NA DIRAMAKINI
WANANCHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara wameshauriwa kuandika urithi kwa ajili ya familia zao wangali hai ili kupunguza migogoro ya kugombania mali zilizoachwa na wazazi pindi wanapoaga dunia.
Ushauri huo umetolewa na Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Vicent John Gienda wakati akitoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia uliozoeleka katika maeneo ya Uvuvi katika kata za Bukima na Kiriba.
Elimu hiyo imetolewa kupitia mikutano ya wananchi waliojitokeza katika Tamasha lilioandaliwa na Shirika la Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) kupitia Mradi wa 'Funguka Paza Sauti kupinga vitendo vya ukatili wa Kijinsia uliozoeleka katika maeneo ya Uvuvi' ambao unafdhiliwa na shirika la Foundation for Civil society.
Ezra Majogoro ni mkazi wa Kijiji cha Bukima ambaye aliuliza swali katika mkutano huo kuwa endapo anaruhusiwa kuandika wosia unaowatambua warithi wake na kuengua baadhi ya watoto wenye umri zaidi ya miaka 18 ambao hawakutoa mchango kwa mzazi wakati wa uhai wake wakiwemo wenye tabia ya kumwibia mzazi na kutapanya mali.
"Naomba unisaidie kama naweza kuandika wosia wangu nikionesha mgao wa mali zangu na kuwaacha baadhi ya watoto ambao umri wao ni zaidi ya miaka 20, ni watu wazima lakini hawana mchango wowote kwangu ili niweke wale amabo naona wanastahili kurithi mali yangu pindi nikiaga dunia," aliuliza Bibi Ezra Majogoro wa Bukima.
Naye Charles Mwiyabi Mutu amesema, ukatili wa kijinsia katika maeneo ya uvuvi umeshamiri hasa utelekezaji wa familia siyo kwa wanawake pekee, bali hata wanaume wamekuwa wakitelekezewa watoto na wake zao na kuondoka kwenda visiwani ambapo huolewa na wanaume wengine huko.
Pia, Mwuyabi amepongeza juhudi za VIFAFIO kwa kujikita naeneo ya Uvuvi ambapo unyanyasaji na vitendo vya ukatili vimeshamili huku hakuna mashirika ya kijamii yanayofanya kazi ya kuwaelimisha wananchi dhidi ya mila zinazosababishwa na ukatili.
Edward Misana ni kijana anayeishi katika Kijiji cha Bukima Kata ya Bukima amesema, vijana wengi katika maeneo ya uvuvi hawafungi ndoa isipokuwa kuishi katika uchumba sugu na kuacha huku watoto wakizaliwa kuishia kutelekezwa baada ya wazazi hao kutengana na kila mmoja kuondoka na kuelekea sehemu nyingine.
Robinson Wangaso ni Mratibu wa Miradi huo ambaye amesema, maeneo ya uvuvi ukatili wa kijinsia uliozoeleka na malezi duni kwa watoto ni changamoto kubwa inayohitaji kutatuliwa kwa wadau mbalimbali kuunganisha nguvu kwa pamoja.
"Watoto wengi sana wanakosa malezi na matunzo sahihi kutoka kwa wazazi hivyo kujiingiza katika ajira za utotoni kwa kufanya kazi katika mialo ya samaki, mimba katika umri mdogo na ndoa kabla ya wakati ni baadhi ya changamoto zilizopo maeneo ya jamii ya Wavuvi,"amesema Robinson Wangaso.
Wangaso amesema, pamoja na mradi huo kufanya matamasha katika maeneo na kata mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Musoma wameanza kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia kupitia shule za sekondari na msingi ili kuwaanda watoto na vijana kujiepusha na athari katika maisha yao ya baadae ili watimize ndoto zao.
Wangaso amesema, mpaka sasa elimu hiyo imetolewa katika shule za Sekondari Kiriba iliyopo halmasha ya Wilaya ya Musoma huku shirika la VIFAFIO likiwa na mkakati wa kufikia shule nyingine za Msingi na Sekondari ndani ya Halmashauri ya wilaya ya Musoma na Bunda mkoani Mara.
Kwa upande wao wanafunzi na wazazi kutoka kata ya Kiriba wamepongeza VIFAFIO kwa kutoa elimu hiyo na kuomba iendelee kutolewa mara kwa mara ili iwafikie wakazi wote wa Kata huyo.
"Tunawakaribisha mrudi tena kutuletea elimu hii ambayo itatusaidia sana kubadilishaa tabia za wananchi na watoto wetu wa kata ya KIRIBA". amesema Magoma Magegu mwakilishi wa wazazi na mjumbe wa Bodi Shule ya Sekondari ya Kiriba.