Serikali kuwanyanganya ardhi waliopewa kuwekeza wakashindwa Zanzibar

NA SABIHA KEIS

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema itawanyanganya umiliki wa ardhi wenyenji na wageni ambao walipewa kwa ajili ya kuwekeza, lakini wameshindwa kuyaendeleza hivyo sheria itachukua mkondo wake bila ya kumuonea mtu muhali.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu waziri Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar, Juma Makungu Juma huko Wilaya ya kati Mkoa wa Kusini Unguja katika ziara maalumu ya kuyatembelea maeneo ambayo wageni na wenyeji walipewa kwa ajili ya kuwekeza, lakini bado hawajawekeza.

Amesema kwamba, Sheria ya Umiliki wa Ardhi, Sheria Namba 12 ya mwaka 1992 kifungu Namba 48 (1a) kinaeleza ukiukaji wa ukodishwaji ardhi (Violetion of the Restrictions in a lease) hivyo wizara yake itahakikisha inafyata sheria kwa wawekezaji wa kigeni na wazawa ambao walipewa maeneo kwa ajili ya uwekezaji na kutoyaendeleza kwa muda uliowekwa.

Alifahamisha kwamba lengo la ziara yake ni kuangalia pamoja na kuyatambua maeneo yote ya ardhi ambayo yametolewa na Serikali na kuwapa watu kwaajili ya kuekeza lakini bado wahusika wameshindwa kuyaendeleza kwa muda uliyowekwa.

Amesema, Serikali haina nia ya kumdhulumu mtu, lakini kuna baadhi ya watu wameshindwa kuyaendeleza maeneo ambayo walipewa hivyo hakuna sababu ya kuwaachia umiliki wa ardhi mwekezaji huyo kwa sababu hakuna faida inayopatikana.
Aidha, Naibu Waziri Juma ametoa wito kwa wawekezaji wote waliopewa maeneo ya ardhi kuhakikisha wanayaendeleza maeneo hayo, kwani uwekezaji hutoa fursa nyingi za ajira kwa vijana pamoja na kuiongezea nchi mapato.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji Kamisheni ya Ardhi Khamis Juma Khamis amefahamisha kuwa zoezi hilo linatarajiwa pia kufanyika katika maeneo yote ya uwekezaji ambapo hapo awali Kamisheni ya Ardhi ilishatoa taarifa kwa wawekezaji wote waliopatiwa lease ya ukodishwaji kuyaendeleza maeneo yao vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.

"Tulishawahi kutoa indhari kupitia vyombo vya habari kwa wawekezaji wote kuhakikisha wanayaendeleza maeneo yao, lakini ziara ya leo tumebaini kuwa kuna maeneo bado yako vilevile hayajaendelezwa chochote, hivyo kwa sasa kinafuata ni utaratibu wa kisheria utatumika,"amesisitiza Khamis.

Naye Sheha wa Shehia ya Uroa, Muhsini Amour Adam ametoa wito kwa wawekezaji ambao mpaka sasa bado hawajayaedeleza maeneo yao kuitumia fursa hiyo kwa kuyaendeleza katika shughuli mbalimbali zikiwemo utalii kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.

Maeneo yaliyotembelewa na kuonekana kuwa bado hayajaendelezwa hadi sasa ni pamoja na Pongwe,Uroa na Marumbi. Aidha, kwa upande wa Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja ziara kama hiyo inatarajiwa kufanyika Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news