NA DIRAMAKINI
IKIWA imesalia miaka miwili kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA-Zanazibar), Dkt. Mzuri Issa amewataka wanawake wenye ndoto za kugombea na kushika nafasi mbali mbali za uongozi kuanza harakati za kujijenga mapema ili waweze kuibuka kidedea na kuwa washindi.
Hii itasaidia kuwa na uwakilishi wa kutoka katika vyombo vya kutunga sheria na kutoa maamuzi pamoja na kushika nafasi za juu kwenye vyama vya siasa.
Dkt,Mzuri aliyasema hayo wakati alipokua akizungumza na wanawake wapatao 45 ambao ni wawakilishi kutoka vyama mbalimbali vya siasa visiwani Zanzibar walioanza mafunzo ya siku tatu ambayo yanalenga kuwajengea uwezo wa kugombea na kushika nafasi mbali mbali za uongozi zikiwemo za ndani ya vyama vya siasa na hata zile za viongozi wa kuchaguliwa majimboni.
Alisema, kwa muda mrefu wanawake wengi wamekua wakishindwa kutimiza malengo yao licha ya kuwa na nia ya kuwa viongozi na tafiti mbali mbali zimeonyesha kuwa miongoni mwa sababu zinazopelekea ni kutojiandaa mapema.
‘’Lazima tutambue kuwa tunakabiliana na changamoto nyingi sana ikiwemo wenzetu wanaume wana hila za kutuhujumu hivyo na sisi wanawake tunapaswa kujiandaa mapema sana na niwaambie tu hakuna kurudi nyuma muda ni sasa,’’aliongezea.
Pia Mkurugenzi huyo wa TAMWA-ZNZ amewataka washiriki hao wa mafunzo pamoja na wanawake wengine kutokata tamaa licha ya changamoto mbali mbali watakazozipitia zikiwemo za kukatishwa tamaa kwa makusudi na watu wenye dhamira mbaya dhidi yao.
Katika hatua nyengine alizungumzia kuhusu suala la rushwa kwenye uwanja wa siasa, ameitaka Serikali kupitia mamlaka husika kuhakikisha wanafuatilia kwa umakini zaidi ili waweze kuwabaini na kuwachukulia hatua stahiki wale wote wanaojihusha na vitendo hivyo na kusisistiza kuwa rushwa ni dhambi na haipaswi kuachiwa ikaendelea kukandamiza haki.
‘’Tunazitaka mamlaka husika kuhakikisha katika michakato yote ya uchaguzi ujao mwaka 2025 wanafuatilia kila hatua kubaini wale wote wenye kujihusisha na rushwa ambapo kwa namna moja au nyengine ni kikwazo cha wanawake kutofikia malengo’’aliongezea.
Akitolea mfano alisema kuwepo madarakani kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kielelezo tosha kinachoonyesha uwezo wa kiongozi mwanamke ambacho wanawake wa Zanzibar wanapaswa kukitumia kama sehemu ya kusonga mbele.
“Rais Samia amekuwa ni kigezo kwetu sote wanawake, na kuwepo kwake madarakani amezidi kutupa moyo na ari mpya kwa wanawake kuingia katika mchakato wa kugombea nafasi mbali mbali za uongozi,”amesema Dkt. Mzuri.
Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo hayo Dkt,Salum Suleiman Ali Kutoka Chuo kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) alisema wanawake wa Zanzibar wanaweza kutimiza malengo yao iwapo watajipanga vizuri.
Pamoja na kujipanga, pia kujitambua na kujiwekea malengo tangu awali na kuwa na utaratibu wa kujipika katika kila hatua kwenye mchakato wake.
Pia alisema wanawake wanapaswa kuacha hofu na kujitoa katika midahalo mbalimbali ambayo alisema inamjenga mwanamke katika kutambua upangiliaji wa hoja ambazo zitamuwezesha kukubalika kwa haraka zaidi kwenye jamii.
‘’Nyinyi wanawake mliopo kwenye mafunzo haya na wengine huko nje ni lazima mutambue kuwa siasa ni mfumo hubadilika kila wakati hivyo munapaswa sana kusoma na kufahamu yanayoendelea kila leo,’’aliongezea.
Sambamba na hayo aliwataka washiriki hao kutambua hadhira na aina ya watu wanaozungumza nao kuepuka kuzungumza mambo yasikua na umuhimu kwenye jamii ambayo alisema yanaweza kushusha hadhi zao na kuonekana ni mtu au watu wasiokua na uwezo wa kuwa viongozi.
Kwa upande wake mkufunzi mwengine Ali Sultan amesema wanawake wanaweza kushinda na kuongeza idadi kubwa zaidi kwenye nafasi za uongozi, iwapo watajijengea utaratibu wa kufanya utafiti katika maeneo wanayotaka kugombea ili waweze kutambua changamoto na kuja na suluhisho ambapo alisema ni kitu muhimu kinachopaswa kufanya.
Kwa upande wao washiriki walisema mafunzo hayo ya siku tatu yamekuja katika kipindi muhimu ambacho wanahitaji kujengewa uwezo zaidi kwa kuwa wana mengi wanayopaswa kujifunza.
Walisema wengi wao wamewahi kugombea nafasi tofauti lakini ni wachache walioweza kufikia melengo na wanaamin walishindwa kwa sababu ambazo wangepatiwa elimu ya awali wangeweza kuibuka kuwa washindi.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanafanyika katika ukumbi wa TAMWA-ZNZ Tunguu wilaya ya kati Unguja kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway Nchini Tanzania kupitia mradi wa kuwawezesha wanawake kuwa viongozi ‘’Strengthening Women in Leadership’’ (SWIL) yanatoa fursa pia kwa washiriki hao kukutana na wawakilishi wa taasisi mbali mbali pamoja na wanasiasa waliofanikiwa kutoa ushuhuda huku lengo likiwa ni kuwajengea uwezo zaidi washiriki.