NA DIRAMAKINI
KLABU ya Young Africans (Yanga) imekabidhiwa zawadi ya fedha taslimu shilingi milioni tano kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Kiasi hicho ni ahadi ya Rais Dkt.Samia ya kununua kila bao litakalofungwa na Simba na Yanga katika Michezo ya Shirikisho na Klabu Bingwa barani Afrika.
Jumapili iliyopita Yanga ilipata sare ya 1-1 dhidi ya Real De Bamako katika mchezo wa kundi D wa Kombe la Shirikisho uliochezwa nchini Mali, hivyo kukidhi vigezo vya ahadi ya Rais kwa zawadi ya shilini milioni tano kutokana na bao hilo.
Timu hiyo imerejea salama kutoka Mali, Jumanne mchana kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Aliyewasilisha kiasi hicho cha fedha kwa Rais wa Yanga,Mhandisi Hersi Said kwenye uwanja wa ndege ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.
Awali Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt.Pindi Chana alikabidhi zawadi ya Shilingi Milioni 15 kwa Rais wa Klabu ya Yanga, Mhandisi Hersi Said ikiwa ni ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hasan kwa klabu hiyo baada ya kuifunga Timu ya TP Mazembe ya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo magoli 3 kwa 1 kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, iliyochezwa Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam siku ya Februari 19, 2023.