Bei za mafuta zashuka tena Zanzibar, tazama bei kamili

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) imetangaza bei za mafuta kwa mwezi Aprili, 2023 huku neema kwa wamiliki wa vyombo vya moto ikiwa kubwa zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili 8, 2023 na ZURA imefafanua kuwa, mamlaka hiyo huwa inapanga bei kwa kuzingatia mambo kadhaa ikiwemo wastani wa mwenendo wa mabadiliko ya bei za mafuta duniani, gharama za uingizaji mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam na Tanga.

Mambo mengine ni thamani ya shilingi ya Tanzania na dola ya Kimarekani, gharama za usafiri, bima na premium hadi Zanzibar, kodi na tozo za Serikali ikiwemo kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na reja reja.

ZURA imebainisha kuwa, bei za mafuta kwa mwezi Aprili, 2023 lita moja ya Petroli itauzwa kwa shilingi 2,780 tofauti na bei ya mwezi Machi ambayo lita ilikuwa shilingi 2,880.

Kwa upande wa Diezel lita kwa mwezi Aprili, 2023 inauzwa kwa shilingi 2,900 tofauti na mwezi Machi ambapo lita ya Diezel ilikuwa inauzwa kwa shilingi 2,980.

Aidha, mafuta ya taa kwa mwezi Aprili, 2023 yanauzwa lita shilingi 2,921 ikiwa ni sawa na bei ya mwezi Machi, 2023 ambapo lita ilikuwa inauzwa kwa shilingi 2,921.

Wakati huo huo, ZURA imebainisha kuwa, mafuta ya ndege mwezi Aprili, 2023 lita inauzwa kwa shilingi 2,500 ikiwa kuna tofauti kubwa na mwezi Machi, 2023 kwani yalikuwa yanauzwa kwa shilingi 2,681.

Pia, ZURA imefafanua kuwa inaendelea kufuatilia na kudhibiti soko la mafuta na bei zake kwa ukaribu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha bei za bidhaa hizo haziongezeki mara dufu na kutolea athari katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

"Aidha, mamlaka inawahimiza wananchi kununua mafuta katika vituo halali vya mafuta na kudai risiti za kielektroniki kila wanaponunua mafuta,"imefafanua sehemu ya taarifa ya ZURA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news