NA MUNIR SHEMWETA-WANMM
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt. Angeline Mabula amezitaka halmashauri nchini kuviandaa vijiji kuwa miji endelevu ya baadaye na yenye tija kiuchumi na kijamii kwa vizazi vinavyo sambamba na kuhimiza upangaji wa vijiji na ujenzi wa nyumba kwa kuzingatia mwongozo wa upangaji na ujenzi wa nyumba bora vijijini.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akiwasili kwa ajili ya kuendesha kikao kazi cha kujadili na kuweka mikakati ya kukwamua changamoto za urasimishaji makazi katika Mkoa wa Geita leo Machi 7, 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).
Dkt.Mabula amesema hayo leo Machi 7, 2023 wakati wa kikao kazi cha kujadili na kuweka mikakati ya kukwamua changamoto za urasimishaji makazi na sekta ya ardhi kwa ujumla katika Mkoa wa Geita.
Amesema, moja ya changamoto kubwa inayoikabili nchi kwa sasa ni kasi kubwa ya ukuaji vitovu vya vijiji inayoambatana na vijiji hivyo kuendelea kupoteza hadhi yake ya kuwa vijiji kwa kusongwa au kumezwa na tabia za kijamii kwa ukuaji usio endelevu.


Mbunge wa Jimbo la Geita, Constantine Kanyasu akizungumza wakati wa kikao kazi cha kujadili na kuweka mikakati ya kukwamua changamoto za urasimishaji makazi katika Mkoa wa Geita leo Machi 7,2023.
‘’Tanzania kwa sasa ina vijiji 12,318 kati ya vijiji hivyo zaidi ya vijiji 10,000 sawa na asilimian 80 ya vijiji vyote vimepimwa mipaka yake na kupewa vyeti vya ardhi vya vijiji ambapo kati ya vijiji hivyo vijiji vyenye mpango ya jumla ya matumizi ya ardhi ni 2, 675 sawa na asilimia 21.7 ya vijiji vyote,"amesema Dkt.Mabula.


Waziri wa Ardhi, Dkt.Angeline Mabula (kulia), Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela (katikati), Mkuu wa Wilaya ya Geita, Boniface Magembe wakiwa katika kikao kazi cha kujadili na kuweka mikakati ya kukwamua changamoto za urasimishaji makazi katika Mkoa wa Geita.
Amebainisha kuwa, jambo hilo linatokana na mamlaka za upangaji kukosa kipaumbele katika kuzijengea uwezo serikali za vijiji ili kutimiza jukumu hilo la kuandaa mipango kina ya makazi ili kusimamia ukuaji wake kama miji ya baadaye.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeandaa Mwongozo wa Upangaji Makazi na Ujenzi wa Nyumba Vijijini mwongozo wenye lengo la kuwasaidia wakijiji kupanga makazi ya vijiji vyao na kujenga nyumba bora na za gharama nafuu kwa njia shirikishi kati ya wataalam wa Mipangomiji, wanavijiji na wadau mbalimbali.