NA MWANDISHI OWMS
WAKILI Mkuu wa Serikali amekitaka Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) kuendelea kuwajengea uwezo wanachama wake ili waweze kufanya kazi kwa weledi na kushirikiana miongoni mwao hasa katika kazi zizinazohitaji wabobezi wa maeneo mahususi ya sheria.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (aliyesimama katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Kaimu Mtendaji Mkuu wa TLS, Bi. Mariam Othman (wa pili kutoka kulia) na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Sarah Mwaipopo (wa pili kutoka kushoto) pamoja na viongozi wengine wa Ofisi hizo mara baada ya kikao kilichofanyika kwenye Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam.
Hayo yameelezwa na Dkt. Boniphace Luhende, Wakili Mkuu wa Serikali akiwa Ofisini kwake leo alipokutana na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Chama cha Mawakili Tanganyika aliyefika kwa ajili ya kujitambulisha.
Amesema kuwa changamoto iliyopo kwa sasa ni kuwa Mawakili wachache sana wamejikita katika eneo moja la ubobezi. Jambo hili linawanyima Mawakili fursa ya kushiriki katika miradi ya kimkakati iliyopo hapa nchini kwa sasa.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (aliyesimama kushoto) akimkabidhi Jarida na Kalenda ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Kaimu Mtendaji Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) Bi. Mariam Othman ambaye amemtembelea kiongozi huyo kwa lengo la kujitambulisha mapema leo tarehe ofisi kwake jijini Dar es Salaam.
Dkt. Luhende amesema kuwa anafahamu namna TLS inavyoshirikiana na taasisi za Sekali na kuipongeza Menejimenti ya TLS kwa kufanya kazi vizuri na kwa kutambua kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ni wadau wa TLS.
‘‘Mdau mkubwa wa TLS ni Serikali kwa sababu ndio muajiri mkubwa na wanachama wengi wa TLS wanatoka hapo na ndio ina watu wengi na miradi mikubwa hivyo huwezi kuikwepa Serikali,“ amesisitiza Dkt. Luhende.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende akizungumza na Kaimu Mtendaji Mkuu wa TLS, Bi. Mariam Othman pamoja na ujumbe wake (hawapo pichani) kuhusu masuala mbalimbali yenye lengo la kuongeza ushirikiano kati ya Ofisi hizo mbili kwenye kikao kilichofanyika leo kwenye Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serili, Dar es Salaam.
Amewataka TLS kufanya utafiti kwenye mada wanazozitoa kwenye semina mbali mbali ili ziendane na mahitaji ya wanachama wao ili waajiri waone umuhimu wa kuwapeleka Mawakili kuhudhuria semina hizo.
Dkt. Luhende amesema kuwa TLS wana jukumu la kuhakikisha kwamba Mawakili wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili, weledi na miiko ya taaluma yao ili kuitendea haki sekta ya sheria nchini na wadau wanaowahudumia.
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa TLS Bi. Mariam Othman ameiomba Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuendeleza ushirikiano uliopo kwa kuendelea kuwafanya Mawakili wa Serikali wanachama hai wa TLS na kuendelea kushiriki katika chama hicho.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Sarah Mwaipopo (aliyesimama kushoto) akimkabidhi Kaimu Mtendaji Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) Bi. Mariam Othman zawadi ya Kalenda ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali mara baada ya kumalizika kikao baina ya viongozi hao. Kikao hicho kimefanyika mapema leo katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali iliyopo Jijiji Dar es Salaam.
“Tumeona ni vema kufika kuonana na wewe ili tujitambulishe na kuomba ushirikiano huo kwa kuwa Mawakili wengi ni wanachama wa TLS,“ amesema Bi. Othman.
Pia, Bi. Othman ameomba Mawakili wa TLS ambao sio waajiriwa Serikali kupewa nafasi ya kuteuliwa kuwa wasuluhishi katika mashauri ya usuluhishi yanayohusisha taasisi za umma.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (aliyesimama katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Kaimu Mtendaji Mkuu wa TLS, Bi. Mariam Othman (wa pili kutoka kulia) na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Sarah Mwaipopo (wa pili kutoka kushoto) pamoja na viongozi wengine wa Ofisi hizo mara baada ya kikao kilichofanyika kwenye Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Udhibiti Ubora na Menejimenti ya Kesi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Mercy Kyamba ameishukuru TLS kwa kuendelea kufanya kazi kwa vitendo na kudumisha ushirikiano na Ofisi hizi mbili na kuwaomba kuangalia jinsi ya kuwafutia Mawakili wa Serikali ambao ni wanachama wa TLS malimbikizo ya ada za uanachama.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Mashauri ya Madai ya Ndani wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, ndugu Deodatus Nyoni amesema kuwa TLS iweke utaratibu wa kuwapatia cheti cha uzoefu cha uendeshaji wa mashauri Mawakili wa Serikali wanaohudhuria mafunzo yanayoendeshwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali. Pia alishauri TLS kutambua Mawakili wanaoendesha mashauri kwenye Mahakama za Rufaa kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (aliyesimama katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Kaimu Mtendaji Mkuu wa TLS, Bi. Mariam Othman (wa kwanza kushoto) pamoja na Kaleb L. Gamaya ambaye ni Mtendaji Mkuu anayemaliza muda wake. Viongozi hao wamemtembelea Wakili Mkuu wa Serikali mapema leo kwa lengo la kujitambulisha walipokutana Ofisini kwake jiini Dar es Salaam.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Sarah Mwaipopo.