwa Rais Samia aliyasema hayo Mei 3, mwaka jana wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti' katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.

“Nimeelekeza sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,"alielekeza Mheshimiwa Rais Samia.

Wakati huo huo, Dkt.Nabiijoshua amefafanua kuwa, "Vivyo hivyo, vyama vya siasa vinashangilia,wafanyakazi wanashangilia,wafanyabiashara wanashangilia,watu wa makundi maalumu wakiwemo walemavu wanashangilia,wavuvi,wakulima,wachimba madini, wanafunzi wa shule za msingi hadi kidato cha sita, wanafunzi wa vyuo vikuu,madhehebu ya dini hadi machifu na wengineo wote wanashangilia, yaani Mama ameligeuza Taifa lote kuwa la mashangilio, watu wanaifurahia nchi yao wenyewe, asante sana Mama.

"Mama unafanana na mvua ikiinyeshea nchi kila mmea hustawi na kutoa maua ya mashangilio tayari kwa kuzaa matumda.

"Japo najua mvua huotesha hata miba ikakuchoma,na wakati mwingine husababisha utelezi tunakuombea usianguke Taifa lote lipo upande wako kukutegemeza Mama yetu mwema, usirudi nyuma tunakuomba sana.Mama umefanana na jua wakati wa mavuno humpa kila mtu matumaini ya kuvuna alichopanda.

"Unafananishwa na kila kitu chema vitaijaza Dunia nikiviandika vyote itoshe kusema umekuja na kutokea kama mwanga gizani, umeangaza umeijua siri ya furaha ya Taifa lako.

"Umekuwa kama merikebu ya Nuhu inayompa salama kila mwenye hekima ya kuijua kesho yake, Mungu akubariki sana Mama yetu mwema.

"Kwa kuwa hii ni wiki ya Wanawake Duniani tunakuombea kwamba kupitia wiki hii MWENYEZI MUNGU aifanye nyota yako izuke tokea Chamwino Dodoma imulike kuwakilisha wanawake wote ulimwengu mzima na taa yako isizimike usiku wakuu wote wa Dunia na waseme Amina,"amefafanua Dkt.Nabiijoshua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news