Waziri Dkt.Mabula asitisha utoaji vibali vya ukarabati majengo chakavu Mwanza

NA MUNIR SHEMWETA-WANMM

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula amesitisha utoaji vibali vya ukarabati kwa majengo chakavu ya chini mkoani Mwanza ili kutoa fursa ya uendelezaji upya viwanja hivyo kwa mujibu wa mpango kabambe. 
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula akioneshwa moja ya jengo ambalo ujenzi wake unaendelea bila kuzingatia mpango kabambe wa Jiji la Mwanza katika eneo la Nyamagana alipofanya ziara kwenye jiji hilo Machi 9, 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).

Aidha, amewaelekeza wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo kuhakikisha ifikapo Juni, 2023 wanawasilisha taarifa za utekelezaji wa sheria ya mipango miji ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mpango kabambe na mipango kina kama ilivyoelekezwa na Sheria ya Mipango miji sura 355 kifungu cha 22(1).
Dkt.Mabula ametoa uamuzi huo leo Machi 9,2023 katika kikao cha utekelezaji wa programu ya urasmishaji makazi na shughuli nyingine za sekta ya ardhi kilichofanyika jijini Mwanza. 

Mipango kabambe inatoa mwongozo wa ukuaji miji na kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali na kudhibiti uendelezaji holela. 
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula akitoka katika moja ya nyumba chakavu inayofanyiwa ukarabati bila kuzingatia mpango kabambe wa jiji la Mwanza eneo la Nyamagana alipofanya ziara kwenye jiji hilo leo.  

Amesema, Jiji la Mwanza ni miongoni mwa majiji yanayokuwa kwa kasi hapa nchini na lenye sifa ya kuwa kitovu cha kiuchumi na kibiashara katika ukanda wa nchi za maziwa makuu na Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Dkt.Mabula, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa uliogharimu kiasi cha dola za Marekani 5,507, 145 sawa na shilingi 9,204,645,495.8 kwa kiwango cha dola kwa shilingi 1671.4 cha wakati huo kwa ajili ya kuandaa mpango kabambe (2015-2035) wa jiji la Mwanza. 
Amesema, pamoja na gharama kubwa iliyotumika kumekuwa na kupuuzwa na kutozingatiwa kwa mpango huo ambao ni nyaraka ya kisheria iliyotangazwa katika Gazeti la Serikali Na 472 la tarehe 19 Juni 2020. 

‘’Sheria ya Mipangomiji sura 355 kupitia fungu la 7 (u) inaipa mamlaka ya jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela kusimamia na kutathmini utekekezaji wa mpango kabambe na mipangokina,"amesema Dkt.Mabula. 
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima akizungumza katika kikao kazi cha utekelezaji wa programu ya urasimishaji makazi na shughuli nyingine za sekta ya ardhi kilichofanyika jijini Mwanza. Kulia ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula.

Fungu la 40 la sheria ya mipangomiji inazipa mamlaka za upangaji nguvu ya kisheria kudhibiti na kusimamia uendelezaji wa mji katika eneo lake la utawala.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amekagua ujenzi wa majengo katika jiji la Mwanza kubaini majengo yanayojengwa bila kuzingatia mpango kabambe wa jiji hilo. 
Katika ukaguzi huo, Dkt. Mabula alibaini baadhi ya majengo ujenzi wake ukifanyika bila kuzingatia mpango kabambe ambapo yamejengwa maduka huku eneo moja likijengwa kiwanja cha michezo katikati ya jiji. 

Ameitaka halmashauri ya jiji la Mwanza kuhakikisha ujenzi au ukarabati unaofanyika kwenye maeneo ya jiji hilo unazingatia mpango kabambe wa jiji hilo. 
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula akizungumza na mkazi wa Nyamagana, Bi. Rukia Yusuf alipofanya ziara kwenye jiji la Mwanza kukagua ujenzi wa nyumba usiozingatia mpango kabambe wa jiji hilo leo

Aidha, ameitaka halmashauri ya jiji la Mwanza kutoa elimu kuhusiana na mpango kabambe wa jiji la Mwanza kwa wananchi wa maeneo hayo ili kuwapa uelewa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news