Rais Dkt.Samia atoa maagizo kwa viongozi wa umma

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi kukumbushana misingi ya uongozi na taratibu za utendaji kazi Serikalini kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo.
Rais Dkt. Samia amesema hayo leo wakati akifungua Mkutano wa Faragha (Retreat) wa Mawaziri na Makatibu Wakuu uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa (AICC).

Aidha, Rais Samia ametoa wito kwa Viongozi hao kuwa na uelewa wa pamoja wa mtazamo na mwelekeo wa Serikali juu ya masuala mbalimbali.
Vile vile, Rais Samia amewataka Viongozi hao kutumia Mkutano huo kukumbushana na kuelekezana juu ya kutimiza ipasavyo wajibu walionao na dhamana walioibeba ya kuwatumikia wananchi.
Rais Samia pia amesema umakini na umahiri unahitajika kwa Viongozi katika kutumia na kusimamia rasilimali watu, vifaa na fedha za umma pamoja na kuwa na mipango na mikakati thabiti ya kutekeleza na kusimamia majukumu yao.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amewataka Viongozi hao kuyasemea mafanikio ya Serikali yaliyopatikana na kuwa wepesi kusahihisha kwa wakati upotoshaji unaofanywa dhidi ya Serikali kupitia watumishi na vitengo vya Habari vya wizarani.
Mkutano huo ambao unafanyika kwa mara ya kwanza tangu Rais Samia aingie madarakani, una lengo la kuwakumbusha Viongozi kuhusu dhana ya uongozi na sifa za kiongozi bora na utaratibu wa utoaji wa maamuzi ya kisera ndani ya Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news