Viongozi wa dini wanaojikweza, kujivika vyeo wamtoa machozi Nabii James Inyassy Nyakia

NA DIRAMAKINI

KIONGOZI wa Kanisa la SOJA MEGA ONE lililopo Mwenge Mpakani jijini Dar es Salaam,Nabii James Inyassy Nyakia amewataka watumishi wa Mungu kujinyenyekeza mbele za Mungu na kuacha tabia ya kujikweza huku wengine wajivika vyeo vingi ambavyo haviendani na hadhi zao.

Nabii Nyakia ametoa rai hiyo ikiwa siku za karibuni wameibuka watu wengi wanaojiita watumishi wa Mungu ambao wamekuwa wakitenda mambo kinyume na ilivyo maamrisho na miongozo ya Mungu kupitia Biblia Takatifu.

"Ukisikia mtu anajitaja kwa vyeo vingi sana mtandaoni badala ya wanaomfahamu au wanaoiona kazi yake kumtaja ujue huyo hamna kitu na kuna namna haiko sawa na mfuatilie utaujua mwisho wake kuwa cheo alikitaka ili kuongeza heshima sio utendaji.

"Ukiwa na utendaji mzuri, vyeo kwako ni kitu kidogo sana ambacho utaitwa na wanaoiona kazi yako na sio unavyojiona wewe.Siku hizi neno Askofu limepoteza heshima yake.

"Neno Daktari limehamia makanisani na zamani tulizoea kuliona kwa wanazuoni wa vyuo vikuu, lakini siku hizi lazima mtu akijitaja majina aweke na neno “PhD”.

"Unaanza kujiuliza, hivi hii PhD inabeba thamani gani katika huduma ya mtu au katika familia yake? Kitendo cha mtu kutoa pesa tu na kuletewa PhD mezani kimeanza kudhalilisha thamani ya PhD hasa makanisani.

"Unajua utamsikia mtu ana PhD, lakini hata kuandaa taarifa ya kanisa ya mwezi hawezi na wala kanisa lake halina mpango kazi wa miaka 5, 25 au 50? Onyesha thamani ya elimu yako katika utendaji wako, sio kwa jinsi watu wanavyokuita na kukusifia huku kichwani mwako ukitambua kuwa mimi kichwa changu hakina uwezo wa kuitwa Daktari wala siwezi ku-hold PhD.Lakini, haya ni majira, nayo yatapita tu,"amefafanua Nabii Nyakia.

Mbali na hayo, Nabii Nyakia amefafanua kuwa, siku za karibuni watu wanaojiita watumishi wa Mungu wamekuwa wakitumia muda mwingi mitandaoni, kuwakashifu, kukejeli na kuwatukana wengine jambo ambalo halina afya mbele za waumini, Taifa na kwa Mungu.

"Kuaibishana na kujisifia imekuwa jambo la sifa sana, vivyo hivyo, kuchambana na kukejeliana ni sehemu ya sifa. Matusi ni ujanja na kuvunjiwa heshima ni sheria na kudharauliana imekuwa kanuni, yaani unaweza kuheshimiwa na washirika kuliko mtumishi mwenzako, hata kama anayafahamu mabaya yako ndiye atakayekuwa wa kwanza kuyaanika mitandaoni tena kwa ukubwa sana.

"Kuna makundi ya kuongoza mitume na manabii, lakini huoni jinsi yanavyoweza kudadavua jambo hili kwa kulikemea au kuchukua hatua stahiki zaidi utaona aibu kwa kuzidi kuaibishwa na wao pia.

"Yaani ni vema ukamweleze mlevi siri yako ya kimadhabahu kuliko mtumishi mwenzako, atakuvua nguo tena ikibidi ataita mpaka press conference ili vyombo vya habari viitangazie Dunia. Hapo ndipo tulipofikia?.

"Ukitaka kufanikiwa kihuduma punguza idadi ya marafiki ambao ni watumishi wenzako, ikibidi ongeza idadi ya watu wa kawaida, utaliponya sana kanisa lako na kuilinda hadhi yako wakati wa anguko lako maana watakuhifadhi kuliko jinsi leo hii watumishi wanavyochambana.

"Leo hii ukiongea na mtumishi mwenzako jua kama hakurekodi basi anakutafutia umbea au anataka kukujua ili ayafahamu madhaifu yako ipo siku akuanike mitandaoni. Ni aibu sana kwa sasa kumwamini mtumishi mwenzako ukamweleze jambo la ndani yako linalokuumiza ili akuombee au akukutakishe na mkeo kama mshauri.

"Ipo siku atamlala mkeo...tuombeane tu wala tusitukanane maana huijui kesho yako atakusaidia nani na utakumbwa na nini. Wewe kuyajua madhaifu yangu usinitangaze mitandaoni. Mimi ni binadamu kama wewe. Nina familia, nina watu nyuma yangu, nina ndugu na marafiki wako mitandaoni. Mungu atusaidie sana.

"Hakika, mimi sio kitu ila thamani yako kwangu iwe kubwa kuliko thamani yangu kwako kuwa kubwa. Heri niwe takataka kwako, lakini wewe uwe marashi kwangu.

"Heri unikabe, lakini mimi nijikalie kimya sana. Ni heri wewe uniitie press conference na kunisema vibaya, lakini mimi niingie kukuombea na kufanya toba juu yangu maana mwisho wetu utabeba hatma yetu, lakini jamani uzeeni kwetu tutasaidiana kweli?.

"Nimeona haya tu kwa ujinga wangu, lakini nakua hata mpumbavu kuongea mbele ya wenye hekima na mpumbavu hutukanwa ili afundishike.Heri niwe mpumbavu utukane wee...labda nitajifunza jambo jipya kupitia matusi unayojitukana au jinsi unavyonidhalilisha.

"Kinyonge machoni pa watu chaweza kuheshimiwhwa mbele za Mungu.Nakuombea kabla sijajiombea, heri kunyenyekea kuliko kuwa na sauti kumbe ulistahili kukaa kimyaa.Sio kila mnenaji ananena yatokayo kwa Mungu, nakaa kimyaa,"amefafanua Nabii Nyakia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news