Waziri Mkuu:Agizo la Rais halipingwi na yeyote, watumishi wa umma zingatieni hilo

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema agizo la Mheshimiwa Rais halipingwi na mtu yeyote na akawataka watumishi wa umma kote nchini wazingatie hilo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu kwenye ukumbi wa Halmashauri, Machi 25, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Agizo la Rais likishatolewa halipingwi na mtu yeyote, kinachofuata ni utekelezaji na siyo kukaa vikao na kupitisha maamuzi mengine ya kulipinga. Hili ni suala la itifaki, na ni la muhimu sana Serikalini,” amesisitiza.

Ametoa kauli hiyo leo Machi 25, 2023 wakati akizungumza na watumishi, wakuu wa idara na wakuu wa taasisi za mkoa wa Simiyu kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo baada ya kumhoji Mkurugenzi Mtendaji wa Busega ni kwa nini hajatekeleza agiszo la Rais Samia Suluhu Hassan la kujenga soko katika eneo la Lamadi na badala yake wakaamua kulipeleka eneo la Nyashimo.


“Busega ni kwa nini hamtekelezi maagizo ya Mheshimiwa Rais ya kujenga soko eneo la Lamadi lakini mmeamua kulipelekea Nyashimo? Iweje madiwani mnakaa tena vikao na kuanza kujadili maelekezo ya Mheshimiwa Rais?” alihoji Waziri Mkuu.


Alipoulizwa maamuzi hayo ya vikao vyao yamefikia hatua gani, Mkurugenzi huyo, Bi. Veronica Sayore alijibu kwamba wameshampata Mhandisi Mshauri ambaye ni Wakala wa Majengo nchini (TBA). Waziri Mkuu alielekeza TBA wafanye hiyo kazi Lamadi na siyo Nyashimo.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema mojawapo ya ajenda za kitaifa ni kudhibiti mmomonyoko wa maadili na ukatili dhidi ya wanawake na watoto na akawataka viongozi hao wasimamie suala hilo kwa karibu zaidi.

“Twende tukasimamie suala la mmomonyoko wa maadili na ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwani hivi sasa kuna vitu vinaingia ambavyo si desturi na mila zetu. Makamu wa Rais amelieleza suala hili vizuri wakati akiwa kwenye Kanisa mojawapo.”

“Tumeanza kuona kuna vitabu vinapenyezwa hadi shuleni. Maafisa Elimu na wakaguzi nendeni mkafanye ukaguzi, vitabu ambavyo havijachapishwa au kupitishwa na taasisi yetu, ili vitumike kwenye syllabus zetu vitoeni, visiingie humo.”


“Kuna suala la mabweni, tembeleeni mkague mabweni kama ni ya wasichana pekee na wavulana peke yao ili wanaoingia huko wasije kutumia mwanya huo. Kaeni na wakuu wa shule wasimamie sana eneo hilo na kuhakikisha kuna patron na matron kwa kila bweni,” amesisitiza.

Mapema, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi, Eng. Mathew Kundo alisema kuwa wizara hiyo ilikuwa ikijenga minara ya mawasiliano 65 kwa mwaka lakini sasa hivi bajeti imeongezeka na mwaka huu wanatarajia kujenga minara 763.

Naye Naibu wa Waziri wa TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange aliwaeleza watumishi hao kwamba imetoa fedha za kutosha kujenga ofisi za Halmashauri katika wilaya za Itilima, Busega na Bariadi likiwemo jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

“Kwenye sekta ya afya, Serikali imeleta sh. bilioni 22.5 za kujenga hospitali ya wilaya za Itilima na Bariadi DC. Na hapa Bariadi TC majengo ni chakavu lakini tumeshaleta sh. milioni 900 za ukarabati ili kuhakikisha hospitaliya Somanda inafanana na hadhi ya mji wa Bariadi,” alisema.

Akitoa taarifa yake, Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Yahaya Nawanda alisema mkoa huo yeye na wakuu wa wilaya wajiwekea utaratibu wa kusikiliza keso za wananchi kila Jumanne na katika kipindi cha miezi sita, wamekwishasuluhisha migogoro 172.

Alisema kwenye sekta ya afya, walipokea sh. bilioni 25 ambazo zimejenga zahanati 59. Vituo vya afya vinne, kununua mashine nne za X-ray na kutoa ajira kwa watumishi 299 wa kada ya afya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news