NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa William Ruto amesema hatakubali utovu wa nidhamu huku akisisitiza utii wa sheria bila shuruti nchini humo.

"Tunapofurahia haki zetu kama watu binafsi, ni lazima tuwe waangalifu ili kuhakikisha kwamba hatukanyagi haki za wengine."
Mheshimiwa Rais Ruto ameyasema hayo hivi karibuni katika Ikulu ya Nairobi, ambapo aliongoza hafla ya kuapishwa kwa Wakili Mkuu wa Serikali, Shadrack Mose.

"Toa uongozi na uhakikishe kuwa Serikali inapata mwongozo sahihi wa kisheria ili kutekeleza majukumu yake," alifafanua. Alimuomba Mwanasheria Mkuu kutetea mfumo unaofaa wa kisheria ambao utaimarisha ushindani wa Kimataifa wa Kenya.
“Ni dhamira yetu kuhakikisha kwamba tunavutia uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni kadri tuwezavyo. Tunataka kukopa kidogo na kufanya zaidi kwa ajili ya nchi."
Rais alibainisha kuwa, mara tu Kenya itakapopata imani ya wawekezaji wa kimataifa, itajiondoa katika ukopaji usio wa lazima. Alimwambia Bw.Mose anapaswa kuhakikisha kuwa Serikali inapata uwakilishi bora wa kisheria katika hatua zote.