NA DIRAMAKINI
WAZAZI na walezi wamehimizwa kuhakikisha wanachangia chakula kwa ajili ya watoto wao ili kula wawapo shuleni, hatua ambayo itasaidia kuinua kiwango chao cha taaluma, ufaulu na kuwawezesha kusoma kwa ufanisi.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Diwani Kata ya Mshikamano iliyopo Manispaa ya Musoma, Mhandisi Charles Mwita wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu wa Shule ya Sekondari Mshikamano iliyopo Manispaa ya Musoma kwa matokeo mazuri ya kidato cha nne mwaka 2022.
"Suala la chakula ni muhimu sana, halikwepeki lazima lizingatiwa sana ili wanafunzi waweze kusoma kwa ufanisi wawapo shuleni, hii itasaidia kuinua ufaulu wao na kuimarisha mahudhurio yao,"amesema Mheshimiwa Charles Mwita.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Mshikamano, Mwalimu George Mugeta amesema, shule imepata mafanikio katika maeneo ya taaluma, nidhamu na baadhi ya wanafunzi wanapata chakula cha mchana shuleni.
Mwalimu Mugeta amesema, shule hiyo inayo mikakati ya kuinua hali ya taaluma ikiwa ni pamoja na kushirikisha wazazi kufuatialia matokeo ya wanafunzi au watoto wao pamoja na kufuatilia maendeleo yao ya kitaaluma.
Mkuu huyo wa shule amesema, ufaulu wa matokeo ya kidato cha nne mwaka jana kwa wanafunzi wa kidato cha nne Daraja la Kwanza Wanafunzi ni 17, Daraja la Pili wanafunzi 27, Daraja la tatu ni 34, Daraja la Nne ni 93, Waliopata Daraja 0 ni wanafunzi 28.
Aidha, Shule ya Sekondari Mshikamano inakabiliwa na upungufu wa walimu wa masomo ya Sayansi, Nyumba za Walimu, Vyumba vya madarasa na Matundu ya Vyoo 41.
"Bado kuna mtazamo hasi kwa baadhi ya Wanajamii kudhani kuwa mambo yote yanafanywa na Serikali wanao mtazamo wa kuwa wajibu wa kuboresha miundombinu ya shule ni jukumu la serikali,"amesema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Mshikamano, Robinson Wangaso amesema, kuimarisha mazingira ya kuinua hali ya taaluma ya shule ni jambo mtambuka, kwani ni jukumu na wajibu wa kila mdau wakiwemo wazazi na walezi wa kata hiyo wote katika kuboresha mazingira ya shule wanalo jukumu la kufanya hivyo.
Wangaso amesema, Serikali inayo majukumu mengi, hivyo wananachi kama wadau muhimu katika kuendesha na kusimamia shule wanapaswa kuwa na mpango mkakati shirikishi katika kushughulikia changamoto zinazoikabili Shule hiyo ili kuzipatia ufumbuzi badala ya kuichia serikali pekee.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Mshikamano, Nanyika Chaki amesema, Serikali ngazi ya kata itahakikisha wanafunzi watoro wanachukuliwa hatua stahiki ili kuboresha mahudhurio katika shule hiyo.
Katika hafla hiyo zawadi na tuzo za vyeti zilitolewa kwa walimu watano ambao walipata ufaulu wa daraja A katika Masomo waliofundisha ambayo ni Bailojia, Kemia, Historia, Kiswahili na Kiingereza.