NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amewataka viongozi wa Sekta ya Uchukuzi, idara na taasisi zake kubaini mapungufu ya watumishi na kuyafanyia kazi ikiwemo kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wasiotimiza wajibu wao.
Akizungumza leo Machi 20, 2023 jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekta ya Uchukuzi, Profesa Mbarawa amesema viongozi wa idara na taasisi ni wajibu wao kugundua changamoto za watumishi wa sekta na kuwachulia hatua wale wasiotimiza wajibu wao.

Aidha, ametoa rai kwa taaisisi zote zilizopo chini ya Sekta ya Uchukuzi kuhakikisha zinawashirikisha watumishi wao katika kupitia mipango na bajeti za taasisi kabla ya kuziwasilisha kwa msajili wa hazina.


“Taasisi nyingi za umma hazitekelezi wajibu huo na kuichafua Serikali, hivyo kila taasisi ifanye uhakiki na uchambuzi wa madeni ya watumishi hususanI wastaafu na kuainisha mikakati ya kulipa madeni hayo,”amesema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Sekta ya Uchukuzi, Gabriel Migire amesema sekta yake imejipanga kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa na serikali inakamilika kwa wakati.
“Nikuhakikishie tunakwenda kuwa wakali ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa na kukamilika kwa wakati hii itasaidia malengo ya serikali kufikiwa kama ilivyopangwa,”amesema.