Vipers yafanya mazoezi ya mwisho kuikabili Simba leo

NA DIRAMAKINI

KLABU ya Vipers kutoka Kitende-Wakiso karibu na Entebe Express Highway nchini Uganda imefanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuvaana na Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam leo katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini humo.

Mazoezi hayo yamefanyika ikiwa tayari wenyeji wao, Simba SC walianza kujinoa tangu mapema katika Uwanja wa Mo Simba Arena ili kujiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers utakaopigwa leo.

Kikosi cha Simba, kiliingia kambini huku wachezaji wote wakishiriki mazoezi isipokuwa Kibu Denis ambaye alifanya peke yake chini ya uangalizi wa daktari kutokana na kupata maumivu katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa nchini Uganda.

Morali za wachezaji ilionekana ipo juu na walifanya jitihada kubwa mazoezini ili kulishawishi benchi la ufundi kuwapa nafasi katika mchezo wa leo.

Awali, wapinzani hao wa Simba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Vipers walitua salama nchini kuelekea mechi yao hiyo ya Kundi C.

Katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Kampala nchini Uganda, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na beki wa kati, Henock Inonga.

"Kama wachezaji, tunajua umuhimu wa mchezo wa kesho ambao hatuhitaji ushindi wowote," alisema beki wa pembeni wa Simba, Shomari Kapombe katika mkutano wa maandalizi ya mechi.

Ushindi wa Simba utawafanya kufikisha alama sita, jambo ambalo linawapa matumaini ya kufuzu hatua ya nane bora.

Katika msimamo wa Kundi C, baada ya mechi tatu walizocheza, Raja Casablanca wanaongoza kwa alama tisa wakifuatiwa na Horoya wenye alama nne huku Simba wakishika nafasi ya tatu wakiwa na alama tatu na Vipers wakiwa mkiani baada ya kuambulia alama moja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news