Waziri Dkt.Mabula:Kijiji cha Msomera kuwa cha mfano kwa vijiji vingine nchini

NA MUNIR SHEMWETA-WANMM 

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula amesema Kijiji cha Msomera kilichopo wilayani Handeni mkoa wa Tanga kitakuwa kijiji cha mfano kwa vijiji vingine nchini kwenda kujifunza kutokana na kuwekewa mpango wa matumizi bora ya ardhi na kusimamiwa vizuri. 
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akipokewa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando alipowasili wilayani humo kwa ziara ya siku moja Machi 22,2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).

Dkt.Mabula amesema hayo Machi 22,2023 wakati wa zoezi la kukabidhi hati miliki za ardhi kwa wananchi waliohamia kijiji hicho kutoka Ngorongoro mkoani Arusha pamoja na wenyeji ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa. 
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akimkabidhi mmoja wa wananchi wa kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga hati milki ya ardhi tarehe 22 Machi 2023. 

"Kijiji hiki sisi kama Serikali chini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan tunakwenda kukifanya kama kijiji cha mfano maana yake watu watatoka maeneo mengine kuja kujifunza hapa kutokana na namna kilivyopangwa na mnavyoisimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi," amesema Dkt.Mabula.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendekeo ya Makazi, wananchi waliopelekwa katika kijiji hicho cha Msomera kutoka Ngorongoro hawakupelekwa kwa bahati mbaya bali ni dhamira na nia njema ya serikali kumuwezesha mtanzania mmoja mmoja. 
"Wote tunajua kabisa nia ya serikali ni njema, kitendo cha kuletwa na kuwa na uhakika wa ardhi kwa ajili ya kujenga na kupewa ardhi kwa ajili ya kilimo kwa ekari tano kwa kila kaya ni jambo la kumshukuru Mungu na Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan,"amesema Waziri Dkt.Mabula. 

Aidha, Dkt.Mabula amewataka wananchi wa kijiji hicho kuepuka migogoro kwa kuwa Msomera ni eneo ambalo serikali inalitupia macho na kujifunza ambapo alisisitiza kuwa wizara yake haitaki kuona panakuwa na vijiji vinavyokuwa bila mpangilio. 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Profesa Wakuru Magigi alisema, awamu ya kwanza ya utekekezaji mradi kwenye kijiji cha Msomera, serikali imejenga takriban nyumba 503 na viwanja vilivyopatikana eneo hilo yaani kupangwa na kupimwa ni 4,620 huku viwanja 14,570 vikiwa vimebuniwa. 
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (katikati waliokaa) pamoja na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga waliokabidhiwa hati milki za ardhi tarehe 22 Machi 2023.

Kwa mujibu wa Profesa Magigi, katika viwanja hivyo kuna maeneo ya huduma mbalimbali ambapo alifafanua kuwa, viwanja vya makazi kila kimoja kina ukubwa wa ekari 2.5 lakini wakati huo huo kukiwa na maeneo ya mashamba yenye ukubwa wa ekari 5 ambapo maeneo hayo yanagawiwa kwa wananchi wanaohamia na wenyeji wa Msomera. 
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando alisema alipoingia wilayani humo alikuta migogoro kadhaa katika eneo hilo la Kijiji cha Msomera hususan ile ya wenyeji na wageni ambapo ofisi yake ilichukua hatua ikiwemo kupitia nyaraka mbalimbali na kutatua changamoto hizo ambapo sasa wananchi wote wanaishi vizuri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news