Rais Dkt.Samia atoa pole kwa Wamalawi kutokana na maafa yaliyotokana na Freddy

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Jamhuri ya Malawi, Mheshimiwa Lazarus Chakwera na watu wa Malawi baada ya kimbunga Freddy kusababisha maafa nchini humo
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia leo Machi 15, 2023 amesema, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasimama pamoja na Wamalawi katika kipindi hiki kigumu huku akiwaombea waliofariki ili Mwenyenzi Mungu awapumzishe salama, na kuwatakia majeruhi kupona haraka.

Salamu hizo zinajiri ikiwa, idadi ya vifo nchini Malawi vilivyotokana na kimbunga Freddy imeongezeka kufikia watu 190 siku ya Machi 14, 2023.
Kwa mujibu wa VOA na AFP, vifo hivyo vilitokea baada ya dhoruba hiyo iliyovunja rekodi kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi wakati kimbunga hicho kilipopiga kwa mara ya pili eneo hilo la Kusini mwa Afrika katika kipindi cha chini ya wiki tatu.

Aidha,baada ya kusababisha maafa nchini Australia mapemwa mwezi Februari, kimbunga Freddy kilivuka Bahari ya Hindi, na kutua Kusini Mashariki mwa Afrika mwishoni mwa mwezi Februari. Mwishoni mwa wiki iliyopita kimbunga hicho kilirejea eneo hilo na kupiga kwa mara ya pili.

"Idadi ya watu waliofariki imeongezeka kutoka watu 99... hadi 190, huku watu 584 wakiwa wajeruhiwa na 37 wameripotiwa kutojulikana walipo," Idara ya Masuala ya Kukabiliana na Majanga nchini Malawi ilisema katika taarifa yake.
Picha na CNN.

Wafanyakazi wanaotoa misaada walisema idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka."Hali ni mbaya sana," alisema Guilherme Botelho, mratibu wa mradi wa dharura wa shirika la kujitolea la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF).

"Kuna majeruhi wengi, waliojeruhiwa, waliopotea au kufariki, na idadi hii inatarajiwa kuongezeka katika siku zijazo."

Watu wengi wameangamia kutokana na maporomoko ya matope yaliyozisomba nyumba katika mji mkuu wa kibiashara wa Blantyre.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news