Washirikishe wengine, usikumbatie vyote

NA LWAGA MWAMBANDE

HIVI karibuni Askofu Lawi Mwankuga wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Mashariki amesisitiza umuhimu wa kushirikishana vipawa vya watu wengine, kwani hakuna aliye mkamilifu zaidi ya Mungu pekee.
Ametoa wito huo mahususi wakati akihubiri kwenye ibada ya Mbaraka wa wachungaji jijini Dar es Salaam huku akisisitiza kuwa, tunaishi kwa kutegemeana.

"Wapakwa mafuta wa Bwana, pateni kushirikisha vipawa vya watu wengine, Yesu alishirikisha vipawa vya watu wengine ili akaombe pamoja nao.

"Hayupo aliye mkamilifu, aliye mkamilifu ni Mungu peke yake, tunaishi tunategemeana na kama yuko mtu ambaye anasema sihitaji msaada wa mtu mwingine, hiyo ni roho ya kiburi.

"Haijatoka kwa Bwana, Yesu mwenyewe aliwahitaji wengine, hata kama walimtelekeza, lakini inaonesha alitambua mchango wa watu wengine, namna gani umetambua mchangao wa wengine, ni namna gani umetambua mchango wake kwake, lakini yeye hajatambua, hiyo ni habari nyingine,"amefafanua Askofu Lawi.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, kuna nguvu ya mafanikio kupitia ushirikishanaji wa vipawa miongoni mwetu katika kuyaendea maono na malengo tuliyojiwekea, hivyo yafaa tukumbuke kuwa, tunategemeana kwa kila jambo, pasipo kushirikishana ni ishara ya kiburi. Endelea;

1:Washirikishe wengine, usikumbatie vyote,
Nena na wao wanene, upate nao wapate,
Fanya na watu waone, kwamba mnakwenda wote,
Sote twategemeana, ubinafsi kiburi.

2:Wewe tambua wengine, ukipatacho wapate,
Mpe nafasi mwingine, uzoefu aupate,
Awe mwembamba mnene, umiliki aupate,
Sote twategemeana, ubinafsi kiburi.

3:Tujifunze kwa wengine, na maarifa tupate,
Tufanye tusijivune, maisha ni yetu sote,
Tukienda tupatane, tutafaidika sote,
Sote twategemeana, ubinafsi kiburi.

4:Tufundishe tukuone, elimu yako tupate,
Tupe nafasi uone, tulichonacho upate,
Ombwe hapo tusione, tusipokuwapo wote,
Sote twategemeana, ubinafsi kiburi.

5:Utende usijione, na hata kufanya pate,
Nyote mshirikiane, Injili ifike pote,
Tukuone tuwaone, mkitenda kazi nyote,
Sote twategemeana, ubinafsi kiburi.

6:Bwana Yesu tumuone, kwenye kazi yake yote,
Wanafunzi tuwaone, aliwatumia wote,
Ili naye wafanane, Injii ifike kote,
Sote twategemeana, ubinafsi kiburi.

7:Kwenda kuomba tuone, wanafunzi awachote,
Lengo wao wapatane, wamuombe Mungu wote,
Lengo wategemeane, wakiombacho wapate,
Sote twategemeana, ubinafsi kiburi.

8:Na kuhani tukuone, unatuongoza sote,
Na wala usijione, kwamba unajua yote,
Nafasi wape wengine, tupate vipawa vyote,
Sote twategemeana, ubinafsi kiburi.

9:Familia tuwaone, mwashirikiana nyote,
Mume mke tuwaone, mnafanya yenu nyote,
Na wala msitengane, ili Baraka mvute,
Sote twategemeana, ubinafsi kiburi.

10:Maishani tujione, dunia ni yetu sote,
Na wenzetu tuwaone, wanacho kitu tupate,
Na wala tusitengane, kwamba tunajua vyote,
Sote twategemeana, ubinafsi kiburi.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news