Waziri Dkt.Tax:Ujio wa Makamu wa Rais wa Marekani ni matokeo ya kuimarika kwa diplomasia ya Tanzania

NA MWANDISHI WETU

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amesema kuwa ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Devi Harris inayotarajiwa kufanyika hapa nchini kuanzia tarehe 29 hadi 31 Machi 2023 ni uthibitisho wa uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Marekani na matokeo ya kuimarika kwa Diplomasia ya Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Wahariri (hawapo pichani) kuhusu ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Devi Harris nchini. Mkutano huo umefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam tarehe 27 Machi 2023. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Elsie Kanza na kushoto ni Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga.

Dkt. Tax ametoa kauli hiyo leo tarehe 27 Machi, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari kuhusu umuhimu wa ziara ya Mhe. Kamala nchini na matarajio ya Tanzania. 

Amesema ziara ya Mhe. Kamala nchini ambayo ni matokeo ya juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kukuza na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani, inalenga pamoja na mambo mengine, kuimarisha ushirikiano hususan kwenye maeneo ya kimkakati ya ushirikiano kama vile biashara, uwekezaji, utalii, elimu, afya na utunzaji wa mazingira.
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme akiwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo, Bw. Gerald Mbwafu wakifuatilia mkutao kati ya Mhe. Dkt. Tax na Wahariri.

Pia amesema kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Marekani ambao ulianza mwaka 1961 unaimarishwa na Program mbalimbali za ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hiyo ambazo kwa kiasi kikubwa zimechangia juhudi za Serikali za kuboresha maisha ya wananchi. 

Amefafanua kuwa Tanzania na Marekani zinashirikiana kupitia program mbalimbali ikiwemo Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR), Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupamana na Malaria (PMI) na Feed the Future. 
Dkt. Tax ameeleza kuwa, Marekani kupitia Program ya PEPFAR imetangaza Bajeti ya miaka miwili ya kiasi cha Dola za 827,801,250 kwa Tanzania kwa kipindi cha kuanzia Oktoba 2024 hadi Septemba 2026. 

Utekelezaji wa program hiyo hapa nchini umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza kuenea kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi pamoja na kuwezesha asilimia 88 ya watu wanaoishi na virusi kujua hali zao, na asilimia 95 kutumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo.

Kuhusu uwekezaji wa Marekani nchini, Mhe. Tax amesema nchi hiyo kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) imesajili jumla ya miradi 266 yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 4,778.6 na kutengeneza ajira zipatazo 54,584 kwa Watanzania.

Akizungumzia ratiba ya Mhe. Kamala nchini, Mhe. Dkt. Tax amesema kuwa mara atakapowasili tarehe 29 Machi, 2023, Kiongozi huyo atapokelewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango. 

Aidha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atampokea rasmi Mhe. Kamala Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 30 Machi 2023 ambapo mapokezi hayo yatafuatiwa na mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili baina ya viongozi hao. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Wahariri (hawapo pichani) kuhusu ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Devi Harris nchini. Mkutano huo umefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam tarehe 27 Machi 2023.

Vilevile, akiwa nchini, Mhe. Kamala ataweka shada la maua katika Makumbusho ya Taifa Jijini Dar es Salaam kama ishara ya kuwakumbuka wahanga wa mabamu yaliyolipuliwa kwenye Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam mwaka 1998. Pia atatembelea Taasisi ya Tanzania Startup Association ya jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukutana na Wajasiriamali Vijana pamoja nakushiriki Futari iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mwenyeji wake Mhe. Dkt. Rais Samia.Mhe. Kamala na ujumbe wake wataondoka nchini tarehe 31 Machi, 2023.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news