Afrika Kusini jino kwa jino na wafanyabiashara dawa za kulevya

NA DIRAMAKINI

MAAFISA usalama kwa kushirikiana na mamlaka zingine nchini Afrika Kusini wameendelea kufanya operesheni kali za kuwasaka wafanyabiashara wa dawa za kulevya katika maeneo mbalimbali ili kuiweka jamii na Taifa salama.

Jitihada hizo zimekuja ikiwa kila mmoja anatambua kuwa,matumizi ya dawa za kulevya ni mojawapo ya sababu kuu za uhalifu wa kikatili katika jamii zetu ikiwemo wengi kupoteza mali na nguvu kazi ya uzalishaji.

Tayari, Wilaya ya Pwani ya Magharibi, Kituo cha Uendeshaji cha Mkoa na Trafiki wa Mkoa nchini humo wamefanikiwa kuondoa kiasi kikubwa cha dawa za kulevya mitaani, jambo ambalo linapongezwa na wananchi wazalendo.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Afrika Kusini (SAPS), Kapteni FC Van Wyk, Jumatano ya Aprili 26, 2023 wakati wa operesheni iliyounganishwa,mamlaka hizo ziliendesha kituo cha ukaguzi wa magari kando ya daraja la uzani la N7 Klawer.

Walisimama na kupekua gari lililotiliwa shaka hali iliyosababisha kutwaliwa kwa jumla ya tembe 41,000 za mandrax ndani ya gari hilo.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Afrika Kusini (SAPS), Kapteni FC Van Wyk amesema, dereva wa gari hilo, mwanamke mwenye umri wa miaka 33 alikamatwa. Anatarajiwa kufika katika mahakama ya Klawer mnamo Ijumaa, ya Aprili 28, 2023 kwa shtaka la kuhusika na dawa za kulevya.

Katika tukio lingine Aprili 26, 2023 makachero kutoka Kituo cha Polisi cha Table View huko Cape Town walipokea taarifa kuhusu mshukiwa ambaye alikuwa amehifadhiwa katika chumba katika hoteli ya Marine Drive, Table View akiwa na kiasi kikubwa cha dawa za kulevya.

Msemaji huyo wa SAPS amesema, kulingana na habari mtu huyo ni msafirishaji wa dawa za kulevya. SAPS walivamia chumba hicho na kukuta vifungashio 13 (zaidi ya kilo 13) vikiwa vimepigwa alama ya tik huku ndani yake ikiwa ni dawa za kulevya na ndani ya chumba hicho hakukuwa na mtu.

Aidha, vifungashio vyote kwa mujibu wa Jeshi la Polisi vilichukuliwa na kuhifadhiwa kama kielelezo huku jeshi hilo likiendelea kufanya uchunguzi wa kisa hicho na wanamsaka mshukiwa.

Uongozi wa polisi wa mkoa uliwapongeza makachero kwa kazi nzuri na uhusiano wao wa kufanya kazi na vyombo vingine vya sheria ili kuweka mazingira salama kwa watu wa mkoa huo.(SAPS)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news