NA LWAGA MWAMBANDE
MACHI 8, mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi na walezi nchini kuangalia sehemu waliyokosea kwenye suala la malezi ya watoto na kulifanyia kazi suala hilo ikiwemo kuzingatia mila na desturi ili kuepuka mmomonyoko wa maadili nchini.
“Kuna mengine ya kuletewa tukatae yale ya kuletewa, sisi kama taifa tukatae yale ya kuletewa, kwa sababu yakija hayamuumizi mmoja, leo yamemuumiza jirani kesho yataingia kwako,”ameagiza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.
Pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameshauri wazazi kuhakikisha watoto wao wanawapa mafunzo ya dini ili kuepukana na mmomonyoko huo wa maadili katika jamii na Taifa.
Wakati huo huo ameshauri viongozi wa dini, serikali kuungana kwa pamoja na kuona nini cha kufanya katika kulinda maadili ikiwemo kuzilinda mila na desturi.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyasema hayo wakati akishiriki Kongamano la Siku ya Wanawake Duniani lilioandaliwa na Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) katika Ukumbi wa Kuringe mkoani Kilimanjaro.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, ingawa usawa ni haki ya wanawake wote pia suala la malezi linapaswa kuwa kipaumbele katika familia baina ya mama na baba ili kuendelea kuwa na familia bora ambayo itakuwa tegemeo katika siku za mbeleni kwa ustawi bora wa Taifa na jamii. Endelea;

1.Hongera kwa siku yenu,
Sisi ni watoto wenu,
Tena ni waume zenu,
Na pia rafiki zenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
2.Na wanaume ni wenu,
Kazini hao wenzenu,
Na pia ni kaka zenu,
Wengine waume zenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
3.Twapenda uwepo wenu,
Na hayo mapenzi yenu,
Yetu sikukuu yenu,
Maishani kwetu tunu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
4.Ulipo uwepo wenu,
Faida jamii yenu,
Malezi yetu ni yenu,
Uzazi wetu ni wenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
5.Mkifanya kazi zenu,
Faida kwetu na kwenu,
Na mahangaiko yenu,
Raha kwetu na kwenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
6.Wanawake siku yenu,
Hiyo ni furaha kwenu,
Katika maisha yenu,
Na kutambulika kwenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
7.Na sisi ni ndugu zenu,
Na tena ni watu wenu,
Wengine rafiki zenu,
Tena ni watoto wenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
8.Tuzione tambo zenu,
Mkifanya mambo yenu,
Tufurahi siku yenu,
Na hata maisha yenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
9.Ni furaha siku yenu,
Hata kwa sisi wenzenu,
Kwa kufanikiwa kwenu,
Faida yetu na yenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
10.Twajua ubora wenu,
Kwa hizo nafasi zenu,
Mliko kote ni kwenu,
Mnafanya mambo yenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
11.Huo uongozi wenu,
Katika nafasi zenu,
Kweli si faida yenu,
Bali ya jamii yenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
12.Kwa maendeleo yenu,
Heri kwa jamii yenu,
Na mafanikio yenu,
Furaha kwa watu wenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
13.Twapata vionjo vyenu,
Mfanyapo mambo yenu,
Huo umakini wenu,
Twapita mikono yenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
14.Udijitali ni wenu,
Zidi fanya mambo yenu,
Usawa uwe ni wenu,
Kazi zote ziwe zenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
15.Mnao wajibu wenu,
Tofauti na wenzenu,
Mambo ya uzazi wenu,
Ni ya kwenu peke yenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
16.Mpini huu ni wenu,
Kujaza dunia yenu,
Hebu fanya zamu yenu,
Afurahi Mungu wenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
17.Shikeni jukumu lenu,
Msiige ya wenzenu,
Kuoana jinsi zenu,
Kinyume na Mungu wenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
18.Maisha yetu ni yenu,
Yako mikononi mwenu,
Watoto wetu ni wenu,
Wataka mapenzi yenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
19.Pendaneni kati yenu,
Kwa maendeleo yenu,
Pia ustawi wenu,
Katika mahali penu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
20.Hii chuki kati yenu,
Ni kuangushana kwenu,
Pia udumavu wenu,
Huko kusikae kwenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
21.Kwa kuimarika kwenu,
Mkishika zamu yenu,
Kwa pamoja na wenzenu,
Tapata makubwa kwenu,
Usawa ni haki yenu,
Wanawake duniani.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602