Bunge latoa ufafanuzi madai ya kutunga kanuni mpya kwa wanahabari

NA DIRAMAKINI

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limetoa ufafanuzi kuhusu habari zilizochapishwa kwenye moja ya magazeti ya kila siku nchini na mitandao ya kijamii kuhusu madai ya kutungwa kwa kanuni mpya za Bunge hilo.

Ufafanuzi huo umetolewa kupitia taarifa iliyotolewa leo Aprili 2, 2023 na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa;Ofisi ya Bunge jijini Dodoma ikifafanua habari hiyo ya Machi 31, 2023 kupitia gazeti hilo liliandika taarifa yenye kichwa cha habari kinachosomeka “Bunge latunga kanuni mpya kwa wanahabari,wadau wang’aka”

Taarifa ya Bunge, imefafanua kuwa, katika taarifa hiyo gazeti lilirejea Kanuni za Bunge Toleo la Februari 2023 kwa kudai kuwa Kanuni hizo zimetungwa mwaka 2023.

"Maudhui ya taarifa hiyo yanalenga kuufahamisha umma kwamba Kanuni hizo zinarudisha nyuma uhuru wa habari kwa kuweka usiri katika shughuli za baadhi ya Kamati.

"Vilevile alieleza kuwa Kanuni zinaelekeza namna ya kupiga picha Bungeni hivyo kuwanyima uhuru wanahabari.
 
Katika taarifa hiyo inaonekana mwandishi aliwahoji Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Ndugu Deodatus Balile na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi Habari ya Dodoma, ndugu Mussa Yusuph ambao walitoa maoni kwamba watafanyia kazi taarifa hizo kwa kuchambua Kanuni, kuhoji na kuonana na Uongozi wa Bunge ili
kuwezesha kupatikana kwa Kanuni walizodai zitakuwa rafiki kwa waandishi wa habari.

"Zaidi ya taarifa hizo, katika mtandao wa kijamii wa Jamii Forums imewekwa taarifa yenye kichwa cha habari “Bunge lachapisha Kanuni mpya za Bunge zenye masharti kwa Waandishi wa Habari.” Taarifa hiyo imeeleza kuwa Bunge limetunga Kanuni mpya za mwaka 2023 zinazoweka masharti ya adhabu kwa waandishi wa habari na kutoa maelekezo mahsusi ya upigaji picha ndani ya Ukumbi wa Bunge.

"Taarifa hiyo imefafanua zaidi kwamba licha ya waandishi wa habari kutakiwa kuingiza kamera Bungeni kwa kibali, wakati wa kupiga picha kamera zinatakiwa zielekezwe kwa Spika au Mbunge anayezungumza wakati huo;

2.0 MASHARTI KUHUSU UANDISHI WA HABARI BUNGENI

Kanuni zinazosimamia ukusanyaji na utoaji habari Bungeni zimeainishwa katika Nyongeza ya Saba ya Kanuni za Kudumu za Bunge. Nyongeza hiyo ilikuwepo kwenye Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Januari, 2016.

Kutokana na uhitaji, Kanuni hizo zilifanyiwa maboresho ili ziweze kuongoza kwa ufanisi ukusanyaji na utoaji wa taarifa za Bunge. Kufuatia maboresho hayo Bunge lilijadili na kupitisha kwa njia ya Azimio Kanuni za Bunge zilizoitwa Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Juni, 2020.

Kabla ya kuanza kutumika, Kanuni hizo zilitangazwa kwenye gazeti la Serikali kupitia Tangazo la Serikali Na. 626 la tarehe 7 Agosti, 2020. Toka wakati huo masharti yanayoongoza waandishi wa habari Bungeni yamekuwa yakizingatiwa ipasavyo ambapo Ofisi ya Bunge haijawahi kupokea maoni wala malalamiko kutoka kwa mtu yeyote ikiwa ni pamoja na wadau wa habari.

3.0 KANUNI ZA BUNGE TOLEO LA FEBRUARI, 2023

Mnamo mwezi Februari, 2023 Mheshimiwa Spika kwa kushauriana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kanuni alifanya marekebisho kwenye Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Juni, 2020.

Marekebisho hayo yalilenga kuboresha muundo wa Kamati za Bunge ili kuendana na Wizara za Serikali kwa nia
ya kuleta ufanisi katika utendaji kazi wa Kamati.

Baada ya marekebisho hayo kufanyika Nyongeza ya Nane ya Kanuni ilitangazwa kwenye gazeti la Serikali kupitia
Tangazo la Serikali Na. 37A la tarehe 7 Februari, 2023.

Marekebisho hayo yaliunganishwa na Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Juni, 2020. Uunganishaji huo (revision) ulitekelezwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo Toleo la Februari, 2023 lilipatikana.

Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Februari, 2023 zinatokana na maboresho ya Nyongeza ya Nane inayohusu Kamati za Kudumu za Bunge. Hivyo, hakuna mabadiliko mengine yeyote yaliyofanyika katika Kanuni au
Nyongeza nyingine zilizobaki.

4.0 UPATIKANAJI WA HABARI ZINAZOHUSU SHUGHULI ZA BUNGE

Nyongeza ya Saba ya Kanuni za Kudumu za Bunge inatoa mwongozo wa kusimamia ukusanyaji na utoaji wa habari za Bunge.

Masharti yaliyomo kwenye Nyongeza hiyo yanaruhusu waandishi wa habari kutekeleza wajibu wao ikiwemo kupata habari zinazohusu shughuli mbalimbali za Bunge.

Habari hizo zimegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni habari za masuala ya kawaida na masuala ya faragha. Masuala ya faragha yamewekewa mipaka na utaratibu wa kuzingatia katika kuzipata na kuzitumia
taarifa hizo.

Vilevile Kanuni zimetaja Kamati ambazo vikao vyake vinapaswa kuwa vya siri kuwa ni Kamati ya Uongozi, Kamati ya Kanuni na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Aidha, Kamati nyingine za Bunge zimewekewa masharti ya kufanya vikao vyake kwa siri wakati zinapofanya kazi za kiuchunguzi.

Lengo la masharti hayo ni kutoathiri utendaji au matokeo ya kazi zinazofanywa na Kamati hadi pale taarifa zitakapowasilishwa Bungeni. Masharti yanayohusu upatikanaji wa habari za kawaida yametajwa katika Kanuni ya 6 na masuala ya faragha yametajwa katika kanuni ya 7 ya Nyongeza ya Saba ya Kanuni.

Ili kusimamia utekelezaji bora wa shughuli za Bunge, Bunge lilitunga Kanuni ya 4 na 5 za Nyongeza ya Saba ya Kanuni zinazosimamia upigaji picha katika ukumbi na maeneo mengine ya Bunge.

Kanuni hizo zimeelekeza utaratibu, namna na makatazo ya upigaji picha Bungeni. Lengo la masharti hayo ni kuhakikisha upigaji picha haungilii shughuli za Bunge.

5.0 HITIMISHO

Ni wazi kuwa maelezo ya waandishi kwamba Bunge limetunga Kanuni mpya za Toleo la Februari Mwaka 2023 si sahihi na zinapotosha. Vilevile maoni kuwa Kanuni za Bunge zinawanyima waandishi wa habari fursa ya kupata na kutoa habari siyo sahihi.

Kwa mujibu wa Masharti ya Kanuni za Bunge waandishi wanao uhuru wa kupiga picha na kutoa Habari za masuala mbalimbali yanayofanyika kwenye Ukumbi wa Bunge, Kamati zake na kwenye ziara za Kamati. Mambo machache yaliyowekewa masharti ya faragha yanaendana na misingi ya Haki, Kinga na Madaraka ambayo Bunge limepewa Kikatiba na kupitia Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura 296.

Kutokana na ufafanuzi wa hapo juu na ili kuepusha kuendelea kusambaa kwa upotoshaji dhidi ya Bunge, tunasisitiza kwamba:-
a) Waandishi wa habari wanao uhuru kutosha wa kuripoti habari za Bunge;
b) Bunge halijatunga Kanuni mpya za Mwaka 2023 kama inavyodaiwa;
c) Kanuni za Bunge zinazotoa mwongozo wa ukusanyaji na utoaji wa habari za
Bunge hazijabadilika na zimekuwa zikisimamia eneo hilo kwa ufanisi;
d) Ofisi ya Bunge imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wandishi wa habari katika utekelezaji wa shughuli za Bunge.

Aidha, Bunge limekuwa likiacha milango wazi ili kupokea maoni na ushauri kwa nia ya kuboresha shughuli za Bunge; na
e) Ofisi ya Bunge inapenda kuwakumbusha waandishi wa habari juu ya umuhimu wa kuzingatia misingi ya uandishi wa habari ikiwemo inayowataka kupata taarifa sahihi kutoka kwa Taasisi husika kabla ya kuchapisha taarifa ili
kuepusha upotoshaji na taharuki inayoweza kujitokeza kwa jamii,"imefafanua kwa kina taarifa hiyo ya Bunge.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news