NA MUNIR SHEMWETA-WANMM
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Amgeline Mabula amewataka wananchi kuchangamkia zoezi la urasimishaji linaloendelea nchini ili kuondokana makazi holela.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akikabidhi hatimiliki za ardhi kwa mume na mke wakati wa zoezi la kukabidhi Hatimiliki za Ardhi kwa wananchi waliorasimishiwa makazi yao kwenye kata za Muriet na Olasiti mkoani Arusha leo Machi 1, 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).
Dkt.Mabula ametoa kauli hiyo leo Machi 1,2023 mkoani Arusha wakati wa zoezi la kukabidhi Hatimiliki za Ardhi kwa wananchi waliorasimishiwa makazi yao katika kata za Muriet na Olasiti mkoani humo.

"Serikali inaendelea na programu ya kupanga na kupima ardhi ikiwa na lengo la kuondoa makazi holela, programu hii inafanyika katika meneo mbalimbali ilianza mwaka 2013 na inategemea kuisha mwaka huu,"amesema Dkt.Mabula.
Kwa mujibu wa Dkt.Mabula, Mkoa wa Arusha una jumla ya mitaa 112 inayofanyiwa urasimishaji ambapo michoro ya mipango miji 391 imeandaliwa na kuidhinishwa yenye viwanja 104,097 na tayari viwanja 55,023 vimewekewa beacon huku upimaji wa viwanja 46,197 ukiwa umeidhinishwa.
Hata hivyo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesikitishwa na mwitikio mdogo wa wananchi waliojitoleza kuchangamkia zoezi hilo la urasimishaji makazi holela nchini.

Aliwasihi wananchi waliorasimishiwa makazi yao kuhakikisha wanalipa kwa wakati gharama za kurasimishiwa maeneo yao ili zoezi la urasimishaji katika mitaa yao liishe kwa wakati.

Aliwakumbusha wananchi kuhusu msamaha wa riba ya kodi ya ardhi uliotolewa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutaka wadaiwa wakubwa kutumia fursa hiyo kabla haijaisha Aprili 30, 2023 kwa kuwa kumekuwa na kawaida kwa wananchi kulalamika kwamba wanaomba kuongezewa muda ikifika mwisho wa siku za msamaha.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Gasper amesema, pamoja na Serikali kuamua kuwarasimishia makazi wananchi, lakini tatizo linaonekana lipo kwa wananchi kutokana na kwa kushindwa kulipia gaharama za kurasimishiwa na wengine kushindwa kuchukua hati ambapo aliwaomba wananchi wa Mkoa wa Arusha kuchangamkia fursa ya zoezi la urasimishaji kabla halijafungwa.
"Sitegemei kuona wananchi wanakuja ofisini kuomba kuongezewa muda na kuwataka kuutumia muda wa sasa vizuri kwa kurasimishiwa makazi yao kutaka uhamasishaji zaidi kwa wananchi katika zoezi hilo,"amesema Gasper.
