Yanga SC yaongoza Kundi D Kombe la Shirikisho barani Afrika

NA DIRAMAKINI

KLABU ya Yanga (Young Africans) imefuzu hatua ya Robo Fainali katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kuibamiza US Monastir mabao 2-0.
Ni kupitia mtanange wa Kundi D ambao umepigwa Machi 19, 2023 katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Kennedy Musonda na Fiston Mayele walifunga katika kila kipindi na kuiwezesha timu yao kutinga hatua ya nane bora, ikiwa ni heshima kwa ushindi wao wa tatu mfululizo wa nyumbani.
Yanga Sc ilianza kupata bao kipindi cha kwanza dakika ya 33 kupitia kwa Kennedy Musonda akipokea krosi kutoka kwa winga wao machachari Jesus Moloko na kuzamisha wavuni.

Aidha, kipindi cha pili Yanga ilirudi ikiwa inalisakama lango la mpinzani wake na kuweza kufanikiwa kupata bao dakika ya 59 kupitia kwa mshambuliaji wao Fiston Mayele licha ya kukosa nafasi nyingi za mabao.
Mafanikio hayo yameifanya Yanga kuongoza kundi lao kwa tofauti ya mabao baada ya kuwa sawa na Monastir wenye alama 10 kila mmoja.

Aprili 2, 2023 klabu hiyo yenye maskani yake Jangwani itasafiri hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kucheza na TP Mazembe katika mgawo wao wa mwisho wa hatua ya makundi.
Katika mechi nyingine, Real Bamako wameibuka washindi wa mabao 2-1 dhidi ya TP Mazembe katika mchezo uliopigwa nchini Mali.

Bamako sasa wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wakiwa na alama tano huku Mazembe wakikita mkia wakiwa na alama tatu na wawili hao wamekosa nafasi ya kujitosa katika robo ya mwaka huu ya kombe la shirikisho.
Mbali na hayo, Yanga imeweka mfukoni shilingi milioni 10 kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye ananunua kila goli la Yanga na Simba katika pambano la kimataifa kwa shilingi milioni tano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news