WAKENYA ACHENI:Hiyo sumu haionjwi, mwisho wake ni mbaya

NA LWAGA MWAMBANDE

LEO Machi 27, 2023 kundi lililojihami kwa silaha limedaiwa kuvamia sehemu ya mali inayomilikiwa na familia ya Rais wa zamani wa Kenya, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta huko Nairobi kwenye barabara ya Eastern Bypass.
Picha na Standard Media.

Waandamanaji hao waliokuwa wakiimba nyimbo zenye hamasa za Mau Mau walisikika wakisema wao pia ni Wakenya na wanastahili kumiliki ardhi sawa na familia ya Kenyatta.

Waandishi wa habari wa Nation walipofika eneo la tukio, walikuta watu wengi walikuwa tayari wameshazifikia mali hizo. Wengi wao walikuwa wamejihami kwa silaha hatarishi yakiwemo mapanga na marungu. Huku wakionekana wakibeba mifugo shambani humo wakiwemo kondoo.

Mwanahabari wa Nation anayeripoti masuala ya uhalifu, Steve Otieno alikuwa miongoni mwa watu ambao walikuwa wanatimiza majukumu yao, lakini mwishowe alishambuliwa na kundi hilo baada ya kugundua kuwa alikuwa mwanahabari aliyeripoti kisa cha uvamizi huo. Baada ya kumvamia walimpora pia simu yake.

Aidha,baadaye,wafanyakazi wa NTV waliofika eneo hilo walikumbwa na hali sawa na gari lao lilipigwa mawe na waporaji hao wenye.

Vivyo hivyo, watu wasiojulikana walivamia Kampuni ya East Africa Specter Limited ambayo inahusishwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, mkuu wa usalama wa kampuni hiyo, Humphrey Waswa ameeleza katika taarifa yake leo.

Shambulio dhidi ya kampuni ya kutengeneza mitungi ya gesi inayomilikiwa na familia ya Odinga liliendana na uvamizi wa ardhi ya Kenyatta huko Barabara ya Eastern Bypass.

East Africa Spectra, iliyokopo Barabara C katika Eneo la Viwanda la Nairobi, inatengeneza na kusambaza mitungi ya gesi nchini Kenya.

“Majira ya saa 11.40 alfajiri ya kuamkia leo, kundi la watu wapatao 50 waliokuwa kwenye pikipiki walifika na kutuvamia na walikuwa wakisaidiwa na magari manne yasiyokuwa na namba.Lengo lao lilikuwa kwa mkurugenzi wetu mkuu kwa sababu ofisi yake ndiyo imeharibiwa,”amesema Bw.Waswa.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anafafanua kuwa,yanayoendelea huko Kenya si ya kuvumilika, kwani mwisho wake ni mbaya kuliko mwanzo. Ni heri uvumilivu, kuheshimiana na kuvutiana subira ili kudumisha amani, umoja na mshikamano kuliko machafuko yasiyokuwa na tija. Endelea;


1.Kenya kinachotokea, huku macho tunafinya,
Kule wanaelekea, yale wanayoyafanya,
Ni kama wanapotea, tunapaswa kuwaonya,
Hiyo sumu haionjwi, mwisho wake ni mbaya.

2.Walianza mandamano, ruksa katiba Kenya,
Wakayasema maneno, mema hata ya kusonya,
Haikuwa mikutano, bila hasara kufanya,
Hiyo sumu haionjwi, mwisho wake ni mbaya.

3.Mafanikio ya mwanzo, kama yamewatekenya,
Ni kama vile mwongozo, kuzidisha kuyafanya,
Katiba yabaki nguzo, ruksa hayo kufanya,
Hiyo sumu haionjwi, mwisho wake ni mbaya.

4.Watu wanakufakufa, damu hiyo watapanya,
Kazi wala siyo dhifa, watu washindwa kufanya,
Kama unakua ufa, miongoni mwa Wakenya,
Hiyo sumu haionjwi, mwisho wake ni mbaya.

5.Wameacha andamana, ona kile wanafanya,
Mali zao waziona, waenda kuzitapanya,
Hata sisi twawaona, nani kitu atafanya?
Hiyo sumu haionjwi, mwisho wake ni mbaya.

6.Kashambuliwa Kenyatta, likuwa Rais Kenya,
Mali zake wamefwata, nani atayewakanya?
Utajiri wamepata, ni nyara wazigawanya,
Hiyo sumu haionjwi, mwisho wake ni mbaya.

7.Odinga hajasalia, na yeye wamemfinya,
Wafanyakazi walia, kile watu wamefanya,
Vurumai zaingia, mnakwenda wapi Kenya?
Hiyo sumu haionjwi, mwisho wake ni mbaya.

8.Mwishoni tukumbushane, nchi ya kwenu ni Kenya,
Hilo mfahamishane, msiivuruge Kenya,
Hivyo vema mpatane, hiyo kubwa sana Kenya,
Hiyo sumu haionjwi, mwisho wake ni mbaya.

9.Kwa wanasiasa Kenya, chungeni mnayofanya,
Tuliombali twaonya, si vema mnayofanya,
Maneno yenu ya kunya, yanaivuruga Kenya,
Hiyo sumu haionjwi, mwisho wake ni mbaya.

10.Hili la kulitambua, kubwa sana nchi Kenya,
Nyote tunawatambua, hamjafikia Kenya,
Hilo mkilitambua, mtafanya kitu Kenya,
Hiyo sumu haionjwi, mwisho wake ni mbaya.

11.Leo wako wa Kenyatta, si Rais tena Kenya,
Odinga wamempata, mali yake kutapanya,
Na kwingine watapita, ndivyo kuvuruga Kenya,
Hiyo sumu haionjwi, mwisho wake ni mbaya.

12.Katiba hiyo ya kwenu, isiwamalize Kenya,
Maandamano ni yenu, yasiwavuruge Kenya,
Na viongozi ni wenu, wasigombanishe Kenya,
Hiyo sumu haionjwi, mwisho wake ni mbaya.

13.Amani twapendelea, ikizidi dumu Kenya,
Tusije tukapokea, wakimbizi toka Kenya,
Au tena kutokea, vuruguvurugu Kenya,
Hiyo sumu haionjwi, mwisho wake ni mbaya.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news