ACHENI KUKWEPA KODI:Bandari bubu sikia, kiama kinawajia

NA LWAGA MWAMBANDE

APRILI 11, 2023 Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Alphayo Kidata amepokea boti mbili za mwendo kasi alizokabidhiwa na mzabuni wa kampuni ya Amikan ventures Ltd kwa ajili ya kitengo maalum cha kuzuia magendo katika Bahari ya Hindi.

Hafla ya kukabidhi boti hizo, imefanyika katika eneo la Bandari ya Dar es Salaam ambapo, Bw.Kidata amesema boti hizo zitafanya kazi ya doria ili kupambana na vitendo vya magendo ambavyo vinahatarisha mipango ya mamlaka hiyo katika kukusanya mapato ya nchi.

Pia, amesema waingizaji wa bidhaa bandia na bidhaa za magendo wamekuwa wakitumia mwanya wa urefu wa mpaka wa Pwani ya Bahari ya Hindi kwa kuingiza bidhaa hizo ikijumuisha dawa, vyakula, mavazi, viatu, vifaa vya kielektroniki,vinywaji na nyinginezo.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande licha ya kupongeza juhudi hizo kubwa za mamlaka, pia ametoa raia kwa Watanzania kuacha kukwepa kodi ili kukwepa mkono wa sheria. Endelea;

1. Mamlaka ya Mapato, hapa kwetu Tanzania,
Kuyaongeza mapato, kodi ziweze ingia,
Inavyo viwili vito, boti mbili za doria,
Acheni kukwepa kodi, mtabanwa kisheria.

2. Dasalamu na Kigoma, boti hizo zawajia,
Sababu magendo noma, jinsi yalivyozidia,
Tena hazitasimama, hadi ndani kuwatia,
Acheni kukwepa kodi, mtabanwa kisheria.

3. Boti zimeshaingia, wizi kuwachafulia,
Nyie mnaotumia, zile za mkato njia,
Bandari bubu sikia, kiama kinawajia,
Acheni kukwepa kodi, mtabanwa kisheria.

4. Wapo watu Tanzania, twafaa kuwachukia,
Kodi wanazichunia, faida kujipatia,
Baharini waingia, njia panya kutumia,
Nyie huko baharini, acheni kukwepa kodi.

5. Boti si za makasia, ni za kisasa sikia,
Mwendo kasi zakimbia, zikiwa kwenye doria,
Kote zitawafikia, nanyi huko mtalia,
Acheni kukwepa kodi, mtabanwa kisheria.

6. Hizo bidhaa bandia, hata za magendo pia,
Inayokuja doria, nawambia mtalia,
Pale zitawafikia, ni kesi ya kisheria,
Acheni kukwepa kodi, mtabanwa kisheria.

7.Hizi bidhaa bandia, kuingia Tanzania,
Kwa kweli zinachangia, uchumi kutuibia,
Tena tukizitumia, shida tunajipatia,
Acheni kukwepa kodi, mtabanwa kisheria.

8.Kidata sisitizia, kwamba mtawafikia,
Waache kutuibia, mapato kutoingia,
Na afya tuharibia, viwango kutofikia,
Acheni kukwepa kodi, mtabanwa kisheria.

9.Bidhaa mwatuibia, uchumi kutochangia,
Dawa na vyakula pia, njia panya mwatumia,
Pia mwatufanyizia, mavazi viatu pia,
Acheni kukwepa kodi, mtabanwa kisheria.

10.Pombe za magendo pia, kodi mnatuibia,
Mwaonywa bora sikia, kesho msije kulia,
Wenyewe wamepania, kuizidisha doria,
Acheni kukwepa kodi, mtabanwa kisheria.

11.Kuijenga Tanzania, lazima kodi lipia,
Hiyo ndiyo twatumia, huduma kujipatia,
Tena vema furahia, kodi unapolipia,
Acheni kukwepa kodi, mtabanwa kisheria.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news