Rais Ruto atoa maagizo kwa watumishi wa umma

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Kenya, Dkt.William Ruto amewataka watumishi wa umma kuwahudumia Wakenya kwa heshima na unyenyekevu.

Pia amesema, lazima washauriane mara kwa mara na wakubali kufahamishwa ili waweze kusaidia kuipeleka nchi mbele.

"Ni wakati wa kuja pamoja, na kufanya kazi pamoja, bila kujali upendeleo wetu wa kisiasa, kutoa huduma zetu zinazohitajika sana kwa watu," alisema.
Mheshimiwa Rais Ruto aliyasema hayo hivi karibuni wakati akiwaapisha Makatibu Wakuu 50 walioteuliwa karibuni, katika Ikulu ya Nairobi.

Miongoni mwa waliokula kiapo ni Evans Kidero, Millicent Omanga, Denis Itumbi, Nicholas Gumbo,Isaac Mwaura, Cate Waruguru, Samuel Tanui na Charles Njagua.

Rais Ruto aliwaambia kwamba, anatarajia kuona taaluma, ujuzi, talanta,nguvu na shauku katika vitendo ili kusukuma ajenda ya maendeleo ya Taifa mbele.

Katika hafla hiyo, pia Makamu wa Rais, Rigathi Gachagua, Mke wa Rais, Rachel Ruto,Kiongozi Mkuu wa Baraza la Mawaziri, Musalia Mudavadi,Mawaziri, Makatibu Wakuu, wabunge ni miongoni mwa viongozi wengine, waliohudhuria.

Rais alibainisha kuwa, maendeleo yanafanywa ili kuinua maisha ya Wakenya, lakini mengi zaidi yatafanywa ikiwa viongozi hao watadumisha umoja, mshikamano na kila mmoja kuwajibika katika nafasi yake.

“Pia tuko njiani kufikisha mbolea ya bei nafuu kwa wakulima. Lengo letu ni kuzalisha zaidi ili kulisha zaidi na kupunguza umaskini nchini,”alisema Rais Ruto ambapo alitangaza kuwa awamu ya kwanza ya Hustler Fund imetoa shilingi 24 bilioni kwa wakopaji milioni 19.

Rais alieleza kuwa, Serikali iko mbioni kupeleka nyumba mpya 200,000 mwaka huu, ikiwa ni jitihada za Serikali kuhakikisha inaziba pengo la mahitaji ya nyumba nchini.

“Hivyo, lazima tufanye kazi kwa bidii, tuwatumikie wananchi kwa bidii tunapoendeleza Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi,"alibainisha.

Hata hivyo, aliwataka Makatibu Wakuu na watumishi wengine wa umma kutambua kuwa, wanapaswa kuhudumu kwa kuzingatia vigezo vya sheria.

“Tumejitolea kwa Kenya ambayo imejengwa juu ya msingi thabiti wa utawala wa sheria. Sisi sote tupo chini ya Katiba, bila kujali msimamo wetu katika jamii,"alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news