TRC yatakiwa kuwekeza kwenye karakana

NA MWANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe.Seleman Kakoso ameitaka TRC kuwekeza kwenye Karakana ili iweze kuzalisha wataalamu na vifaa ambavyo kwa sasa vinaletwa kutoka nchi za nje kwa ajili ya ujenzi,ukarabati na utekelezaji wa miradi ya reli nchini.
Ameyasema hayo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilipotembelea na kukagua karakana ya ukarabati wa vichwa vya Treni ya kawaida-MGR iliyopo mkoani Morogoro

“Wekeni bajeti nzuri ambayo itasaidia karakana kutengeneza vifaa ambavyo vinawezekana kutengenezwa hapa nchini, ukizingatia tunaelekea kipindi cha bajeti kuu ya Serikali, hivyo shirikianeni na wizara na sisi kama kamati tupo tayari kuwaunga mkono,”amesisitiza Mhe. Kakoso

Kwa upande wake Naibu Waziri Sekta ya Uchukuzi, Mhe.Atupele Mwakibete amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inaeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukarabati vichwa na mabehewa ya treni ili kuboresha huduma ya Reli ya kati nchini ambapo Juni 30, 2021 Serikali ya Awamu ya Sita iliiingia mkataba wa Dola za Kimarekani milioni 10.5 na Kampuni ya SMH RAIL kutokea nchini Malaysia kwa kutumia karakana ya Morogoro kufanya ukarabati mkubwa wa vichwa vya treni ya kawaida-MGR.

‘‘Ukarabati huu ni wa kufufua vichwa vya treni ya kawaida tisa vya reli ya kati ambapo viwili ni vya njia kuu na saba ni vya sogeza na unaohusisha ufungaji wa vipuri vipya, injini mpya, bodi mpya na unatarajiwa kukamilika ifikapo Julai,2023,” amesisitiza Mhe. Mwakibete.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania,Amina Lumuli amesema Karakana ya Vichwa vya Treni Morogoro inakumbana na changamoto mbalimbali kama vile ugumu wa upatikanaji vipuri kwa wakati, pamoja na upungufu wa rasilimali fedha.

Shirika la Reli Tanzania lina jumla ya vichwa vya treni ya kawaida-MGR 59,vichwa 43 vikiwa vya njia kuu na 16 vikiwa vya Sogeza na kati yake vichwa vinavyofanya kazi ni 44 ambapo vichwa 30 ni njia kuu na vichwa 14 sogeza na limeendelea kukuza wataalamu wa ndani kwa kuwapatia ujuzi wa kimasomo ndani na nje ya nchi ili kuendana na teknolojia ya kisasa na mabadiliko ya mara kwa mara ya vipuri kwa minajili ya kuboresha usafiri wa reli ya kawaida nchini kwa maslahi ya Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news