Dkt.Kongela awapa mbinu watumishi NHC kuyafikia malengo, matarajio kwa ustawi bora wa shirika

NA GODFREY NNKO

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dkt.Sophia Kongela amewataka watumishi wa shirika hilo kutekeleza majukumu yao ya kazi kwa kuzingatia kanuni, taratibu na kwa uadilifu mkubwa ili kuweza kuyafikia matarajio na malengo ya shirika kupitia Sekta ya Nyumba nchini.
Dkt.Kongela ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba (NHC) 2023 ameyasema hayo leo Aprili 3, 2023 makamo makuu ya shirika Kambarage House jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo umewaleta pamoja menejimenti ya shirika, viongozi wa shirika kutoka katika mikoa na wawakilishi wa wafanyakazi kutoka katika mikoa ya shirika kwa kuzingatia muundo wa mkataba wa baraza.

"Kama mnavyokumbuka, shirika kwa mwaka mmoja uliopita lilikuwa likipitia mpango mkakati wa muundo wake, na lengo la mapitio hayo ilikuwa ni kuwa na mpango mkakati unaojibu matarajio ya watanzania katika sekta ya nyumba. 
"Ili kuweza kutekeleza mpango mkakati huo ilibidi pia, kupitia muundo wetu kwa lengo la kuufanya muundo huo uweze kubeba majukumu yaliyoainishwa kwenye mpango mkakati. Mpango mkakati huo na muundo wa utumishi wa shirika ulishapitishwa na bodi yenu na kuridhiwa na mamlaka husika.

"Na ninaamini mtaendelea kuelimishana ili kila mfanyakazi aweze kushiriki kikamilifu katika kuutekeleza ipasavyo mipango yote ya shirika ipasavyo.
"Na hili jambo kwa kweli ni la muhimu sana, kwani hata kama tutakuwa na sera,sheria na kanuni nzuri kiasi gani, katika mahali pa kazi pasipokuwa na uelewa wa pamoja na ushirikiano baina ya mwajiri na watumishi inakuwa vigumu sana kwa taasisi kutimiza malengo yake. Hivyo mlitumie baraza hili kulishauri shirika kwa lengo la kuleta tija na ufanisi katika shirika,"amefafanua kwa kina Dkt.Kongela.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dkt.Sophia Kongela amesema, anatarajia kupitia uadilifu kwa watumishi kutaliwezesha shirika hilo la umma kustawi na kufikia matokeo chanya.

"Tumepewa dhamana ya kusimamia hili shirika kuhakikisha Sekta ya Nyumba nchini inakuwa, hivyo tufanye kazi kwa bidii,"amesema.
Amesema, bodi yake inapenda kuona kila mfanyakazi wa shirika ambaye anafanya kazi vizuri katika utekelezaji wa maadili ya msingi wa shirika anapatiwa pongezi na stahiki zake.

"Lakini pia, kwa mfanyakazi ambaye hatekelezi majukumu yake kwa uadilifu achukuliwe hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yake, hauwezi kuwa unapongeza,na kuna mwingine anakuwa hafanyi vizuri ukawa unamuona kwamba yuko sahihi, hapana. 

"Kwa hiyo wakupongezwa wapongezwe, ambao wanahitaji kuchukuliwa hatua za kinidhamu wachukuliwe kwa taratibu zilizopo ili kuhakikisha watumishi wote wanafanya kazi kama timu na kwa kuzingatia maadili ya shirika yanayotuongoza.
"Bodi ya shirtika ipo tayari kumpongeza mtumishi mbunifu yeyote atakayelisaidia shirika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, na vile vile haitamvumilia yeyote mzembe asiyetimiza wajibu wake.Kwa sababu, mwisho wa siku tunaumia wote,"amefafanua Dkt.Kongela.

Madeni

Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi ameeleza umuhimu wa kuweka na kutekeleza mikakati thabiti itakayofanikisha ukusanyaji wa madeni yote ambayo yanadaiwa na shirika katika maeneo mbalimbali nchini ili yaweze kujenga nyumba mpya.

Amesema, mpango mkakati wa miaka 10 wa shirika hilo ambao unaelekeza ufanyike ujenzi wa nyumba zaidi ya 10,000 nchini, hautafikiwa ikiwa shirika litashindwa kukusanya madeni hayo kwa wakati.

"Tuhakikishe madeni yote yanakusanywa kwa ufanisi ili kuwezesha ujenzi wa nyumba nyingi nchini, ninaamini kila mmoja akiwajibika kikamilifu hayo yote yatafanikiwa,"amesisitiza.

Mwenyekiti wa Baraza

Awali akimkaribisha mgeni rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dkt.Sophia Kongela, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba (NHC) ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa shirika, Hamad Abdallah amesema kuwa, mkutano huo una umuhimu mkubwa katika shirika hilo.
Pia amesema kuwa, dhamira kubwa ya baraza huwa ni kupitisha bajeti ya shirika, "kabla ya kuja katika kikao chako cha bodi, bajeti huwa inaandaliwa katika hatua tofauti, huwa inaanzia katika ngazi za mikoa, inakuja kwenye menejimenti kunakuwa na majadiliano ya kina. 

"Baada ya hapo kwa mujibu wa taratibu inakuja kwenye kikao cha baraza, ambacho ndicho kikao hiki, nacho pia huwa kinapitia na kutoa maoni yao,na kama kuna maboresho kisha inakuja kwenye vikao vya bodi,"amefafanua Abdallah.
Amesema, hicho ni kikao ambacho wafanyakazi kwa kada tofauti huwa wanashiriki katika kuandaa mpango, kwa sababu bajeti ndiyo mpango wa mwaka ujao wa fedha, wakiangazia wanaenda kufanya nini na wanataka kufanikisha nini.

"Na hili kulifanya hilo vizuri, tulianza mkutano wetu jana, tukianza na Extended Management Team, lakini katika mkutano huo tuliwaalika wajumbe wa baraza ambao hawaingii kwa kawaida katika Extended Management Team, sababu za kufanya hivyo ni ili waweze kuangalia uwasilishaji wa taarifa za mikoa, lakini vile vile na uwasilishaji wa taarifa za kurugenzi mbalimbali. "Ili waweze kuangalia hatua ambayo tunapiga, lakini viler vile tuna changamoto gani. Na kuweza vile vile kushiriki katika kutoa suluhisho la kutatua changamoto hizo,"ameongeza Mwenyekiti huyo wa Baraza la Wafanyakazi na Mkurugenzi Mkuu wa NHC.

Shukurani

Wakati huo huo, akitoa neno la shukurani kwa niaba ya wajumbe wa baraza hilo, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Fatma Chillo amesema kuwa, wameyapokea maelekezo, mapendekezo na maagizo ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dkt.Sophia Kongela ili kuendelea kuongeza ufanisi katika shirika.
"Tukuahidi yale yote ambayo umeyazungumza,maagizo uliyoyatoa na mapendekezo, sisi wana NHC tumeyapokea na tunakuhaidi tutayafanyia kazi kwa nguvu zetu zote na kwa uadilifu. Tutahakikisha tunafanya kazi kwa bidii ili tuweze kujenga shirika letu, ili tuweze kujenga Taifa lilo bora, taifa lenye afya, Taifa lenye nidhamu pia kuweza kuendeleza maendeleo kwa namna ambavyo tumepewa majukumu sisi watendaji,"amefafanua Chillo. 

Tuzo

Kupitia mkutano huo, dereva wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mkoa wa Kilimanjaro, Joseph Kamundi ametunukiwa tuzo na vocha ya fedha taslimu shilingi milioni 10, aliyozawadiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah, kufuatia kufurahishwa na dereva huyo, kulitunza gari la Shirika la Nyumba la Taifa na kuokoa fedha nyingi ambazo zingetumika kufanyia matengenezo. 
Tuzo hiyo ni mwendelezo wa juhudi za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) za kuendelea kutambua na kuthamini michango ya wafanyakazi wanaofanya kazi kwa bidii ndani ya shirika ili kuliwezesha kuyafikia malengo yake.

Meneja Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),Bw.Muungano Saguya akisoma wasifu amesema, miongoni mwa vigezo ambavyo vinamuwezesha mfanyakazi kuwa bora zaidi ni pamoja na kuonesha nidhamu ya hali ya juu kwa manufaa ya shirika.
Jambo lingine ni mfanyakazi kutunza mali za shirika ili ziweze kudumu, kuokoa gharama za uendeshaji katika vitengo au idara ikiwemo kuongeza uzalishaji kwa ustawi bora wa shirika. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news