SERIKALI YASEMA INAZINGATIA MASUALA YA KIJINSIA NCHINI

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha kwamba masuala ya usawa wa kijinsia kwa ujumla yanapewa kipaumbele na wanawake wanashirikishwa kwenye masuala ya kidijitali, uvumbuzi na teknolojia nchini.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Sarah Mwaipopo (aliyesimama katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wanawake wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali mara baada ya kumaliza kikao kifupi kwa ajili ya kujadili kauli mbiu ya Siku ya Wanawake Duniani kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi hiyo jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi.Sarah Mwaipopo alipokuwa akiongea na wanawake wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yenye kauli mbiu “Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia ni Chachu katika kuleta Usawa wa Kijinsia”.

Amesema kauli mbiu ya mwaka huu inawataka wanawake kuhakikisha kwamba katika safari ya kuelekea kwenye usawa wa kijinsia ngazi zote wanakuwa ni wabunifu na wenye uwezo na maarifa ya kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia. 

Aidha, wanawezeshwa kutumia mifumo na nyenzo mbalimbali za kidijitali na kupatiwa mafunzo ya masuala ya kiteknolojia.

“Kauli mbiu hii inatuhamasisha sisi wanawake kuhakikisha kwamba tunaitumia siku hii kama fursa ya kushiriki kikamilifu kuainisha mafanikio, changamoto na mahitaji yetu yanayohusiana na masuala ya kidijitali na kiteknolojia na kushauriana namna bora ya kuandaa mikakati ya utekelezaji, “ amesema Mwaipopo.Wanawake kutoka Ofisi Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakiwa wameshika bango la Ofisi hiyo wakati wakiandamana kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani katika maandamano yaliyofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,1977 inasisitiza masuala ya usawa wa kijinsia kwenye nyanja zote sambamba na sheria mbalimbali, Kanuni na sera ambazo Serikali inasimamia na kufanikisha utekelezaji wake.

“Serikali imesaini mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa ambayo nayo inasisitiza masuala ya kijinsia katika maeneo yote ikijumuisha masuala ya uvumbuzi na teknolojia.Sote tunafahamu ya kwamba tupo katika karne ya 21 ambayo kila kitu kinafanyika kwa kutumia teknolojia na nyenzo za kidijitali kwa hiyo hakuna nchi inayoweza kuendelea au kupata maendeleo bila ya kuwa na teknolojia,‘‘amesema Mwaipopo.

Amewataka wanawake katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuhakikisha wanashiriki na kushirikishwa kwenye masuala ya kiteknolojia kwa kupatiwa fursa kwa kadri bajeti na rasilimali fedha inavyoruhusu ili kuwawezesha kutekeleza vyema majukumu ya usimamizi na uendeshaji mashauri ya madai na usuluhishi katika ngazi zote ambazo mashauri husika yanapokelewa, kusajiliwa, kuandaliwa nyaraka na kupatiwa uwakilishi Mahakamani.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Sarah Mwaipopo (aliyesimama katikati) akiongoza maandamano ya wanawake kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Dar es Salaam kuelekea Uwanja wa Mashujaa kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mkoa wa Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, Watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, walishiriki maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwenye Viwanja vya mnazi mmoja Dar es salaam. 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makala ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mkoa wa Dar es Salaam amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema katika mkoa wake ameendelea kuwawezesha wanawake mkoani humo ili kuhakikisha wanasimama vyema katika nyanja zote ikiwemo masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makala ambaye alikuwa Mgeni Rasmi akizungumza na watumishi wa Serikali, taasisi binafsi, asasi za kiraia pamoja na wananchi walioshiriki Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani iliyofanyika kimkoa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa kufikia mwezi Machi mwaka huu, Serikali mkoani Dar es Salaam imefanikiwa kutoa mikopo nafuu kwa wanawake wanaofanya shughuli mbalimbali mkoani humo ambapo katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2022/2023 kiasi cha shilingi bilioni 13.9 zilitengwa na kutolewa kwa wanawake ikiwemo vijana na wenye ulemavu.

Makala ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kujiunga kwenye vikundi na kuvisajili ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo katika halmashauri zote za jiji la Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Wanawake wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Celina Togocho akipuliza vuvuzela kuashiria kuanza kwa maandamano ya Madhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

“Natoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kujiunga kwenye vikundi vilivyosajiliwa ili waweze kunufaika na fedha mbalimbali ndani ya halmashauri zote za jiji la Dar es Salaam,” alisema Mhe. Makala.

Kuhusu umuhimu wa maadhimisho haya Mhe. Makala ameeleza kuwa maadhimisho haya yanajenga hamasa na ushiriki katika kuchangia na kuleta usawa wa kijinsia na na uwezeshaji wa wanawake katika kutekeleza masuala mbalimbali ikiwemo kuimarisha mifumo ya kijamii na hamasa kwa jamii kwa minajili ya kuleta usawa wa kijinsia, kuongeza msukumo wa ushiriki wa wanawake katika uongozi na vyombo vya vya kutoa maamuzi, kubadilisha Taarifa na uzoefu kuhusu masuala ya jinsia na uwezeshaji wanawake , utekelezaji wa maazimio, mikataba na itifaki za kimataifa ambazo nchi yetu imeridhia.

Faida nyingine za maadhimisho haya ni kushirikisha na kutoa mrejesho kwa wananchi kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mikataba ya kimataifa na kikanda pamoja na mipango ya sera za kitaifa, kisekta kuhusu masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wananchi kiuchumi na kijamii.

Amefafanua kuwa nchi yetu pia inatambua umuhimu na mchango wa mwanamke katika siasa, jamii na uchumi hivyo mwaka huu nchi yetu inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Wanawake kama ambavyo na sisi mkoa wa Dar es Salaam tunaadhimisha leo siku hii muhimu.
“Kwa sasa Siku ya Wanawake Duniani inaadhimishwa kila baada ya miaka mitano, wakati huu kila mkoa unaadhimisha pekee yake kama ambavyo tuko hapa kuadhimisha shughuli hii,” alisema Mhe. Makala.

Akizungumzia kauli mbiu ya mwaka huu inayosema, “Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia: Chachu katika kuleta Usawa wa Kijinsia”, Mhe. Makala amesema kuwa kauli mbiu hii inaenda kuelimisha, kuhimiza, na kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa uwepo wa haki na usawa katika jamii katika kufikia malengo endelevu hivyo wadau mbalimbali wa maendeleo ya wanawake nchini, viongozi wa Serikali, siasa, dini, na asasi za kiraia tuungane wote kwa pamoja katika kutekeleza kauli mbiu hii.
Ifahamike kuwa Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani ilianza mwaka 1911 kufuatia maandamano ya Wanawake wafanyakazi wa viwandani nchini Marekani waliokuwa wakipinga mazingira duni ya kazi kama vile ukosefu wa huduma za kijamii na unyanyasaji katika ajira, hivyo kuendelea kuadhimisha Siku hiyo ni kuenzi mchango wa wanawake katika Ujenzi wa Taifa.
Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani katika mkoa wa Dar es Salaam yamefanyika katika Uwanja wa Mnazi Mmoja yakitanguliwa na maandamano ya wanawake kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwemo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, mashirika binafsi na asasi za kiraia yaliyoanzia katika Viwanja vya Mashujaa vilivyopo eneo la Mnazi Mmoja Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news