Gavana Tutuba:Mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri misingi ya usimamizi wa uchumi

NA GODFREY NNKO

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba amesema, nguvu ya pamoja katika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi inahitajika hususani kuendelea kuyatunza mazingira, kwani madhara yake ni makubwa katika Sekta ya Uchumi.
"Pia kuna changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo kwenye mikutano (Benki ya Dunia na IMF hivi karibuni) iliongelewa sana, ni janga kubwa ambalo linaathiri misingi ya usimamizi wa uchumi.

"Kwa sababu linaharibu uzalishaji,lakini linaharibu mauzo nje,na linaharibu hata mfumuko wa bei kwa sababu unapotokea uhaba wa vitu ndivyo mchakato wote unaathirika."

Amesema,kwa kuliona hilo jumuiya ya Kimataifa imeamua kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha wanapata ufumbuzi ambao utasaidia kila nchi kupata usaidizi wa kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Pia amesema, kadri joto linavyoongezeka duniani ndivyo yanavyotokea majanga mengine yakiwemo mafuriko na milipuko ya magonjwa ambayo yanaathari mbaya katika ukuaji wa uchumi."Kwa hiyo tuendelee kuchukua hatua kadri inavyohitajika, vivyo hivyo tuendelee kumuomba Mwenyenzi Mungu; 

Gavana Tutuba ambaye alikuwa mgeni rasmi katika futari iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa wafanyakazi wake, majirani wa benki, watoto wa madrasa, makundi maalumu wakiwemo wadau mbalimbali ameyasema hayo Aprili 20, 2023 katika makao makuu madogo ya benki hiyo jijini Dar es Salaam.

Amesema, tukio kama hilo la kuwafuturisha wadau mbalimbali mbali na Dar es Salaam limefanyika pia katika matawi yote ya benki ikiwemo makao makuu jijini Dodoma, makao makuu madogo jijini Zanzibar, matawi ya Mtwara, Arusha, Mbeya na Mwanza.

Pia amewashukuru wadau wote ambao wameitikia wito wao wa kushiriki pamoja katika futari hiyo. "Tunashukuru sana kwa kujumuika kwenu na sisi,tunaamini sadaka ya kwanza na sadaka ya mwisho zote ni sadaka zinaenda kwa Mwenyenzi Mungu,kwa hiyo tunashukuru sana kwa kujumuika kwenu na sisi kama Benki Kuu ya Tanzania kama sehemu ya jamii tunayoishi.

"Taasisi hii ina watumishi Waislamu na Wakristo na inawezekana wapo ambao hawana dini pia, lakini wote tunatengeneza taasisi moja ambapo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa uhuru wa kila mmoja kuabudu kulingana na imani yake, ilimradi asiathiri taratibu za wenzake.
"Kwa hiyo, sisi tuliona ni jambo jema kuandaa kwa pamoja, ikiwa ni hatua moja wapo ya kuwapongeza watumishi wenzetu ambao ni Waislamu ambao Mwenyenzi Mungu amewatunuku ari na afya ya kufanya kazi kwa bidii katika kipindi chote cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kwa hiyo, niendelee kuwapongeza Waislamu wote ambao wameendelea kufanya kazi vizuri katika kipindi hiki cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani."

Amesema, katika mikutano ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) hivi karibuni ambayo alishiriki, alishuhudia watu wakiipongeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na jitihada zake za kuimarisha uchumi ambazo zinaonesha matokeo chanya.

“Juzi nilikuwa kwenye mikutano ya Benki ya Dunia na IMF wameisifu nchi yetu kwa usimamizi mzuri wa uchumi ikilinganishwa na mataifa mengine duniani."
Katika hatua nyingine, Gavana Tutuba amesema, ili Taifa liweze kufikia malengo makubwa katika kustawisha uchumi wake, kila Mtanzania anapaswa kufanya kazi kwa bidii.

"Sisi kama Benki Kuu tunaendelea kusimamia uchumi wa nchi yetu na niwahakikishie uchumi wetu uko imara, mfumuko wa bei umedhibitiwa na fedha yetu pia iko imara, sekta ya fedha inazidi kukua.

“Ninachoomba kutoka kwenu ni ushirikiano wa kila mmoja, tufanye kazi kwa bidii ili tuimarishe uchumi, kwa sababu uchumi imara hutokana na uzalishaji, tukiweza kuzalisha zaidi na sekta itakuwa,tukiweza kusimamia zile micro economic basi na kiwango cha ukuaji wa uchumi kitaendelea vizuri,"amefafanua Gavana Tutuba.

Pia amewaomba kuendelea kuliombea Taifa liendelee kuwa na mshikamano, umoja,amani na liendelee kuweka mazingira mazuri zaidi ya watu kufanya kazi na kujituma, kwani mataifa ambayo yana changamoto ya migogoro yameshindwa kufikia malengo ya kukuza uchumi.

RC Dar

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Amos Makalla, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa kuandaa hafla hiyo ambayo imeyakutanisha makundi mbalimbali katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani.
"Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa niwapongeze sana Benki Kuu kwa sadaka hii kubwa,"amefafanua Mheshimiwa Mpogolo huku akisisitiza kuwa, mafundisho ya viongozi wa dini katika kipindi chote cha mfungo yamekuwa na nguvu kubwa katika kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano nchini.

Pia amesema, mawaidha yaliyotolewa katika hafla hiyo ambayo yaliangazia katika nguzo muhimu za kiuchumi kila mmoja akiyafanyia kazi hususani kufanya kazi kwa bidii, Taifa litazidi kusonga mbele kiuchumi.

Nguzo za uchumi

Kwa upande wake, Imam wa Msikiti wa Maamour Upanga jijini Dar es Salaam, Sheikh Issa Othman (Mufti London) ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Maulama amesema, kuna misingi sita inayoelezea Uislamu na Uchumi ambayo ni Udugu, Kufanya Wema, Ushauri Nasaha, Kuheshimu Makubaliano, Hofu ya Mungu, na Huruma au Kuhurumiana.

Amesema, uchumi unaojengwa kwenye misingi hiyo huwa ni imara ambapo mmoja hawezi kujichukulia maamuzi kujinufaisha mwenyewe au kumuumiza mwingine na mara zote wema huwa unatawala ikiwemo hofu ya Mungu.

Naye Sheikh Muharram Mziwanda amesema,umoja, mshikamano ni miongoni mwa mambo muhimu ambayo yanapaswa kuzingatiwa katika kuhakikisha uchumi unaendelea kustawi.
Picha zote na Benki Kuu.

"Niwaombeni, kila mmoja alikotoka tuhakikishe tunatengeneza amani, ifike wakati katika kazi zetu, hebu acha kushughulika na mambo ya wengine, shughulika na mambo yako.

"Tuhakikishe tunaendelea kuenzi amani na utulivu kila mmoja kwenye nafasi zetu na tuchape kazi kwa bidii, uchumi unahitaji kuchapa kazi, tukifanya hivyo,tutaona matokeo,"amefafanua.

Majukumu ya BoT

Jukumu la msingi la Benki Kuu ya Tanzania ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei na kujenga mfumo wa fedha ulio imara na unaofaa kwa ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa.

Majukumu mengine ya Benki Kuu ya Tanzania ni kutoa sarafu ya nchi ambayo ni Shilingi ya Tanzania, kusimamia na kudhibiti mabenki na taasisi za fedha.

Pia, kusimamia na kudhibiti mifumo ya malipo nchini,kuhifadhi akiba ya nchi ikiwemo fedha za kigeni, Benki ya Serikali, Benki ya Mabenki na kutoa ushauri juu ya masuala ya uchumi na fedha kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news