NA MWANDISHI WETU
MWENYEKITI wa Kamati ya Michezo ya Kombe la Mei Mosi Taifa 2023 ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ta Kondoa, Dkt Khamis Mkanachi Aprili 19, 2023 ametoa elimu kuhusu kanuni na taratibu za michezo hiyo, ambayo inashirikisha wafanyakazi wa taasisi za umma na binafsi.
Dkt. Mkanachi amesema kanuni za michezo hiyo kipengele namba 13 kinaruhusu wafanyakazi wa kudumu na wa mkataba kuanzia miezi sita na kuendelea, vimeelezea sifa za watumishi hao na adhabu ambazo timu itaadhibiwa kulingana na kosa la kuchezesha mchezaji ambaye sio mwajiriwa wa kudumu maarufu kama mamluki.
“Kanuni za michezo hii zimeandaliwa kwenye kikao cha pamoja cha Kamati ya Maandalizi ambacho kilifanyika Machi 2023, na kila klabu imekuwa ikiwasomea washiriki wao, ili waepuke kukiuka kanuni na taratibu zetu za michezo hii, ambayo ni kisherehekeshaji cha kabla ya Sherehe za Wafanyakazi Duniani ambazo hufanyika Mei Mosi,” amesema Dkt. Mkanachi.
Amesema, michezo ya mwaka huu inashirikisha timu 33 kutoka kwenye mashirikisho makubwa manne ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), Shirikisho la michezo ya taasisi za umma na binafsi (SHIMMUTA), shirikisho la michezo ya Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA) na Shirikisho la michezo ya majeshi (BAMMATA), ambapo wanachezo michezo ya soka, netiboli, mpira wa wavu, kuvuta kamba, riadha, karata, bao na draft.
Hata hivyo, akizungumzia rufaa iliyokatwa na timu ya Benki ya CRDB kwa Kamati ya mashindano wakipinga kupokwa pointi sita walizopata baada ya kuwafunga Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na RAS Dodoma kutokana na kuchezesha wachezaji ambao sio wafanyakazi halali wa ofisi hiyo, amesema baada ya kupitia maelezo ya pande zote ya CRDB na Kamati ya Rufaa, walijiridhisha maamuzi ya awali yaliyotolewa kuwa wapokwe pointi tatu pekee kutokana na TRA kukata rufaa, lakini warudishiwe pointi tatu za RAS Dodoma maana hawakukatiwa rufaa.
“Kamati yangu ilifanya mazungumzo na Kamati ya Rufaa, na kugundua iliwaita TRA na CRDB na zaidi ilizungumza na wale wachezaji waliokatiwa rufaa na ilibainika kuwa kati ya wale wachezaji watatu waliokatiwa rufaa na waligundulika sio wawili watumishi halali kutokana na kutokuwa na vielelezo vinavyomtambulisha mtumishi ikiwemo vitambulisho vya kazi na hati ya mshahara, ila walikuwa na barua ya kuonesha ni wafanyakazi mafunzoni yaani internship, ambao katika kanuni za michezo yetu hawaruhusiwi,” amesema Dkt. Mkanachi.
Lakini amesema wachezaji hao wamezuiwa tu kushiriki kwenye michezo hiyo na sio kuzuiwa kuendelea kufanya kazi na Benki ya CRDB, hivyo waendelee kuwatumika kama walivyokuwa wanawatumiwa lakini waangalie taratibu zao za ajira ili wachezaji hao waendelee kuwasaidia pia katika eneo la michezo hatua itakayowasaidia kuwatumia mwakani kihalali katika michezo hii, ambayo inafanyika kila mwaka kwenye mkoa utakaopendekezwa.
Pia amesema wameichukua changamoto hiyo ya kikanuni ili kwa mwakani waweze kupanua wigo wa ushiriki wa watumishi kwenye michezo hii kwa kuboresha kanuni na taratibu hatua itakayosaidia kupata timu nyingi zaidi zitazoshiriki kwani wapo wananchi waliojiajiri wakiwemo waendesha bodaboda, au mama na baba lishe wanastahili kushiriki pia.