HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM MAJALIWA MAJALIWA (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2023/2024
UTANGULIZI
Shukrani
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge za Utawala, Katiba na Sheria; Afya na Masuala ya UKIMWI; Ustawi na Maendeleo ya Jamii; na Bajeti zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mfuko wa Bunge, sasa naliomba Bunge lako lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2022/2023 na Mwelekeo wa Kazi zake kwa mwaka 2023/2024.

Aidha, naomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa fadhila zake ambazo zimetuwezesha kukutana hapa leo kwa ajili ya kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2022/2023 na mwelekeo wake kwa mwaka 2023/2024 tukiwa wenye afya njema.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa huu ni Mkutano wa 11 wa Bunge la 12 ambao ni mahsusi kwa ajili ya mjadala wa bajeti.

Niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tuitumie vyema fursa hii kutoa maoni na ushauri ili kuisaidia Serikali kuimarisha utekelezaji wa vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango na Bajeti ya Mwaka 2023/2024.
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali itapokea maoni na ushauri wenu na kuyafanyia kazi kwa maslahi mapana ya wananchi.
Salamu za Pole
Mheshimiwa Spika, nchi yetu kwa nyakati tofauti imekumbwa na maafa na matukio mbalimbali yaliyosababisha athari mbalimbali zikiwemo vifo, majeruhi, na uharibifu wa mali na mazingira.

Nitumie fursa hii kuwapa pole Watanzania wote waliopoteza ndugu, jamaa na mali zao katika maafa. Aidha, ninamwomba Mwenyezi Mungu awajalie majeruhi wote uponyaji wa haraka na aendelee kuwapumzisha kwa amani wale waliopoteza maisha.
Salamu za Pongezi
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutuongoza vyema na kupata maendeleo na mafanikio makubwa katika kipindi kifupi cha miaka miwili ya uongozi wake. Mafanikio hayo ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu na huduma za afya, maji, elimu, umeme na uchukuzi, kuboresha hali ya chakula na lishe na kuimarisha hali ya kisiasa nchini na mahusiano ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kutokana na uongozi wao makini na jitihada zao katika kuhakikisha Taifa letu linapata maendeleo.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya teuzi na mabadiliko ya baadhi ya watendaji wakuu wa taasisi na viongozi wa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mabadiliko hayo, yamelenga kuimarisha utendaji kazi Serikalini ikiwa ni pamoja na utoaji huduma bora na kushughulikia kero mbalimbali za wananchi.
Mheshimiwa Spika, ninawapongeza viongozi na watendaji wote walioteuliwa na Mheshimiwa Rais wetu mpendwa kushika nyadhifa mbalimbali. Kipekee, niwapongeze Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama Mbunge wa Peramiho na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu; Mheshimiwa George Boniface Simbachawene Mbunge wa Kibakwe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora; na Mheshimiwa Abdallah Hamis Ulega Mbunge wa Mkuranga na Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Vilevile, nimpongeze Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwinjuma almaarufu Mwana FA, Mbunge wa Jimbo la Muheza kwa kuteuliwa kushika nafasi ya Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Ninawatakia kila la kheri viongozi wote walioteuliwa katika utekelezaji wa majukumu yao mapya.
Mheshimiwa Spika, vilevile, nitumie fursa hii kuwasisitiza wateuliwa wote kuzingatia maelekezo mbalimbali ya Mheshimiwa Rais yakiwemo aliyatoa kwenye semina ya viongozi iliyofanyika hivi karibuni, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 pamoja na mipango ya kitaifa na kimataifa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, natoa rai kwa viongozi hao kuhakikisha wanatanguliza mbele maslahi ya Taifa na kuwahudumia wananchi ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kukupongeza wewe binafsi kwa kuliongoza Bunge hili kwa hekima na umahiri mkubwa. Nimpongeze pia Mheshimiwa Naibu Spika kwa namna ambavyo ameendelea kusimamia shughuli za Bunge kwa uwezo mkubwa. Waheshimiwa Wabunge wenzangu hakika mtakubaliana nami kuwa Viongozi hawa ni makini sana na wameonesha ukomavu mkubwa wa kisiasa wakati wote wakiendesha vikao vya Bunge hili. Nitoe wito kwetu sote tuendelee kuwapa ushirikiano ili waendelee kuliongoza vema Bunge letu na kulifanya liendelee kuheshimika ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii, kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Madaba na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria; Mheshimiwa Stansilaus Nyongo, Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI; Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalumu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii; Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Babati Vijijini na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na wajumbe wote wa kamati hizo kwa michango yao iliyosaidia kuboresha Mpango na Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mfuko wa Bunge.
Mheshimiwa Spika, ninatambua ulifanya mabadiliko ya Wenyeviti na Wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge. Nitumie fursa hii kuwapongeza sana wote walioteuliwa na kuwatakia kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yao. Vilevile, ninawashukuru sana Wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge lako tukufu kwa ushauri walioutoa wakati wa kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Maoni na ushauri wao utazingatiwa vilivyo wakati wa utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2023/2024.
Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu lilifanya uchaguzi wa wenyeviti wa Bunge ambao watakusaidia kuongoza vikao vya Bunge. Niwapongeze Mheshimiwa Najma Murtaza Giga Mbunge wa Viti Maaalum na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, na Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile Mbunge wa Mufindi Kusini na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kwa kuchaguliwa kuwa wenyeviti wa Bunge. Nawapongeza sana na kuwatakia majukumu mema ya kuliongoza Bunge.
Mheshimiwa Spika, ninawashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri; Katibu Mkuu Kiongozi; Wakuu wa Mikoa; Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Makatibu Wakuu; Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Naibu Makatibu Wakuu; na Wakuu wa Wilaya, Idara, Mashirika, Wakala na Taasisi zote za Serikali kwa ushirikiano mkubwa mnaonipa katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kipekee, niwapongeze na kuwashukuru wafanyakazi wote wa Serikali na taasisi zake kwa kufanya kazi kwa weledi, utaalamu na umahiri mkubwa na hivyo, kuwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee, nawashukuru Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, Mbunge wa Peramiho na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu); Mheshimiwa Profesa Joyce Lazaro Ndalichako, Mbunge wa Kasulu Mjini na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu); Mheshimiwa Paschal Patrobas Katambi, Mbunge wa Shinyanga Mjini na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na Mheshimiwa Ummy Hamis Nderiananga, Mbunge wa Viti Maalumu na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu.
Mheshimiwa Spika, vilevile, nawashukuru sana Dkt. Jim James Yonazi, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu); Prof. Jamal Adam Katundu, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu); Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo; Wakuu wa taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu; Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu na wafanyakazi wote kwa ushirikiano mkubwa wanaonipatia wakati nikitekeleza majukumu yangu.

Aidha, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitamshukuru Mheshimiwa George Boniface Simbachawene Mbunge wa Kibakwe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. John Antony Kiangu Jingu, Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu na Bwana Kaspar Kaspar Mmuya, Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa ushirikiano walionipa wakati wakiwa Waziri wa Nchi, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu mtawalia katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu). Ahsanteni na Hongereni Sana!
Mheshimiwa Spika, ninapenda pia kuzishukuru sekta binafsi, nchi rafiki, washirika wa maendeleo, taasisi na mashirika ya kimataifa na madhehebu ya dini kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuleta maendeleo. Serikali inatambua na kuthamini michango yenu hususan katika utekelezaji wa afua muhimu kwa kutoa misaada, mikopo nafuu na wakati mwingine utaalamu, kitendo ambacho kimekuwa chachu ya kuharakisha maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba kuwasilisha makadirio ya bajeti ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa vipaumbele vilivyobainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020; maelekezo ya nyaraka za kisera za kitaifa, kikanda na kimataifa ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki 2050, Ajenda 2063 ya Maendeleo ya Afrika, Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano, na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/2024.
UTEKELEZAJI WA MIRADI YA KIPAUMBELE KWA MWAKA 2022/2023
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo itakayoimarisha uchumi wa nchi na maendeleo ya watu. Hadi kufikia Januari, 2023 zimetolewa takribani Shilingi trilioni 8.64 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya reli, barabara, viwanja vya ndege, huduma za jamii na nishati. Utekelezaji wa miradi hiyo upo katika hatua mbalimbali kama ifuatavyo:
Mosi: Ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR)
Serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 762.99 kutekeleza mradi huo ambapo kipande cha Dar es Salaam Morogoro (km 300) utekelezaji umefikia asilimia 97.91; kipande cha Morogoro Makutupora (km 422) asilimia 92.23; kipande cha Mwanza - Isaka (km 341) asilimia 25.75; kipande cha Makutupora - Tabora (km 371) asilimia 4.59; na kuanza kwa ujenzi wa kipande cha Tabora - Isaka (km 165) na Tabora Kigoma (Km 506).
Pili: Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2,115)
Serikali imetoa takribani Shilingi bilioni 869.93 kwa ajili utekelezaji wa mradi huu ambao umefikia asilimia 83. Zoezi la ujazaji maji katika bwawa lilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Desemba 2022. Hadi Februari, 2023 kiwango cha maji kimefikia mita 134.39 kutoka usawa wa Bahari ikilinganishwa na kiwango cha mita 163 kinachohitajika ili kuanza uzalishaji.
Tatu: Uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania
Utekelezaji wa mradi huu umegharimu takribani Shilingi bilioni 20.52. Shughuli zilizofanyika ni pamoja na kulipa sehemu ya gharama za ununuzi wa ndege tano ambapo kati ya hizo, ndege moja ni aina ya Boeing 767-300F ya mizigo, ndege mbili aina ya Boeing 737-9, ndege moja aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na ndege moja aina ya De Havilland Dash 8-Q400. Ndege nne kati ya hizo zinatarajiwa kuwasili nchini kabla ya Novemba, 2023 na ndege moja ya mizigo inatazamiwa kuwasili nchini hivi karibuni. Kuwasili kwa ndege hizo kutasaidia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutanua mtandao wa safari za ndani na nje ya nchi na hivyo kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za uchumi kama utalii, biashara na kilimo.
Nne: Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania) lenye urefu wa km 1,443
Takribani shilingi bilioni 30.39 zimetolewa ili kulipa fidia wananchi 7,486 kati ya 9,122 wanaopisha eneo la mkuza wa bomba; na Serikali imeendelea kulipa hisa za umiliki katika Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki hadi kufikia dola za Marekani milioni 131.0. Aidha, tayari kibali cha kuanza ujenzi wa Bomba la Mafuta kimetolewa Januari, 2023. Vilevile, ujenzi wa karakana ya kuweka mfumo wa kupasha joto mabomba katika kijiji cha Sojo, Nzega Tabora umefikia asilimia 49.
Tano: Mradi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi
Takribani shilingi bilioni 39.84 zimetolewa ili kuendelea na ujenzi wa kiwanda ambao umefikia asilimia 75. Aidha, hekta 219 zimepandwa miwa na kufanya ukubwa wa eneo lililopandwa miwa kufikia hekta 2,974 sawa na asilimia 83 ya lengo la kupanda hekta 3,600. Kiwanda hicho kinatarajiwa kuongeza uzalishaji wa tani 50,000 za sukari kwa mwaka pindi kitakapoanza uzalishaji na hivyo kupunguza mahitaji ya kuagiza sukari nje ya nchi.
Sita: Mradi wa Daraja la Kigongo Busisi (Mwanza)
Takribani shilingi bilioni 93.09 zimetolewa kuendelea na ujenzi wa daraja hili ambao umefikia asilimia 63. Kukamilika kwa Daraja hili kutapunguza muda wa Wananchi kuvuka eneo la Kigongo Busisi kutoka takribani masaa 2 mpaka dakika 4 kwa kutumia usafiri wa gari na dakika 10 kwa watembea kwa miguu. Aidha, daraja hili litakuwa na uwezo wa kupitisha magari ya aina yote wakati wote na kubeba uzito wa hadi tani 160.
Saba: Miradi ya Ujenzi na Ukarabati wa Viwanja vya Ndege
Serikali ilitoa takribani shilingi bilioni 77.23 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ambapo utekelezaji umefikia asilimia 10.2. Kazi nyingine ni kukamilika kwa upanuzi wa njia ya kutua na kuruka ndege na kufungwa kwa mfumo wa kuongozea ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Dodoma; kukamilika kwa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Geita; na kuendelea na ujenzi na ukarabati wa Viwanja vya Ndege vya Songea kwa asilimia 98, Iringa asilimia 42 na Musoma asilimia 43.
HALI YA UCHUMI
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja sasa, Dunia imekumbwa na msukosuko wa kiuchumi kutokana na vita inayoendelea baina ya nchi za Ukraine na Urusi. Vita hiyo ilianza wakati uchumi wa dunia ukiwa bado haujatengemaa kutoka kwenye madhara ya janga la UVIKO 19. Kwa msingi huo, tumeshuhudia uchumi wa mataifa makubwa hususan katika bara la Ulaya ukiyumba na gharama za maisha kuongezeka kutokana na mfumuko wa bei za nishati na chakula duniani.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Fedha la Duniani ya Januari, 2023, kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia imepungua kutoka asilimia 6.2 mwaka 2021 hadi asilimia 3.4 mwaka 2022. Aidha, kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia inatarajia kupungua na kufikia asilimia 2.9 mwaka 2023. Vilevile, kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi zilizoendelea imepungua na kufikia asilimia 2.7 mwaka 2022 kutoka asilimia 5.4 mwaka 2021 na inatarajiwa kupungua na kufikia asilimia 1.2 mwaka 2023.
Mheshimiwa Spika, uchumi wa nchi zinazoendelea na zinazoibuka kiuchumi ulipungua na kufikia asilimia 3.9 mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 6.7 mwaka 2021. Aidha, ukuaji wa uchumi katika nchi zinazoendelea na zinazoibuka kiuchumi barani Asia, ikijumuisha China na India ulipungua na kufikia asilimia 4.3 mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 7.4 mwaka 2021. Kwa upande wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ukuaji wa uchumi ulipungua na kufikia wastani wa asilimia 3.8 mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 4.7 mwaka 2021.
Mheshimiwa Spika, kiwango cha wastani wa ukuaji wa Pato la Taifa kwa kipindi cha mwaka 2022 kwa nchi nyingi za ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika ni asilimia 4.0 ikilinganishwa na wastani wa ukuaji wa asilimia 4.2 mwaka 2021. Aidha, wastani wa ukuaji wa uchumi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulikuwa ni asilimia 5.6 mwaka 2022 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5.7 mwaka 2021. Hali hii imesababishwa na kupungua kwa uzalishaji na shughuli za kiuchumi katika nchi husika kwa mwaka 2020 kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo: utekelezaji wa masharti yaliyowekwa kuzuia maambukizi ya UVIKO-19 kama kufunga mipaka, kusitisha safari za ndege za kimataifa, kusitisha baadhi ya shughuli za kiuchumi zinazohusisha mikusanyiko na kuzuia watu kutoka nje.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kusuasua kwa ukuaji wa uchumi wa dunia na mataifa ya Afrika hususan nchi za ukanda wa Jangwa la Sahara, Jumuiya za SADC na Afrika Mashariki, hali ya ukuaji wa uchumi kwa nchi yetu kwa kipindi cha robo ya kwanza hadi ya tatu ya mwaka 2022 imeimairika ikilinganishwa na mwaka 2021. Katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2022, uchumi wa taifa ulikua kwa wastani wa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 4.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2021. Ukuaji chanya wa uchumi ulichangiwa na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu, barabara, reli na viwanja vya ndege; kuongezeka kwa uzalishaji wa madini, hususan dhahabu na makaa ya mawe, kuongezeka kwa mikopo katika sekta binafsi ambayo imechochea shughuli za kiuchumi na kuongezeka kwa shughuli za utalii.
Mheshimiwa Spika, ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2022 unatarajiwa kupungua hadi kufikia wastani wa asilimia 4.7 kutoka ukuaji wa asilimia 4.9 mwaka 2021 na kuongezeka hadi kufikia asilimia 5.3 mwaka 2023. Maoteo ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania yamezingatia hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kukabiliana na athari zitokanazo na vita kati ya Ukraine na Urusi ikiwemo: kuchochea uzalishaji katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na madini; uimarishaji wa miundombinu ya barabara mijini na vijijini, nishati na maji; uboreshaji wa huduma za jamii; kuendelea na utekelezaji wa miradi inayochachua shughuli za kiuchumi ikiwemo reli, upanuzi wa bandari, usambazaji umeme vijijini; na uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji. Hata hivyo, kulingana na utabiri wa hali ya hewa ambao umebainisha uwezekano wa kuwa na mvua chini ya wastani, hali hiyo inaweza kuathiri uzalishaji katika sekta ya kilimo, upatikanaji wa nishati ya umeme, na maji na hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi.
Mfumuko wa Bei
Mheshimiwa Spika, madhara ya vita vya Urusi na Ukraine yamesababisha kuongezeka kwa kasi ya kupanda bei ya mafuta duniani na hivyo kuchangia kuongezeka kwa gharama za uzalishaji na usafirishaji na kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei nchini kwa mwaka 2022 ulifikia wastani wa asilimia 4.3 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.7 mwaka 2021. Hata hivyo, kiwango hiki kipo ndani ya malengo ya kati ya asilimia 3.0 hadi 5.0 na vigezo vya mtangamano wa kiuchumi wa kikanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika. Sababu zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei katika kipindi husika ni pamoja na: kupanda kwa bei za bidhaa ikiwemo mafuta ya kula, mbolea na petroli kufuatia kuvurugika kwa mnyororo wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma katika soko la dunia uliotokana na athari za vita kati ya nchi za Urusi na Ukraine; na kupungua kwa upatikanaji wa mazao ya chakula nchini na nchi jirani kulikosababishwa na mabadiliko ya tabianchi hususan maeneo yanayotegemea mvua za vuli.
Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei nchini unatarajiwa kuendelea kuwa tulivu na kubaki katika wigo wa tarakimu moja na ndani ya vigezo vya mtangamano wa kiuchumi vya kikanda kutokana na hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ikiwemo: kuongeza bajeti katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na nishati ili kuchochea uzalishaji wa ndani na kupunguza nakisi ya urari wa biashara; usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti; utulivu wa thamani ya shilingi na kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini.
UWEKEZAJI
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuimarisha uwekezaji hapa nchini. Katika mwaka 2022/2023, Serikali kupitia Bunge lako tukufu imetunga Sheria ya Uwekezaji Tanzania Namba 10 ya Mwaka 2022 ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuweka mazingira bora ya uwekezaji. Aidha, Serikali imeendelea kuratibu mradi wa maandalizi ya Kongani ya Viwanda ya Kwala yenye ukubwa wa ekari 2,500 ambapo kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni tatu zinatarajiwa kuwekezwa. Mradi huu unatarajiwa kuzalisha jumla ya ajira za moja kwa moja 100,000, ajira zisizo za moja kwa moja 300,000 na bidhaa za takriban Dola za Marekani bilioni 6 kwa mwaka. Vilevile, Serikali inaendelea kuratibu maandalizi ya kongani na maeneo mengine ya kiuchumi ikiwemo, Kongani ya Magu na Misungwi pamoja na Eneo Maalumu la Kiuchumi Nala.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza programu zinazolenga kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini. Programu hizi zinajumuisha kuboresha mazingira ya uondoshaji wa shehena bandarini ambapo Serikali inajenga Mfumo wa Pamoja wa Kielektroniki wa Uondoshwaji wa Shehena Bandarini. Aidha, Serikali imekamilisha mkakati wa uendeshaji wa mfumo huo na Mfumo wa Utoaji wa Vibali na Leseni za Mazao utakaounganishwa na Mfumo wa Pamoja wa Kielektroniki wa Uondoshwaji wa Shehena Bandarini kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa vibali na leseni za mazao.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika miradi na programu za maendeleo ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi. Aidha, Serikali itaendelea kufanya mapitio ya sera, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayohusu uwekezaji kwa lengo la kuweka mazingira bora ya uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kukuza ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati ya uwekezaji.
SIASA
Hali ya Siasa na Kuimarika kwa Demokrasia Nchini
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla hali ya siasa nchini ni tulivu na Vyama vya Siasa vinaendelea kutekeleza majukumu yao ikiwemo kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, Serikali imeendelea kuratibu vikao vya maridhiano ya kisiasa na Vyama vya Siasa nchini ili kuleta umoja, amani na utulivu katika nchi yetu ambao umekuwa ni utamaduni wetu tangu tupate uhuru. Kipekee naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kunakuwepo na mtangamano wa kisiasa nchini unaojumuisha siasa safi, za kiustaarabu na zinazoheshimu mawazo ya kila mmoja wetu.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kukuza na kuimarisha demokrasia ya vyama vingi nchini, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeratibu shughuli za Vyama vya Siasa kwa kuhakikisha kunakuwepo na fursa sawa katika shughuli za siasa nchini. Katika mwaka 2022/2023, Serikali imetoa ruzuku jumla ya shilingi bilioni 17.5 kwa vyama vya siasa sita vyenye sifa ya kupata ruzuku. Vyama hivyo ni NCCR-Mageuzi, CCM, CHADEMA, DP, CUF na ACT-Wazalendo. Hatua hii, imesaidia kuendeleza na kuimarisha uendeshaji wa shughuli za vyama vya siasa na demokrasia nchini.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, chaguzi ndogo za ubunge ziliendeshwa katika jimbo la Amani, Zanzibar na udiwani katika kata 12 Tanzania Bara. Chaguzi hizo zimefanyika kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo vifo na baadhi ya Waheshimiwa Madiwani kukosa sifa za kuendelea na nyadhifa hizo. Nitumie fursa hii kuvishukuru vyama vyote vilivyoshiriki chaguzi hizo kwani vimeonesha ukomavu mkubwa wa kisiasa. Kipekee nikipongeze Chama cha Mapinduzi kwa ushindi wa Jimbo la Amani pamoja na viti 12 vya udiwani katika chaguzi hizo.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, shughuli za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 pamoja na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka 2024 zitaendelea. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na kulifanyia maboresho Daftari la Kudumu la Wapiga Kura; kuboresha mifumo ya menejimenti ya uchaguzi; kuendelea na mchakato wa marekebisho ya sheria za uchaguzi; kuandaa kanuni za uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani; na kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi. Nitumie fursa hii kuwaomba viongozi wa vyama vya siasa kuhamasisha Wanachama na Watanzania wote wenye sifa kujiandikisha kwenye daftari hilo na kupata kitambulisho halali cha mpiga kura pale zoezi hilo litakapoanza rasmi.
BUNGE
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Ofisi ya Bunge imeendesha mikutano mitatu ya Bunge na mikutano mitatu ya Kamati za Kudumu za Bunge. Katika kipindi hicho, jumla ya maswali ya msingi 460 pamoja na ya nyongeza 1,426 yaliulizwa Bungeni na kujibiwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, Bunge pia lilijadili na kupitisha miswada saba na maazimio mawili ya Kimataifa yanayotokana na Kamati za Kudumu za Bunge na hatimaye kuwasilishwa Serikalini kwa utekelezaji. Vilevile, Kamati za Kudumu za Bunge zilifanya uchambuzi wa Miswada ya Sheria, Sheria ndogo, Taarifa za Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Taarifa za Utendaji wa Wizara na Taasisi za Serikali na ufuatiliaji wa utekelezaji wa afua za UKIMWI.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Ofisi ya Bunge itaendelea kusimamia shughuli za mikutano minne ya Bunge na mikutano minne ya Kamati za Kudumu za Bunge. Kuratibu ushiriki wa Wabunge katika mikutano ya kimataifa ikiwemo Bunge la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bunge la Umoja wa Afrika na Mabunge ya Jumuiya ya Madola. Aidha, Ukumbi wa Bunge utaendelea kuimarishwa pamoja na kukarabati jengo la kumbi za Bunge na majengo ya ofisi.
MAHAKAMA
Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali ya awamu ya sita kuhakikisha haki inapatikana kwa wananchi wote bila kujali hadhi ya mtu, uchumi wala kabila. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imeendelea kufanya maboresho mbalimbali ya kiutendaji pamoja na ujenzi wa miundombinu muhimu ya mahakama kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji wa mahakama na kuimarisha mifumo ya utoaji haki.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali imekamilisha miradi ya ujenzi wa Mahakama tatu za hakimu mkazi katika Mikoa ya Lindi, Songwe na Katavi. Aidha, ujenzi wa Mahakama za Wilaya 28 katika Wilaya za Same, Mwanga, Tandahimba, Nanyumbu, Namtumbo, Mvomero, Gairo, Ngara, Kilombero, Mkinga, Kakonko, Buhigwe, Uvinza, Butiama, Rorya, Itilima, Busega, Mbogwe, Nyanghwale, Kyerwa, Misenyi, Tanganyika, Kaliua, Manyoni, Bunda, Kilindi, Rungwe na Sikonge umekamilika. Vilevile, ujenzi wa mahakama ya mwanzo katika Wilaya ya Kilindi eneo la Kimbe na ukarabati wa Mahakama Kuu ya Tabora pamoja na Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi umekamilika.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa Mahakama nne za Wilaya za Ulanga, Ubungo, Liwale na Kwimba pamoja na Mahakama za Mwanzo saba za Kinesi, Mahenge, Luilo, Newala, Usevya, Nyakibimbili na Kabanga. Kwa upande mwingine, inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la makao makuu Jijini Dodoma, nyumba za majaji na ukarabati wa jengo la zamani la makao makuu Dodoma na jengo la mahakama Wilaya ya Maswa.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mifumo ya utoaji haki, Serikali imeongeza majaji wa mahakama ya rufaa kutoka 16 hadi 24 na wa mahakama kuu kutoka 78 hadi 98. Vilevile, idadi ya mahakimu iliongezeka kutoka mahakimu 245 hadi 293.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023 Mahakama imesikiliza na kukamilisha mashauri 134,989. Ufanisi huu umechangiwa na ongezeko la watendaji katika mahakama, kuendesha mashauri na mikutano kwa njia ya mtandao na kukamilika kwa miundombinu muhimu ya mahakama.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu kwa lengo la kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi ili huduma hizo zipatikane kwa wakati na gharama nafuu.
SEKTA ZA UZALISHAJI
Kilimo
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika sekta ya kilimo ili kuinua Pato la Taifa na la mtu mmoja mmoja. Aidha, hatua mbalimbali zenye lengo la kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara zimeendelea kuchukuliwa. Hatua hizo ni pamoja na: kuwezesha wakulima kupata mbegu bora zinazoendana na hali ya hewa nchini; kutoa ruzuku ya pembejeo hususan mbolea na mbegu; kuwezesha upatikanaji wa teknolojia mpya na zana za kisasa; kuimarisha huduma za ugani; kuongeza eneo la umwagiliaji kwa kuanzisha skimu mpya na kukarabati skimu za umwagiliaji zilizopo; na upatikanaji wa masoko ya mazao ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha wakulima wananufaika na mauzo ya mazao.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali imesaini mikataba 31 yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 284.14 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa skimu za umwagiliaji. Mikataba hiyo inahusu ujenzi wa mabwawa nane, skimu mpya 13 na ukarabati wa skimu za umwagiliaji 17. Ujenzi na ukarabati wa skimu hizo utaongeza eneo la umwagiliaji kwa hekta 50,930 na hivyo kufanya eneo la umwagiliaji kufikia hekta 778,210.6 kutoka hekta 727,280 mwaka 2021/2022.
Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za hali ya hewa, hali ya upatikanaji wa chakula cha kutosha katika maeneo yote nchini imeendelea kuimarika. Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023, uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa ulikuwa tani milioni 17.4 ikilinganishwa na mahitaji halisi ya tani milioni 15.1. Uzalishaji huo umeihakikishia nchi utoshelevu wa chakula kwa asilimia 115 kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2023/2024.
Mheshimiwa Spika, pamoja na uwepo wa ziada ya mazao ya chakula. Nitoe wito kwa Watanzania kuhifadhi mazao ya nafaka kwani utengamano wa hali ya chakula nchini umeendelea kuwepo kutokana na ziada inayotokana na mazao yasiyo ya nafaka.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha hali ya chakula inaendelea kuimarika. Hadi Januari, 2023, tani 29,084.21 za mahindi zilisambazwa katika Halmashauri 59 zilizopata changamoto ya upungufu wa chakula kwa mwaka 2022/2023. Mahindi hayo yaliuzwa kwa bei ya chini ya soko ili kuimarisha upatikanaji wa chakula katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua hizo, Serikali imeendelea kuratibu upatikanaji wa mbolea, mbegu bora na viuatilifu kwa wakati ili kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo. Hadi Februari, 2023 upatikanaji wa mbolea umefikia tani 407,333 sawa na asilimia 58.33 ya mahitaji ya tani 698,260. Upatikanaji huo umechangiwa na tani 28,672 zilizozalishwa ndani, tani 251,697 zilizoingizwa kutoka nje ya nchi na tani 126,963 ambazo ni bakaa ya msimu wa 2022/2023. Serikali inaendelea kuhakikisha mbolea iliyobaki inapatikana na kusambazwa kwa wakulima kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya kila mkoa na kupunguza makali ya bei.
Mheshimiwa Spika, Serikali katika kukabiliana na changamoto ya uzalishaji wa ndani wa mafuta kula, imetoa tani 591.1 za mbegu za alizeti kwa wakulima wa mikoa ya Singida, Dodoma, Kagera, Mbeya na Mwanza kwa utaratibu wa ruzuku. Hatua hiyo, itasaidia kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kuagiza kutoka nje ya nchi. Vilevile, imegawa lita 63,606 za viuatilifu katika mikoa 15 nchini ili kuthibiti viwavijeshi, nzi wa matunda na ndege waharibifu aina ya Quelea Quelea. Hatua hiyo imesaidia kuokoa ekari 159,015 za mazao mbalimbali yakiwemo mahindi na mpunga.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kasi ya kutoa huduma kwa wakulima inaongezeka, Serikali imeendelea kuimarisha huduma za ugani kwa kutoa mafunzo na vitendea kazi kwa maafisa ugani. Licha ya hayo, imeanzisha Kituo Cha Huduma kwa Wateja. Kituo hicho kimeshatoa huduma ya ushauri na taarifa za kilimo kwa wakulima na wadau wapatao 12,248. Aidha, kwa kupitia mfumo wa M-Kilimo, wakulima 7,269,101 na Maafisa Ugani 9,985 wamesajiliwa kwa ajili ya huduma za ushauri wa kitaalamu. Teknolojia hii itawawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kuyafikia masoko ya mazao kwa njia ya simu.
Kuimarisha Ushirika
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuimarisha ushirika nchini. Hatua hizo ni pamoja na kutoa mafunzo kwa watendaji, kuimarisha udhibiti na usimamizi wa vyama vya ushirika; kuhamasisha Wananchi kujiunga au kuanzisha vyama vya ushirika; kuimarisha upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi; kukuza matumizi ya TEHAMA na kufanya kaguzi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hatua hizo, mauzo kuipitia Vyama vya ushirika yameongezeka ambapo hadi Januari 2023, zimeuzwa jumla ya tani milioni 1.83 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.7 ikilinganishwa na tani 597,298 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.5 mwaka 2021/2022 kutoka kwenye mazao ya tumbaku, korosho, pamba, kahawa, ufuta, kakao, mkonge, chai, mbaazi, soya, zabibu, miwa na maharage.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa uwezeshaji, Benki ya Maendeleo ya Kilimo imefanikiwa kutoa mikopo ya moja kwa moja yenye thamani ya shilingi bilioni 78.54 kwa wakulima 119,797 wanaojishughulisha na kilimo, mifugo na uvuvi. Aidha, kupitia Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo imetoa dhamana ya mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 12.95 na kunufaisha wananchi 961 katika mikoa 20 katika shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kuongeza uzalishaji na tija; kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji, na upatikanaji wa pembejeo. Vilevile, itaendelea kuimarisha huduma za ugani na upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo na kuwajengea uwezo wakulima wadogo.
Mifugo
Mheshimiwa Spika, kuimarika kwa huduma za ugani ikiwemo utoaji elimu kwa umma kuhusu ufugaji bora wa ngombe wa maziwa wa kibiashara umesababisha kuongezeka kwa uzalishaji wa maziwa kufikia lita bilioni 3.62 katika mwaka 2022/2023 ikilinganishwa na lita bilioni 3.4 mwaka 2021/2022. Aidha, uzalishaji wa zao la nyama umeongezeka kwa asilimia 4.3 kutoka tani 769,966.66 mwaka 2021/2022 hadi tani 803,264.32 mwaka 2022/2023. Vilevile, jumla ya vipande milioni 14.19 vya ngozi vyenye thamani ya shilingi bilioni 31.11 vilizalishwa ikilinganishwa na vipande milioni 13.56 vyenye thamani ya shilingi bilioni 28.5 vilivyozalishwa mwaka 2021/2022.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali imenunua pikipiki 1,200 na magari 13 ili kurahisisha utoaji wa huduma za ugani katika ngazi ya Kata na Vijiji. Vilevile, Serikali imewezesha mafunzo rejea kwa Maafisa Ugani 487 na wataalam wawakilishi 28 kutoka sekta binafsi katika kanda nane. Mafunzo hayo yalihusu Mpango wa Mabadiliko wa Sekta ya Mifugo, Ufugaji bora na wa Kibiashara, Fursa za Uwekezaji katika sekta ya mifugo, matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za ugani, uboreshaji wa kosaafu za mifugo, udhibiti wa magonjwa ya mifugo, uendelezaji wa malisho na upatikanaji wa maji.
Mheshimiwa Spika, vifo vya mifugo vinavyotokana na magonjwa yanayoenezwa na kupe vimepungua kwa takriban asilimia 60. Mafanikio hayo yametokana na hatua ya Serikali kuimarisha huduma za mifugo pamoja na ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo majosho ya kuogesha mifugo.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya mifugo kwa kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za mifugo, malisho, maji na vyakula vya mifugo. Hali kadhalika, Serikali itaboresha huduma za utafiti na mafunzo ya taaluma za mifugo pamoja na kuanzisha na kuendeleza vituo atamizi vya uwekezaji vya vijana.
Uvuvi
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuinua kipato cha wananchi wake, kuimarisha upatikaji wa samaki na uendelevu kupitia ukuzaji wa viumbe maji. Katika mwaka 2022/2023, tani 28,856.87 za samaki zilivuliwa kutoka katika ukuzaji viumbe maji ikiwemo ufugaji kwenye mabwawa na vizimba. Kiasi hicho cha samaki kiliwezesha mauzo ya nje ya nchi yenye thamani ya shilingi bilioni 238.49. Vilevile, tani za mwani 4,134.6 zenye thamani ya shilingi bilioni 4.34 zilizalishwa na kuuzwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali imeendelea kuboresha hali ya masoko ya samaki nchini kupitia ujenzi wa masoko mbalimbali ya samaki. Masoko yaliyoboreshwa ni pamoja na Zingibari (Halmashauri ya Mkinga), Kipumbwi (Pangani), Ngombo (Nyasa), Manda (Ludewa), Maporomoko (Tunduma), Kyamkwikwi (Muleba), Nyamikoma (Busega) pamoja na mialo ya kupokelea samaki katika Halmashauri za Momba (Masuche), Nkasi (Karungu) na Chato (Chato beach).
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora za mifugo, malisho, vyakula vya mifugo na maji. Vilevile, itatoa kipaumbele katika kuimarisha afya ya mifugo, kuboresha huduma za ugani, kuanzisha na kuendeleza vituo atamizi vya uwekezaji vya vijana, kuimarisha huduma za utafiti na mafunzo ya taaluma za mifugo.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali itaendelea kuimarisha Shirika la Uvuvi Tanzania, usimamizi na udhibiti wa ubora, usalama na viwango vya samaki na mazao ya uvuvi pamoja na kuimarisha huduma za utafiti, mafunzo na ugani. Aidha, Serikali itaimarisha miundombinu ya masoko ya samaki, vituo vya kuendeleza ukuzaji wa viumbe maji na kuanza ujenzi wa meli za uvuvi katika bahari kuu.
MALIASILI NA UTALII
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha sekta za maliasili na utalii kupitia utekelezaji wa programu mbalimbali ili kukuza utalii, kuitangaza nchi yetu na vivutio vyake kitaifa na kimataifa pamoja na kuimarisha mchango wa sekta hizo kwenye pato la Taifa. Katika mwaka 2022/2023, programu mbalimbali zimeendelea kutekelezwa ikiwemo Programu ya Tanzania - The Royal Tour na utangazaji wa vivutio vya utalii kupitia matukio mbalimbali na vyombo vya habari ikiwemo Tanzania Safari Channel.
Mheshimiwa Spika, kutokana na jitihada hizo, idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kutoka watalii 922,692 katika mwaka 2021 hadi kufikia watalii takriban milioni 1.4 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 57.7. Vilevile, idadi ya watalii wa ndani imeongezeka kutoka watalii 788,933 mwaka 2021 hadi watalii milioni 2.4 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 199.5. Aidha, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeendelea kuwa hifadhi bora duniani ambapo kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi 2022 imepata tuzo ya dhahabu ya utoaji wa huduma bora iliyotolewa na European Society for Quality Research.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, kumekuwa na changamoto ya ongezeko la watu, mifugo, makazi holela na shughuli za kibinadamu hivyo kukosekana kwa uwiano baina ya uhifadhi, ukuzaji wa utalii na maendeleo ya jamii. Hali hiyo imekuwa ikitishia uendelevu wa hifadhi na ustawi wa maisha ya watu wanaoishi katika hifadhi hiyo kutokana na sheria za uhifadhi kutoruhusu shughuli nyingi za kiuchumi na kimaendeleo katika eneo hilo. Ili kutatua changamoto hiyo, Serikali iliendesha zoezi la hiari la kuondoa makazi na shughuli za kibinadamu ndani ya Hifadhi kwa kuhamisha wenyeji waliokuwa tayari kuhama kwenda kwenye maeneo yaliyotengwa katika Kijiji cha Msomera katika Halmashauri za Wilaya za Handeni na Kilindi mkoani Tanga.
Mheshimiwa Spika, zoezi hilo limefanyika kwa umakini mkubwa na kwa kuzingatia haki za wanaohama. Hadi kufikia Januari, 2023 jumla ya kaya 1,524 zenye watu 8,715 na mifugo 32,842 zilikuwa zimejiandikisha kwa ajili ya kuhama kwa hiari kwenda Kijiji cha Msomera. Kati ya kaya hizo, kaya 551 zenye watu 3,010 na mifugo 15,521 tayari zimehamishwa kwa hiari kwenda Msomera.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024 Serikali itaendelea kuibua na kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati ikiwemo utalii wa fukwe, mikutano na matukio, meli, michezo na utamaduni. Vievile, itaendelea kuimarisha miundombinu katika maeneo ya hifadhi, kukarabati majenzi ya kale na kuyatangaza kidijitali pamoja na kutekeleza mikakati ya kuongeza thamani ya mazao ya misitu.
MADINI
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuipa kipaumbele sekta ya madini ili kuhakikisha inanufaisha wananchi na kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa. Katika mwaka 2022/2023, Serikali ilianzisha vituo 26 vya ununuzi wa madini na kutoa jumla ya leseni tano za uchenjuaji wa madini. Aidha, jumla ya shilingi bilioni 409.66 sawa na asilimia 85.43 ya lengo la shilingi bilioni 479.51 zilikusanywa kutokana na mrabaha, ada ya ukaguzi, mauzo ya madini kwenye masoko na vituo na ada ya leseni za uchimbaji.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kuhamasisha biashara na uwekezaji katika sekta ya madini; kuwaendeleza wachimbaji wadogo; kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini; kusimamia mifumo ya ukaguzi wa shughuli za migodi; na kuzijengea uwezo taasisi zinazosimamia sekta hiyo.
NISHATI
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza azma yake ya kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kuhakikisha wananchi wake wanapata nishati ya umeme, mafuta na gesi kwa uhakika na bei nafuu.
Umeme
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili. Hadi Machi, 2023 asilimia 76.7 ya Vijiji vya Tanzania Bara vimeunganishwa na huduma ya umeme. Utekelezaji wa miradi hiyo ikiwa ni pamoja na mkakati wa kuboresha upatikanaji wa nishati bora na safi ya kupikia kwa wananchi wanaoishi vijijini inaendelea vizuri na ipo katika hatua mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali imekamilisha ufungaji wa mitambo mitatu yenye uwezo wa kuzalisha megawati 135 katika mradi wa Kinyerezi I Extension. Kufungwa kwa mitambo hiyo kumeongeza uwezo wa mitambo kufua umeme katika gridi ya Taifa kwa asilimia 7.52. Aidha, uboreshaji wa mtandao wa miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme nchini umesaidia kuboresha maisha ya watu kwa kutoa fursa za kiuchumi na kijamii.
Mafuta na Gesi
Mheshimiwa Spika, katika kutimiza azma ya kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi kupikia ifikapo mwaka 2033, kimeundwa kikosi kazi cha Taifa kuchakata na kutoa suluhu ya afua ya nishati safi ya kupikia ambacho nakisimamia mimi mwenyewe. Hii ni kufuatia maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia. Kazi zinazoendelea ni pamoja na kuandaa rasimu ya Dira ya Taifa ya miaka 10 ya kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na Rasimu ya Mpango Mkakati.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa gesi, Serikali inaendelea kufanya tafiti katika vitalu vya mafuta na gesi asilia katika vitalu vya kimkakati ikiwa ni pamoja na kuimarisha Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia na Mkakati wa matumizi ya nishati jadidifu na tungamotaka.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kukamilisha utekelezaji wa miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa nishati ya umeme, mafuta na gesi. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu na kusambaza umeme katika vitongoji 36,336 vya Tanzania Bara.
ARDHI
Mheshimiwa Spika, sekta ya ardhi imeendelea kuwa kiungo wezeshi kwa shughuli za sekta nyingine za uzalishaji ikiwemo viwanda, kilimo, mifugo, maliasili, utalii, madini na miundombinu. Katika, mwaka 2022/2023, Serikali imeandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 110 katika Halmashauri za Wilaya 16 na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya tatu za Kigoma, Nsimbo na Ngorongoro. Idadi hii inafanya kuwa na jumla ya vijiji 2,673 vyenye Mipango ya Matumizi ya Ardhi.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kuwezesha na kuandaa Mipango ya Matumizi ya ardhi ya Vijiji, Wilaya na Kanda; utatuzi wa migogoro ya ardhi; kuboresha Mfumo wa Taarifa za Matumizi ya Ardhi nchini; na kupanga, kurasimisha na kumilikisha ardhi kwa wananchi.
USAFIRI NA USAFIRISHAJI
Mheshimiwa Spika, miundombinu ya usafiri na usafirishaji ni msingi wa uchumi wa Taifa na inatoa huduma muhimu kwa wananchi wetu. Usimamizi thabiti wa miundombinu hiyo unaipa fursa Serikali kuongeza thamani ya huduma na rasilimali fedha zinazoonekana moja kwa moja kwa manufaa ya jamii.
Barabara na Madaraja
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali imejenga jumla ya kilomita 317.65 za barabara kwa kiwango cha lami ambazo zimehusisha barabara kuu, barabara za mikoa na wilaya. Ujenzi huo umesaidia kurahisisha utoaji wa huduma ya usafiri na usafirishaji katika maeneo tofauti nchini na umezingatia uendelevu kwa watumiaji wa sasa na wa baadaye.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kupunguza msongamano wa magari katika majiji na miji ili kuongeza ufanisi katika utendaji na utekelezaji wa majukumu ya wananchi na ukuaji wa uchumi wa Taifa. Katika hatua za kuhakikisha kuwa huduma za uchukuzi zinaboreshwa, Serikali inaendelea na Awamu ya Pili, Tatu, Nne na Tano ya ujenzi wa barabara na Miundombinu ya Mabasi yaendayo Haraka Mkoani Dar es Salaam na ujenzi wa barabara za mchepuo (bypass) katika Mkoa wa Dodoma na Wilaya ya Maswa.
Mheshimiwa Spika, Awamu ya Pili (BRT II) ya ujenzi huo inayohusisha barabara ya Kilwa kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam kuelekea Mbagala na barabara ya Kawawa kutoka makutano ya Magomeni kupitia Changombe hadi makutano ya barabara ya Kilwa umefikia asilimia 82. Mradi huu una barabara zenye urefu wa kilomita 20.3; vituo vya mabasi 29; barabara za juu mbili; majengo mawili ya Terminal; Depot moja na Feeder station nne.
Aidha, Awamu ya Tatu (BRT III) inayohusisha Barabara ya Nyerere kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Gongolamboto yenye urefu wa kilomita 23.6 imekamilika kwa asilimia 5.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Jiji la Dodoma, ujenzi wa barabara ya mchepuko ya Dodoma umelenga kupunguza foleni ya magari katikati ya Jiji kutokana na magari yanayosafiri katika ushoroba wa kati na ushoroba wa Barabara Kuu ya Trans-Africa 4 inayoanzia Cape Town, Afrika Kusini hadi Cairo, Misri. Mradi huu wenye barabara yenye urefu wa jumla ya kilomita 112.3 umefikia kwa asilimia 17 katika sehemu ya kwanza na sehemu ya pili imefikia asilimia 22. Aidha, ujenzi wa barabara ya mchepuo Maswa (Maswa Bypass) yenye urefu wa kilomita 11.3 kwa kiwango cha lami umefikia asilimia 72.
Vivuko
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kujenga vivuko vipya na kukarabati vivuko vilivyochakaa nchini ili kuwaondolea kero ya usafiri wananchi wanaotegemea vivuko ili kuharakisha na kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Katika mwaka 2022/23, Serikali imeendelea na ujenzi wa vivuko vipya vya Kisorya Rugezi, Ijinga Kahangala, Bwiro Bukondo na Nyakarilo Kome. Vilevile, ujenzi wa vivuko vya Buyagu Mbalika na Magogoni Kigamboni upo kwenye hatua za ununuzi. Aidha, ukarabati wa vivuko vya MV Musoma, MV Kazi, MV TEMESA na MV Tanga umekamilika kwa asilimia 100 na ukarabati wa vivuko vya MV Misungwi, MV Nyerere, MV Kilombero, MV Mara, MV Ujenzi, MV Kitunda, MV Ruhuhu, MV Old Ruvuvu na MV Magogoni unaendelea.
Viwanja vya Ndege na Usafiri wa Anga
Mheshimiwa Spika, usafiri wa anga ni kiungo muhimu katika kuchangia ukuaji wa pato la mtu binafsi na Taifa kwa ujumla. Usafiri huu umeendelea kutengeneza fursa za ajira zilizo rasmi na zisizokuwa rasmi, kuimarisha upatikanaji wa huduma za usafiri wa uhakika, na hivyo kutoa mchango muhimu katika maendeleo ya kiuchumi. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika uimarishaji na uboreshaji wa huduma za usafiri wa anga nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka 2022/2023 imeendelea na awamu ya kwanza ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato. Kukamilika kwa ujenzi wa kiwanja hiki kutarahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa kutoka na kuingia katika Jiji la Dodoma, kati ya Tanzania na nchi mbalimbali; kukuza utalii na uchumi na kuongeza fursa za ajira. Aidha, ujenzi huo utakapokamilika pamoja na kuimarisha usafiri anga kwa kuruhusu ndege kubwa na za kimataifa kutua, utasaidia kufanya Jiji la Dodoma kuwa jiji la kisasa na kimataifa.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha usafiri wa anga, mashirika ya ndege ya KLM, Eurowing, Edelweiss Airline na Saudia Airline yameanza kutoa huduma za usafiri wa anga kuanzia Tanzania. Hatua hizi zitaendelea kuimarisha sekta ya utalii na hivyo kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye mapato na ukuaji wa uchumi.
Reli
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali imefanya ununuzi wa vifaa vya uendeshaji wa Reli ya SGR ambapo utengenezaji wa mabehewa 59 ya abiria umefikia asilimia 92. Kati ya mabehewa hayo, 14 yaliwasili nchini Novemba, 2022 na 45 yaliyobaki yanatarajiwa kuwasili Mei, 2023. Aidha, utengenezaji wa vichwa vya treni 17 vya umeme na seti 10 za treni (Electric Multiple Unit - EMU) kwa ajili ya treni ya abiria umefikia asilimia 31.6 na seti moja ya treni hizo inatarajiwa kuwasili Juni, 2023. Aidha, utengenezaji wa mabehewa 1,430 ya mizigo umefikia asilimia 35. Upatikanaji wa vifaa hivyo utaboresha na kuongeza kiwango cha ubebaji mizigo na kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji, na hivyo kupunguza gharama za maisha.
Mheshimiwa Spika Aidha, katika mwaka 2022/2023, pamoja na uendelezaji wa ujenzi wa Reli ya SGR, Serikali imeendelea na ukarabati wa njia ya Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma. Mkataba wa ukarabati wa njia ya reli ya Kaliua-Mpanda ulisainiwa Novemba, 2022.
Usafiri katika Maziwa Makuu
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji katika maziwa makuu, Februari, 2023, meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu iliyo katika Ziwa Victoria ilishushwa majini kwa ajili ya ukamilishaji. Meli hiyo inatarajiwa kuanza kutoa huduma katika mwaka 2023/2024. Aidha, ukarabati wa meli ya MV Umoja katika Ziwa Victoria na MT Sangara katika Ziwa Tanganyika unaendelea. Kukamilika kwa meli hizo kutaboresha huduma za usafiri wa abiria na mizigo kwa njia ya meli; kufungua masoko mapya ndani na nje ya nchi; kurahisisha shughuli za kibiashara, uzalishaji wa mazao, uvuvi, madini; na kuchochea utalii katika maeneo ya maziwa makuu.
Bandari
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza Mradi wa Bandari Kavu ya Kwala ambapo ujenzi wa barabara ya zege yenye urefu wa kilomita 15.5 kutoka Vigwaza umefikia asilimia 98 na ujenzi wa bandari umefikia asilimia 87. Kukamilika kwa bandari hiyo na kuanza kutumika kutapunguza msongamano wa mizigo na magari katika bandari ya Dar es Salaam, kuongezea nafasi ya kuhifadhi mizigo na kupunguza muda wa magari kusafirisha mizigo. Hali hiyo itaiwezesha bandari ya Dar es Salaam kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na hivyo kuongeza mapato kwa bandari na wafanyabiashara.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, sekta ya usafiri na usafirishaji itaendelea kukamilisha ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa huduma za usafiri kwa njia reli, anga, barabara na majini. Aidha, Serikali imeamua kwa dhati kuanza ujenzi wa bandari ya Bagamoyo kwa kuhamisha wananchi waliolipwa fidia, wanaotakiwa kupisha ujenzi wa bandari na kuanza maandalizi ya ujenzi wa miundombinu wezeshi kwa ajili ya bandari ya Bagamoyo ikiwemo barabara, reli na umeme.
MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na teknolojia ya habari nchini kwa lengo la kuongeza chachu ya maendeleo ya jamii, siasa, usalama na uchumi kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia ulimwenguni.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali imeendelea kutekeleza Mfumo wa Anwani za Makazi kwa kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyatoa tarehe 08 Februari 2022 wakati wa uzinduzi wa Operesheni Anwani za Makazi. Utekelezaji wa Mfumo huo umefanyika nchi nzima ambapo hadi Februari, 2023 jumla ya taarifa milioni 12.66 za Anwani za Makazi zikijumuisha majengo na viwanja zimekusanywa. Utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi umewezesha utambuzi wa mtu, kitu au jengo lilipo na hivyo kuimarisha usalama na kurahisisha utoaji wa huduma na ufikishaji wa bidhaa mahali stahiki. Aidha, Serikali inaendelea na uhakiki wa taarifa za anwani za makazi zilizokusanywa ili kuboresha taarifa hizo.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imekamilisha ujenzi wa minara 1,201 katika kata 1,087 zenye vijiji 3,378. Kwa upande wa Zanzibar ujenzi wa minara 42 umekamilika na kufanya eneo lote la Zanzibar kuwa na mawasiliano ya simu. Aidha, Serikali imesaini mikataba ya ujenzi wa minara katika kata 1,242 zenye vijiji 3,654 Tanzania Bara. Kukamilika kwa miradi hiyo kutafanya Taifa kuongeza usikivu katika mawasiliano ya njia ya simu na usafirishaji wa taarifa kwa kasi na kiwango kinachokusudiwa. Nitoe wito kwa Watanzania wote kuendelea kuchangamkia fursa zinazotokana na matumizi ya teknolojia ya mawasiliano katika kujenga uchumi wa kidijitali.
Uchumi wa Kidijitali
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kuwa fursa za kidijitali na uchumi zimekuwa zikiongezeka ulimwenguni. Fursa hizo zimewezesha ushiriki wa watu wengi na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kimtandao. Vilevile, maendeleo ya kidijitali yamerahisisha mawasiliano ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa kupunguza gharama, kuokoa rasilimali muda na upatikanaji wa taarifa na fursa mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu huo, Serikali katika mwaka 2023/2024 itaendelea na maandalizi ya Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali ili kuhakikisha nchi yetu haibaki nyuma katika ulimwengu wa kidijitali na kuwa wananchi wananufaika na fursa zitokanazo na uchumi huo. Kwa upande mwingine, Serikali itaendelea kujenga misingi ya matumizi ya TEHAMA ikiwa ni pamoja na kuendeleza na kuboresha Mfumo wa Kidijitali wa Mfumo wa Anwani za Makazi.
HUDUMA ZA JAMII
Elimu
Mheshimiwa Spika, tangu awali, Serikali ya awamu ya sita imejipambanua katika kuinua viwango vya elimu kwa kuweka mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia. Hii ni pamoja na kuhakikisha kila mtoto wa Tanzania anapata fursa ya kusoma na kumaliza mzunguko wa elimu kama inavyotakiwa. Ili kutekeleza azma hiyo, Serikali imeendelea kujenga, kukarabati na kukamilisha miundombinu ya kutolea elimu katika ngazi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali imeendelea na ujenzi wa shule mpya 231 za sekondari, upanuzi wa shule kongwe 18 za sekondari, ujenzi wa shule mpya sita za Msingi, ujenzi wa vyumba vya madarasa 1,072 katika shule kongwe za msingi, na ujenzi wa nyumba za walimu 809 ambapo kati ya nyumba hizo, 298 ni za walimu wa shule za msingi na 511 za walimu shule za sekondari. Aidha, imeendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa shule za wasichana za bweni kidato cha tano na sita katika mikoa yote Tanzania bara ambapo ujenzi wa shule 10 kati ya 26 umekamilika.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea pia kutoa mikopo na kuongeza wigo wa upatikaji wa mikopo ya elimu ya juu sambamba na kuboresha miundombinu ya vyuo vya elimu ya juu nchini. Katika mwaka 2022/2023, kiasi cha shilingi bilioni 654 zilitengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ikilinganishwa na shilingi bilioni 570 zilizotengwa mwaka 2021/2022. Aidha, idadi ya wanufaika imeongezeka kutoka 177,605 mwaka 2021/2022 hadi 202,877 mwaka 2022/2023.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeongeza kiwango cha posho ya kujikimu ya wanafunzi wa elimu ya juu kutoka shilingi 8,500 hadi shilingi 10,000 kwa siku. Mafanikio haya ni kielelezo tosha cha umakini, uzalendo, maono na mapenzi makubwa ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha ustawi wa maisha ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu. Kwa upande mwingine, kupitia Samia Scholarship, Serikali imetoa ufadhili kwa wanafunzi 244 wa kike wenye ufaulu wa juu ili kusoma katika vyuo vikuu mbalimbali katika fani za utabibu, uhandisi, sayansi, teknolojia na hisabati. Ama kwa hakika Mama anajali!
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kuhuisha Mitaala ya Elimu na kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi na elimu ya juu.
Maji
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji ikiwa ni pamoja na kuhifadhi na kulinda vyanzo vya maji, kujenga mabwawa makubwa, ya kati na madogo katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuongeza uwezo wa nchi kuhifadhi maji na kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya mijini na vijijini.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza dhamira yake ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji mijini na vijijini inafikia asilimia 95 na 85 mtawalia mwaka 2025. Hadi kufikia Februari, 2023, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji mijini imeongezeka kutoka asilimia 86 mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 88 na vijijini imeongezeka kutoka asilimia 72.3 mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 77.
Mheshimiwa Spika, ongezeko la hali ya upatikanaji wa huduma ya maji mijini na vijijini limetokana na kukamilika kwa miradi 36 ya maji mijini na miradi 382 ya maji vijijini inayonufaisha wananchi zaidi ya milioni mbili. Aidha, miradi mingine 139 mijini na 647 vijijini ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji vijijini na mijini ikiwemo miradi ya miji 28; ujenzi wa bwawa la Kidunda; kuanza ujenzi wa Bwawa la Farkwa; kujenga mabwawa ya ukubwa wa kati; kuanza ujenzi wa miradi ya uondoshaji wa majitaka; na kuimarisha usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za maji ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Afya
Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali ya awamu ya sita kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora za afya. Kwa msingi huo, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika sekta ya afya kwa kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha utoaji wa huduma hizo. Mikakati hiyo ni pamoja na ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Mheshimiwa Spika, Serikali katika kutekeleza azma yake kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, imekamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mtwara; na Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Mara, Songwe, Shinyanga, Geita na Katavi. Aidha, imekamilisha ujenzi wa hospitali 59 za halmashauri, ukarabati wa hospitali kongwe 19 za halmashauri na ujenzi wa maboma ya zahanati 300. Tayari vituo hivyo vimeanza kutoa huduma.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha utoaji wa huduma za afya za dharura, Serikali imejenga majengo ya huduma za dharura katika hospitali za kanda na kufikisha hospitali 36 zenye huduma hiyo kutoka hospitali saba mwaka 2020. Mafanikio haya yamepatikana kutokana na jitihada za makusudi za Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani kwa mara ya kwanza tangu uhuru, nchi yetu imeweka historia ya kuwa na mfumo wa huduma za dharura kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Taifa. Awali huduma hizo zilikuwa zinapatikana katika ngazi ya Kanda na Taifa pekee. Uwepo wa huduma za dharura katika hospitali zetu utapunguza vifo kwa asilimia 40.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa, ujenzi wa miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya hauwezi kuwa na tija pasipokuwa na watumishi wenye weledi, vifaa, vifaatiba na vitendanishi. Kutokana na ukweli huo, hadi kufikia Februari, 2023, Serikali imesambaza vifaa vyenye thamani ya shilingi bilioni 44.3 pamoja na kuajiri watumishi wa kutoa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya. Aidha, kupitia Programu ya Mfuko wa Pamoja wa Afya, jumla ya shilingi bilioni 48.35 zimetolewa kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za afya.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za afya, kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, kuimarisha utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, kuimarisha huduma za afya ya uzazi na kudhibiti magonjwa ya mlipuko. Vilevile, itaendelea kutoa mafunzo kwa wataalam wa sekta ya afya katika ngazi za ubingwa na ubingwa bobezi.
HUDUMA KWA MAKUNDI MAALUM
Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ambapo mwaka 2022/2023 ilitenga jumla ya shilingi bilioni 3.46 kwa ajili ya kukamilisha ukarabati wa vyuo vya Watu Wenye Ulemavu vya Mtapika (Masasi Mtwara), Luanzari (Tabora), Sabasaba (Singida) na Yombo (Dar es Salaam). Ukarabati huu umewezesha Chuo cha Luanzari kuanza kutoa mafunzo kwa kudahili wanafunzi 400 baada kufungwa kwa zaidi ya miaka 10.
Mheshimiwa Spika, ili kuongeza ufanisi wa upatikanaji, utunzaji, uchakataji na utumiaji wa taarifa za watu wenye ulemavu, Serikali imetengeneza Mfumo wa Kielektroniki wa Watu Wenye Ulemavu. Mfumo huo utawezesha kumsajili na kumtambua mtu mmoja mmoja mwenye ulemavu, mahali alipo, shughuli anayoifanya na mahitaji yake. Vilevile, utawawezesha kuunganishwa na huduma mbalimbali zikiwemo kupata cheti za kuzaliwa, matibabu, kuandikishwa shule ya awali na msingi, mikopo ya asilimia mbili inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri na vifaa saidizi.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali imeandaa Mwongozo wa Utekelezaji, Ujumuishwaji na Uimarishaji wa Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu wa Mwaka 2022. Mwongozo huo utasaidia kuhakikisha masuala ya usawa, haki, fursa na huduma kwa watu wenye ulemavu yanaimarishwa katika nyanja zote za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka 2023/2024 imepanga kuwawezesha watu wenye ulemavu kujiajiri na kuajiriwa kwa kuongeza fursa za mafunzo ya ufundi stadi na marekebisho kutoka watu 460 hadi 1,400.
Huduma kwa Wazee
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwatambua na kutoa huduma za msingi za chakula, malazi, mavazi na matibabu kwa wazee wasiojiweza. Hadi sasa tunao wazee 268 wanaoishi katika makazi 14 ya wazee ya Kibirizi, Njoro, Kolandoto, Bukumbi, Ipuli, Fungafunga, Mwanzange, Misufini, Nunge, Nyabange, Kilima, Sukamahela, Magugu pamoja na Nandanga. Ninatoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi kwa ujumla tuendelee kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwahudumia wazee na hii ni namna bora ya kutambua umuhimu na michango waliyotoa katika ujenzi wa Taifa hili.
ULINZI NA USALAMA
Mheshimiwa Spika, hali ya ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi yetu imeendelea kuwa shwari bila uwepo wa matukio hatarishi. Katika kuhakikisha hali ya usalama nchini inaendelea kuimarishwa, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeendelea kulinda mipaka ya nchi; kudumisha amani, usalama wa raia, mali zao na kufundisha wananchi ulinzi wa umma.
Mheshimiwa Spika, Jeshi letu limeendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika katika operesheni mbalimbali za ulinzi wa amani. Katika mwaka 2022/2023, vikosi vyetu vilipeleka waangalizi wa kijeshi, wanadhimu na makamanda kwenye nchi zenye migogoro za Lebanon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Msumbiji. Ushiriki huo ni muhimu kwa kuwa unalitambulisha Taifa kimataifa, kuwaweka askari wetu tayari kila wakati, kujifunza teknolojia mpya na kushirikisha vijana katika kuleta amani.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutambua, kusajili na kutoa vitambulisho vya Taifa ili kuwezesha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kiusalama. Aidha, hivi karibuni Serikali imefanya marekebisho ya Kanuni za Usajili na Utambuzi wa Watu za Mwaka 2023 ili kuwawezesha Watanzania kuendelea kutumia Vitambulisho vya Taifa bila kuwa na ukomo wa matumizi. Hatua hii inapunguza usumbufu na gharama kwa wananchi na Serikali.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kutoa wito kwa watoa huduma wote zikiwemo Ofisi za Balozi mbalimbali hapa nchini waendelee kutambua na kutoa huduma stahiki kwa wananchi wenye vitambulisho vya Taifa bila kujali tarehe za ukomo zilizo kwenye vitambulisho hivyo.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024 Serikali itaendelea kuviimarisha na kuviongezea uwezo vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuvipatia vifaa na zana bora za kisasa. Vilevile, Jeshi litaendelea kuwajengea vijana wa Kitanzania ukakamavu, uzalendo na uwezo wa kujitegemea.
MASUALA YA KAZI NA WAFANYAKAZI
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kazi na wafanyakazi kwa kusimamia viwango vya kazi pamoja na masuala ya afya na usalama mahali pa kazi. Katika mwaka 2022/2023, jumla ya kaguzi 3,327 za viwango vya kazi zilifanyika sawa na asilimia 69.31 ya kaguzi 4,800 zilizopangwa kufanyika. Vilevile, kaguzi 96,693 zinazohusu afya na usalama mahali pa kazi zilifanyika ambapo kumekuwa na ongezeko la upimaji wa afya kutoka wafanyakazi 125,616 mwaka 2021/2022 hadi wafanyakazi 169,735 mwaka 2022/2023. Kufuatia kaguzi hizo, waajiri 173 waliokiuka sheria za kazi walichukuliwa hatua.
Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, Serikali imeimarisha Mfumo wa Kielektroniki wa Kushughulikia Maombi ya Vibali vya Kazi. Uimarishaji wa mfumo huo, pamoja na mambo mengine umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa vibali vya kazi nchini. Mathalani, hadi kufikia Februari, 2023 jumla ya vibali vya kazi 8,576 vilitolewa sawa na asilimia 92.14 ya maombi ya vibali 9,307 yaliyopokelewa.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa sheria za kazi, uratibu wa ajira za wageni na masuala yote yanayohusu usalama na afya mahali pa kazi. Aidha, Serikali itaendelea, kutoa elimu na ushauri kwa wafanyakazi, waajiri na vyama vyao ili kuwa na rasilimali watu imara na yenye tija kwa maendeleo endelevu ya Taifa letu.
HIFADHI YA JAMII
Mheshimiwa Spika, sekta ya hifadhi ya jamii imekuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi pamoja na ustawi kwa wananchi. Aidha, hadi Februari, 2023 deni la shilingi trilioni 2.17 limelipwa katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa umma (PSSSF). Fedha hizo ni stahili ya mafao kwa wanachama waliorithiwa kutoka uliokuwa Mfuko wa PSPF Mwaka 1999.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Mfuko wa PSSSF umelipa mafao kwa wastaafu, wategemezi na wanufaika wengine wapatao 41,939 yenye thamani ya shilingi trilioni 1.074 na pensheni ya kila mwezi ya shilingi bilioni 507.28 sawa na wastani wa shilingi bilioni 63.41 kila mwezi kwa wastaafu 158,351. Aidha, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umelipa mafao ya shilingi bilioni 438.32 kwa wastaafu, wategemezi na wanufaika wengine wapatao 66,628. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 72.3 zililipwa kama pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu 27,570 ikiwa ni wastani wa shilingi bilioni 9.04 kwa kila mwezi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mapenzi makubwa aliyonayo kwa wananchi wake, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alielekeza kurejesha michango ya watumishi walioondolewa kazini kwa kughushi vyeti. Utekelezaji wa maelekezo hayo umeanza ambapo hadi sasa jumla ya watumishi 11,896 wamerejeshewa michango yao yenye thamani ya shilingi bilioni 35.02 kupitia PSSSF na NSSF. Mifuko hiyo inaendelea kuwalipa watumishi hao kadri inavyopokea taarifa kutoka kwa waajiri.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kujenga mazingira wezeshi kwa waajiri, kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji, na kupunguza gharama za uendeshaji ili kukuza uchumi wa nchi na kulinda rasilimali watu. Hatua hizo ni pamoja na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kupunguza kiwango cha uchangiaji kwa waajiri wa sekta binafsi kutoka asilimia 0.6 hadi asilimia 0.5.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya hifadhi ya jamii kwa kuhakikisha wananchi wengi wanajumuishwa katika mpango wa Hifadhi ya Jamii wa uchangiaji. Natoa wito kwa sekta isiyo rasmi ikiwemo mama/baba lishe, machinga, bodaboda, wakulima, wavuvi, wafugaji, na wengineo kujiunga na mifuko hiyo kwa manufaa yao ya baadaye.
Ukuzaji wa Fursa za Ajira na Ujuzi
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu masuala ya uzalishaji wa fursa za ajira nchini kupitia utekelezaji wa miradi ya kielelezo, kujenga mazingira wezeshi kwa wawekezaji na kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi. Katika mwaka 2022/2023, jumla ya fursa za ajira 547,031 zilizalishwa. Kati ya hizo, ajira 321,363 zilizalishwa kupitia Serikali na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na 225,668 kupitia sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha wahitimu wa mafunzo ya ujuzi wanaunganishwa na fursa za kujiajiri. Utaratibu huo utamwezesha mhitimu wa mafunzo ya ujuzi kupata sehemu ya uzalishaji yenye viwango vinavyohitajika chini ya usimamizi wa watalaamu wenye uzoefu katika fani husika kwa kipindi maalumu cha miezi 6 hadi 12 kutegemeana na aina ya fani.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kuwezesha na kuratibu masuala ya ukuzaji wa fursa za ajira na kazi za staha kwa kuboresha na kutekeleza Sera, Mikakati na Mipango mbalimbali ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ili kuhakikisha nguvu kazi ya Taifa inapata fursa za kujiajiri au kuajiriwa ili kuchangia katika maendeleo ya Taifa.
UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza shughuli mbalimbali zinazolenga kuwawezesha wajasiriamali kukuza mitaji yao na kufikia masoko makubwa kupitia Vituo vya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Katika mwaka 2022/2023, jumla ya shilingi bilioni 326.6 zimetolewa kwa wajasiriamali 903,763. Kati yao wanawake ni 478,994 sawa na asilimia 53 na wanaume 424,769 sawa na asilimia 47. Upatikanaji wa fedha hizo umewawezesha wajasiriamali kuanzisha na kukuza biashara zao. Aidha, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (Women Development Fund - WDF), mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 663.4 ilitolewa kwa wanawake 96 ili kuwawezesha kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kuimarisha utendaji wa mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuwaunganisha wajasiriamali na fursa za kiuchumi. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha vituo vya uwezeshaji ili kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi.
MAENDELEO YA VIJANA
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwawezesha vijana ili kujiari, kushiriki kwenye shughuli za maendeleo na kuchangia katika pato la Taifa. Katika mwaka 2022/2023, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.88 kwa ajili ya kuwezesha miradi 85 ya vijana katika sekta za kilimo, viwanda na biashara kwenye halmashauri 28. Aidha, Serikali imetoa mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi, kurasimisha na kuendeleza biashara kwa vijana 2,497 walio katika mikoa ya Kagera, Dodoma, Katavi, Shinyanga na Lindi.
Vilevile, kazi ya kuboresha Mwongozo wa Utoaji mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana imekamilika na mfuko unatoa mikopo kwa vijana walio katika vikundi, mtu mmoja mmoja na kampuni.
Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, Serikali imeendelea kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili kupitia Mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora. Mpango huo unalenga kuongeza ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo kwa kuwapatia mafunzo, mashamba, mitaji na kuwaunganisha na fursa za masoko. Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Mpango huo imeanza mkoani Dodoma katika Shamba la Chinangali II lenye ukubwa wa ekari 400. Aidha, zaidi ya hekta 47,000 zimeshapatikana katika mikoa mbalimbali nchini na upimaji udongo unaendelea.
Mheshimiwa Spika, kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, Serikali imetoa fursa za mafunzo ya ujuzi wa kujiajiri au kuajiriwa kwa vijana 14,542 katika fani mbalimbali kupitia mafunzo ya uanagenzi, uzoefu wa kazi, ufugaji wa samaki na viumbe maji na kilimo cha kisasa kwa njia ya vizimba.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kuimarisha uwezo wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana katika kutoa mikopo na mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana wengi ili kuwawezesha kujiajiri na kuchangia uchumi wa Taifa. Vilevile, itaanzisha kampeni ya kuwashawishi vijana kushiriki katika kilimo.
MASUALA MTAMBUKA
Sensa ya Watu na Makazi 2022
Mheshimiwa Spika, nchi yetu ilitekeleza zoezi la Sensa ya Watu na Makazi tarehe 23 Agosti, 2022. Zoezi hilo lililojumuisha sensa ya watu na makazi, anwani za makazi na majengo lilifanyika kwa mafanikio makubwa na wananchi kuonesha ushirikiano wa hali ya juu. Matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi yalizinduliwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 30 Oktoba, 2022. Matokeo hayo ya awali yamechangia kwa kiasi kikubwa katika maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali ya mwaka 2023/2024. Aidha, Serikali imekamilisha ripoti nane ambazo zimejikita kwenye mgawanyo wa idadi ya watu kwa umri na jinsi. Ripoti hizi zitasaidia kuongeza wigo wa matumizi ya takwimu.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito kwa viongozi wenzangu na wananchi kuwa tuendelee kuhamasisha matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi, majengo na anwani za makazi katika biashara, shughuli za kijamii na mipango ya maendeleo ya nchi. Aidha, nitumie fursa hii kulishukuru Bunge lako tukufu kwa ushirikiano mkubwa ambao Waheshimiwa Wabunge walionesha wakati wa utekelezaji wa zoezi la sensa. Nawashukuru wenyeviti wa kamati za sensa katika ngazi mbalimbali kwa uongozi wao mahiri, makamisaa wa sensa na wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi na wananchi wote katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi, Majengo na Anwani za Makazi.
Mapambano Dhidi ya Rushwa
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali imeendelea kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi ambapo nguvu kubwa ilielekezwa kwenye uzuiaji wa vitendo hivyo. Hadi kufikia Februari, 2023, kesi za rushwa zipatazo 696 zikiwemo kesi mpya 203 ziliendeshwa mahakamani. Kati ya kesi hizo, kesi 248 ziliamuliwa mahakamani na watuhumiwa 142 walikutwa na hatia.
Mheshimiwa Spika, vilevile, ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo 810 yenye thamani ya shilingi trilioni 6.89 umefanyika. Kutokana na ufuatiliaji huo, miradi 119 yenye thamani ya shilingi billioni 46.04 ilionekana kuwa na kasoro mbalimbali katika utekelezaji na inaendelea kufanyiwa uchunguzi ili hatua stahiki zichukuliwe.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024 Serikali itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi kwa kuweka kipaumbele katika kuzuia vitendo vya rushwa. Serikali pia itatoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya vitendo vya rushwa kupitia programu ya TAKUKURU- RAFIKI.
Mapambano Dhidi ya UKIMWI
Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu UKIMWI umeendelea kuwa miongoni mwa majanga makubwa duniani kwa miongo kadhaa sasa. Serikali kwa kutambua ukweli huo, imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za mapambano dhidi ya ugonjwa huo. Jitihada hizo ni pamoja na kuandaa mikakati na kutekeleza afua mbalimbali za kupunguza maambukizi, unyanyapaa pamoja na vifo vitokanavyo na janga hilo.
Mheshimiwa Spika, kama mtakumbuka katika maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ya mwaka 2022 yaliyofanyika mkoani Lindi, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua Mkakati wa Tano wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI wa Mwaka 2021/2022 2025/2026. Mkakati huo umelenga kuhakikisha kuwa malengo ya sifuri tatu yatafikiwa ifikapo mwaka 2030. Malengo hayo ni kudhibiti maambukizi mapya ya VVU, kukomesha unyanyapaa na kutokomeza vifo vitokanavyo na UKIMWI.
Mheshimiwa Spika, kutokana na jitihada zilizofanyika ikiwemo matumizi ya dawa za ARV, afua za kinga zinazotekelezwa na wadau mbalimbali nchini na afua za mabadiliko ya tabia, tohara ya kitabibu kwa wanaume na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, maambukizi mapya ya VVU kwa watu wazima (miaka 15 na zaidi) yameshuka kutoka 110,000 mwaka 2010 hadi 54,000 mwaka 2022. Wakati huo huo, vifo vinavyotokana na UKIMWI vimepungua kwa asilimia 55 kutoka vifo 65,000 mwaka 2010 hadi 29,000 mwaka 2022. Vilevile, maambukizi mapya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yameshuka kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 7 mwaka 2022.
Mheshimiwa Spika, matumizi ya dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI kwa WAVIU wanaojua hali zao za maambukizi yameongezeka kutoka asilimia 95 mwaka 2016 hadi asilimia 98 mwaka 2022. Hadi kufikia Desemba, 2022 WAVIU zaidi ya milioni 1.5 walikuwa kwenye huduma za tiba na matunzo. Aidha, WAVIU wanaofahamu hali zao za maambukizi na wapo kwenye matibabu ni asilimia 99 na WAVIU waliopo kwenye matibabu na wamefubaza VVU ni asilimia 98. Mafanikio haya ni makubwa ikilinganishwa na malengo ya Kimataifa ya kufikia 95-95-95.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana, bado kuna mambo mengi yanayohitaji kufanyika ili kufikia azma yetu ya kumaliza kabisa janga la UKIMWI. Kwa kutambua hilo, Serikali itaendelea kutenga rasilimali za kutosha kwa ajili ya Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI, na kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za UKIMWI pamoja na afua nyingine mahsusi za kudhibiti janga hilo. Kwa upande mwingine, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutekeleza afua za mapambano dhidi ya UKIMWI. Nitumie fursa hii kushukuru sana asasi za kiraia na wadau wa maendeleo kwa michango yao katika mapambano ya kutokomeza UKIMWI nchini.
Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua madhara ya dawa za kulevya kwa nguvu kazi hapa nchini, imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya dawa hizo. Katika mwaka 2022/2023, imeendesha oparesheni za kuwakamata wanaojihusisha na biashara hiyo pamoja na kuzuia mianya ya kusafirisha na kusambaza dawa hizo. Katika oparesheni hizo watuhumiwa 7,113 pamoja na kilogramu 20,450.30 za dawa za kulevya zilikamatwa. Dawa hizo ni heroin kilogramu 53.01, cocaine gramu 843.55, bangi kilogramu 12,869.39, mirungi kilogramu 7,525.53, na aina nyingine ya dawa za kulevya (Methamphetamine na Mescaline) gramu 1,024.7. Aidha, iliteketeza ekari 69 za mashamba ya bangi katika maeneo mbalimbali nchini na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha huduma za matibabu kwa watumiaji wa dawa za kulevya kwa kuongeza idadi ya kliniki zinazotoa huduma kwa waathirika wa dawa za kulevya kutoka 9 mwaka 2020/2021 hadi kliniki 15 zinazohudumia waathirika zaidi ya 14,500 mwaka 2022/2023. Licha ya hayo, Serikali kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi imewezesha waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu wapatao 245 kupata mafunzo ya ujuzi kupitia vyuo vya VETA, Don Bosco na SIDO.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia na kuratibu uendeshwaji wa nyumba za upataji nafuu 44 nchini, kuzijengea uwezo asasi za kiraia 65 ambazo zinatoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya kwa jamii, kuandaa Mwongozo wa Utoaji Elimu kuhusu Tatizo la Dawa za Kulevya nchini ambao umezinduliwa tarehe 02 Julai, 2022 kwa lengo la kuwapatia elimu na mbinu sahihi kulingana na mahitaji ya makundi mbalimbali ya kijamii. Nitoe wito kwa wadau wote mkiwemo Waheshimiwa Wabunge wenzangu, asasi za kiraia, viongozi wa dini, vyombo vya habari na jamii nzima kushirikiana na Serikali kutoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya ili kuokoa kizazi cha sasa na kijacho.
Uratibu wa Maafa
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha nchi inakuwa stahimilivu dhidi ya majanga kwa kuweka utaratibu mzuri wa kushughulikia masuala ya maafa hapa nchini. Ili kuweka utaratibu huo, Serikali imetunga Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya Mwaka 2022; Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa wa Mwaka 2022-2027; Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa wa Mwaka 2022; Mkakati wa Taifa wa Afya Moja wa Mwaka 2022-2027; na Mwongozo wa Taifa wa Kupambana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu wa Mwaka 2022. Kama mtakumbuka, Nyaraka hizo nilizizindua tarehe 09 Februari, 2023 kwa ajili ya utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, nyaraka hizo zimeweka utaratibu wa kuhakikisha Wizara, Idara, Taasisi za Umma na zisizo za Umma, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zinashiriki kikamilifu katika kutekeleza shughuli za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga. Aidha, zimeweka pia utaratibu wa kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali iliyotoweka pindi maafa yanapotokea. Nitoe wito kwa taasisi husika kuandaa mipango kazi na taratibu za usimamizi wa maafa pamoja na ushughulikiaji wa dharura.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, jumla ya wajumbe 555 wa Kamati za Usimamizi wa Maafa na Waratibu wa Maafa walipata mafunzo ya kuimarisha uwezo wa utendaji kazi katika mikoa ya Arusha, Morogoro, Kilimanjaro, Lindi, Mtwara na Singida. Aidha, jumla ya wavuvi 344 katika mwambao wa Ziwa Victoria na vijana 40 wa kujitolea katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Songwe na Tabora walipata mafunzo ya uokoaji, yaliyowaongezea uwezo wa kukabiliana na maafa kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza ushirikiano na nchi nyingine katika kushughulikia masuala ya maafa ikiwemo nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kusaini mkataba wa kuanzisha Kituo cha Huduma za Binadamu na Operesheni za Dharura cha Kanda ya SADC. Lengo la kuanzisha kituo hicho ni kusimamia utoaji wa huduma na misaada ya kibinadamu kwa nchi wanachama. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, masuala ya majanga hayana mipaka na hayana muda na yanahitaji jitihada za pamoja katika kuyashughulikia.
Mheshimiwa Spika, kama mtakumbuka, katika kuendeleza uhusiano na nchi nyingine, hivi karibuni nchi yetu imeungana na mataifa mengine duniani kutoa misaada ya kibinadamu kwa nchi zilizopatwa na maafa makubwa yaliyosababisha vifo na majeruhi, uharibifu wa mali na mazingira. Nchi hizo ni pamoja na Malawi iliyokumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga Freddy kilichotokea tarehe 13 Machi, 2023 na nchi ya Uturuki iliyokumbwa na tetemeko la ardhi mwezi Februari, mwaka huu. Misaada iliyotolewa kwa nchi ya Malawi ni pamoja na mahindi tani 1,000, mablanketi 6,000, mahema 50, fedha taslimu shilingi milioni 705, dawa za binadamu na helkopta 2 kwa ajili ya kusaidia uokoaji. Aidha, fedha taslimu dola za Marekani milioni moja zilitolewa kwa nchi ya Uturuki.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea na ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa Jijini Dodoma, kuimarisha maghala ya vifaa vya misaada ya kibinadamu kwa kuongeza vifaa na kuendelea kutoa misaada kwa waathirika wa maafa. Hata hivyo, kila wizara na taasisi watalazimika kujiandaa kwa vifaa vya kukabiliana na kulingana na mahitaji ya wizara au taasisi husika.
Uratibu wa Masuala ya Lishe
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali imeendelea kutekeleza afua mbalimbali za lishe ili kuimarisha afya na hivyo kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Kutokana na umuhimu wa masuala ya lishe, tarehe 30 Septemba, 2022 Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisaini mikataba na Wakuu wa Mikoa yote Tanzania Bara kwa lengo la kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwenye masuala ya lishe ikiwa ni pamoja na kuhakikisha halmashauri zinatenga shilingi 1,000 kwa kila mtoto chini ya miaka mitano. Vilevile, alielekeza fedha zinazopangwa kutekeleza afua za lishe kutolewa kwa wakati na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhamasishaji wa utekelezaji wa afua za lishe bora na kuweka mikakati ya kuhakikisha vyakula vinavyohitajika kukamilisha lishe vinapatikana katika ngazi zote.
Mheshimiwa Spika, maelekezo hayo ya Mheshimiwa Rais yaliongeza chachu ya utekelezaji wa masuala ya lishe sambamba na malengo yaliyoainishwa kwenye Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe wa Mwaka 2021/2022 - 2025/2026. Aidha, katika Mkutano wa Nane wa Wadau wa Lishe Kitaifa, uliofanyika Disemba, 2022 Mkoani Mara, Mkakati wa Sekta Binafsi unaoainisha mikakati ya sekta hiyo kuiunga mkono Serikali kuimarisha hali ya lishe nchini ulizinduliwa.
Mheshimiwa Spika, kutokana na jitihada mbalimbali za Serikali na wadau, yapo baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ambayo ni pamoja na kupungua kwa udumavu kutoka asilimia 34.4 mwaka 2015/2016 hadi asilimia 30 mwaka 2022 na kupungua kwa kiwango cha ukondefu kutoka asilimia 4.5 hadi 3.3 katika kipindi hicho.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Pili wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe wa Mwaka 2021/2022 - 2025/2026. Nitoe wito kwa wananchi kuzingatia ulaji sahihi wa vyakula mchanganyiko kama tunavyoelekezwa na wataalamu wetu wa masuala ya lishe. Vilevile, niwaombe wadau wa maendeleo na sekta binafsi waendelee kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha hali ya lishe nchini.
Mazingira
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita katika kuweka msisitizo wa uhifadhi wa mazingira imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali pamoja na maboresho ya Sera na Sheria ili ziwiane na mahitaji ya sasa ya kitaifa, kikanda na kimataifa. Katika kutelekeza azma hiyo, Serikali imeandaa Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022 - 2032) kwa lengo la kutoa mwongozo wa hatua za kuchukua ili kutatua changamoto za mazingira nchini kwa kuzingatia sehemu husika na hatua mahsusi zinazopaswa kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeandaa Kanuni za Biashara ya Kaboni za Mwaka 2022 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali kupitia GN 636 kwa lugha ya Kingereza na GN 637 kwa lugha ya Kiswahili. Aidha, Serikali imeandaa Mwongozo kwa ajili ya kutoa maelekezo mbalimbali kuhusu ushiriki wa wadau katika biashara hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine Serikali imeratibu ushiriki wa nchi katika mikutano ya kimataifa. Mikutano hiyo imekuwa na mafanikio na munafaa kwa Taifa letu ambapo kupitia Mkutano wa 27 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Tanzania imepata miradi ya nishati jadidifu ambayo itafadhiliwa na Benki ya Dunia, Taasisi ya Afrika 50 na Shirika la Nishati la Afrika kwa kushirikiana na kampuni ya China Renewable Energies.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira na kuchukua hatua za kupunguza uharibifu wa mazingira. Aidha, itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu hifadhi na usimamizi wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi na fursa ya biashara ya kaboni. Vilevile, itaratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191 pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu mabadiliko ya Sheria na Sera ya Mazingira.
UCHUMI WA BULUU
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha wananchi juu ya kuibua fursa zilizo kwenye Uchumi wa Buluu kupitia matumizi endelevu ya rasilimali maji kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira na ushirikishwaji wa jamii. Hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kuendelea kukamilisha Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu pamoja na Mkakati wa Utekelezaji. Sera hiyo italenga kukuza uwekezaji katika rasilimali za Uchumi wa Buluu; kuongeza fursa za ajira na kazi za staha kupitia shughuli za uchumi wa buluu; na kuwa na usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za uchumi wa buluu unaozingatia misingi ya utawala bora.
Utawala Bora
Mheshimiwa Spika; Serikali imeendelea kujenga uelewa wa pamoja kwa wadau wote hususan wananchi kuhusu masuala ya kisheria, upatikanaji wa haki zao, kuongeza uwazi na kupunguza gharama. Vilevile, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kukamilisha rasimu ya Awali ya ufasiri wa Sheria Kuu 219 na Sheria Ndogo 148 kwa lugha ya Kiswahili. Zoezi la ufasiri wa Sheria Kuu na Sheria Ndogo zote kutoka lugha ya Kingereza kwenda lugha ya Kiswahili ili kupanua wigo wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kama lugha ya Sheria katika vyombo vya utoaji haki ikiwemo Mahakama, Mabaraza na vyombo vingine vyenye jukumu la kutoa haki linaendelea.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kutekeleza Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala na kuendelea kutafsiri sheria kutoka lugha ya Kiingereza kuwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi kuelewa mwenendo wa mashauri yanayowahusu na hivyo kuweza kupata haki zao.
MFUMO WA SERIKALI WA TEHAMA
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya Mfumo wake wa TEHAMA wa kubadilishana taarifa ambapo hadi sasa jumla ya mifumo 60 ya Taasisi 55 imeunganishwa na inabadilishana taarifa. Utekelezaji huo pia ni maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa na mifumo michache inayobadilishana taarifa. Uunganishaji wa mifumo hiyo umeongeza tija na ufanisi katika kuwahudumia wadau hususan wananchi.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kurahisisha utendaji kazi kwa kutumia mfumo wa TEHAMA, kupunguza gharama za kutoa huduma ili kutoa unafuu kwa wananchi pamoja na kuimarisha mifumo inayobadilishana taarifa.
UKATILI DHIDI YA WATOTO
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza afua mbalimbali za kupinga ukatili dhidi ya watoto shuleni na nje ya shule. Katika mwaka 2022/2023, hatua zilizochukuliwa ili kupinga ukatili huo ni pamoja na kuunda madawati 1,393 ya ulinzi na usalama wa mtoto katika shule za msingi na sekondari kwenye mikoa ya Rukwa, Arusha, Tanga, Dar es Saalam, Pwani, Shinyanga, Dodoma na Geita. Vilevile, Mabaraza ya Watoto 560 yameundwa kwa lengo la kutoa fursa kwa watoto kutoa maoni yao kwa uhuru na kuwajengea uwezo wa kujiamini, kujieleza na kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu haki na ustawi wa watoto.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeendelea kuhamasisha jamii kushiriki katika ulinzi na usalama wa mtoto ili kutokomeza ukatili dhidi ya watoto. Aidha, kupitia jitihada mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (2021/2022 - 2024/2025), wananchi wameendelea kuhamasishwa kujitolea kwa hiari kupambana na vitendo vya ukatili ikiwa ni pamoja na kutambua wajibu wao juu ya ulinzi wa mtoto kuanzia ngazi ya familia.
Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa mamlaka zinazohusika chini ya uratibu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kuimarisha mfumo wa ushughulikiaji wa matukio ya ukatili dhidi ya watoto ndani na nje ya shule unaowajumuisha wasimamizi wa shule, wazazi, walezi na jamii na kuandaa mfumo jumuishi wa kukusanya taarifa na takwimu za vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
MUUNGANO
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwa lengo la kuulinda, kuuenzi na kuudumisha muungano wetu. Katika mwaka 2022/2023, jumla ya hoja nne kati ya nane zilipatiwa ufumbuzi na kuondolewa katika orodha ya hoja za Muungano. Vilevile, Serikali iliandaa kitabu kinachoitwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar: Chimbuko, Misingi na Maendeleo. Kitabu hiki kimepatiwa ithibati ili kitumike kama kitabu cha ziada kwa shule za sekondari nchini na kuendelea kukuza uelewa kuhusu Muungano.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zitaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuendelea kutatua changamoto zilizosalia kwa lengo la kuulinda, kuuenzi na kuudumisha muungano wetu.
USHIRIKIANO WA KIKANDA NA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika, sote tumeshuhudia kuimarika kwa mahusiano yetu na nchi nyingine, jumuiya za kikanda na mashirika ya kimataifa chini ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kuimarika kwa ushirikiano huo kumetokana na Serikali kuendelea kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje inayoweka msisitizo katika kutekeleza diplomasia ya kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mahusiano na mataifa mengine duniani, Viongozi wetu Wakuu wakiongozwa na Rais wetu wameshiriki katika ziara mbalimbali ambazo zimeiletea manufaa makubwa nchi yetu. Mathalan, Novemba 2022, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliitembelea China kufuatia mwaliko uliotolewa na Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China. Vilevile, viongozi wetu wakuu wameshiriki katika ziara mbalimbali za kikazi katika nchi za Marekani, Qatar, Ethiopia, Kenya, Misri, Oman, Afrika Kusini, Rwanda, na Burundi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ziara hizo, nchi yetu imenufaika katika uboreshaji wa miundombinu, huduma za jamii, biashara, uwekezaji, uchumi wa kidijitali, maendeleo ya kijani, uchumi wa bluu, uvuvi, fedha, utalii, afya na kilimo.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza diplomasia ya kiuchumi, Serikali imeratibu majadiliano ya awamu ya pili ya kuanzisha Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) kwa upande wa Afrika Mashariki. Ushiriki wa nchi yetu katika eneo huru la biashara utachochea ukuaji wa uchumi na biashara, kukuza ushiriki wetu katika biashara ya Dunia na kujenga uwezo wa kuongeza thamani ya bidhaa kupitia sera bora za kukuza teknolojia, ubunifu na ushindani.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kufungua nchi kiuchumi kwa kuvutia uwekezaji na kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini; kuimarisha mahusiano ya kikanda na kimataifa na kutangaza fursa za utalii na uwekezaji katika sekta mbalimbali za maeneo ya kipaumbele hususan uchumi wa bluu na kidijitali.
SERIKALI KUHAMIA DODOMA
Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya sita imeendelea kutekeleza kwa vitendo zoezi la Serikali kuhamia Dodoma kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma za Serikali kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali imeendelea na awamu ya pili ya ujenzi wa majengo ya Ofisi za Wizara na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba. Ujenzi huo umefikia wastani wa asilimia 60. Aidha, kazi nyingine zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato kitakachogharimu shilingi bilioni 165 na ujenzi wa barabara ya mzunguko ya nje yenye urefu wa kilomita 112.3 kwa gharama ya shilingi bilioni 221. Kwa upande wa Balozi na Jumuiya za Kimataifa, balozi za nchi za Ujerumani, Ufaransa, China na Umoja wa Mataifa zimefungua ofisi ndogo jijini Dodoma.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kukamilisha awamu ya pili ya ujenzi wa majengo ya Ofisi za Wizara, Ofisi za Taasisi na miundombinu ya kudumu kwenye Mji wa Serikali pamoja na kuendelea kuratibu uhamiaji wa taasisi.
SANAA, UTAMADUNI NA MICHEZO
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kukuza utamaduni, sanaa na michezo imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta hiyo kwa kuzingatia kuwa sekta hii ni chachu ya kuendeleza utamaduni wa Kitanzania, utambulisho wa Taifa, chanzo kikubwa cha ajira, huimarisha afya pamoja na kuchangia katika pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, ili kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kusajili vituo 30 vya kufundisha Kiswahili. Kati ya hivyo: vituo 10 vipo katika Balozi za nchi yetu nchini Korea Kusini, Ufaransa, Italia, Mauritius, Nigeria, Sudan, Zimbabwe, Uholanzi, Cuba na Umoja wa Falme za Kiarabu; vituo vinne nje ya Balozi zetu katika nchi za Afrika Kusini, Italia, Ujerumani na Ethiopia na vituo 16 vya kufundisha lugha hiyo vimeanzishwa nchini. Aidha, kwa upande mwingine Tanzania imesaini makubaliano na nchi ya Afrika Kusini kuwezesha nchi hiyo kutumia Kiswahili kuwa lugha ya kujifunza na kufundishia katika elimu ya msingi.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeendelea kuimarisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ili kuwawezesha wasanii kuendeleza kazi zao kwa kuwapa mikopo na elimu ya ujasiriamali. Hadi kufikia Februari, 2023 tayari imeshatoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.07 kwa wanufaika 45 ambao ni wasanii na wadau wa sanaa. Mikopo hiyo imewawezesha wasanii na wadau wa sanaa kuandaa kazi bora na zenye uwezo wa kuhimili ushindani katika soko la sanaa.
Mheshimiwa Spika, kwa nafasi hii, nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa motisha kwa vilabu vya ndani vinavyoshiriki mashindano ya kimataifa kupitia Goli la Mama ambapo amekuwa akitoa shilingi milioni tano kwa kila goli linalofungwa. Sote tumeshuhudia Simba Sports Club almaarufu Wekundu wa Msimbazi wakijitwalia kitita cha shilingi milioni 50 wakati huo huo klabu ya Young Africans Sports Club almaarufu Timu ya Wananchi wakijitwalia shilingi milioni 45.
Mheshimiwa Spika, ninavipongeza sana vilabu hivyo kwa kufika hatua ya robo fainali katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Barani Afrika. Ni matumaini yetu sote kuwa vilabu hivyo na vingine vinavyoshiriki mashindano ya kimataifa vitaendelea kujituma na kupambana ili vikombe vya ushindi vije nyumbani.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2023/2024 Serikali itaendelea kuratibu Programu ya Ukarabati wa Viwanja vya Michezo katika shule 56 katika mikoa yote Tanzania Bara; kuratibu Programu ya Sanaa na Michezo ya kuanzia ngazi ya Mtaa kwa Mtaa kuelekea ngazi za juu ikiwemo Taifa Cup; kutenga maeneo ya michezo kwa lengo la kujenga miundombinu ya mchezo na kuimarisha michezo katika ngazi za mikoa na wilaya; kuhakikisha kazi za sanaa na utamaduni zinazoandaliwa zinazingatia maadili ya jamii na Taifa kwa ujumla; na kuendelea kutambua maeneo ya urithi wa utamaduni na ukombozi katika mikoa na halmashauri za wilaya kwa lengo la kulinda, kuhifadhi na kuendeleza maeneo hayo ili kuinua utalii wa kiutamaduni na kiukombozi nchini.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024, Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kuratibu utekelezaji wa sera na shughuli za Serikali ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi; kuratibu shughuli za maafa nchini; kuratibu shughuli za Serikali Bungeni; kushughulikia kero na malalamiko mbalimbali ya wananchi; kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utendaji wa Serikali; na kuratibu masuala yanayohusu kazi, maendeleo ya vijana, ajira, hifadhi ya jamii na huduma za watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, nimeeleza kwa muhtasari baadhi ya shughuli ambazo Serikali imetekeleza kwa kipindi kilichopita na mwelekeo wa kazi zitakazofanyika kwa mwaka 2023/2024. Kwa kuhitimisha, ninapenda kusisitiza mambo muhimu yafuatayo:
Mosi: Wizara, taasisi za Serikali, Tawala za Mikoa na Halmashauri ziimarishe ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa nidhamu ya matumizi ya fedha za umma pamoja na kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango na Bajeti ya Mwaka 2023/2024 hususan miradi ya kitaifa ya kimkakati;
Pili: Wadau wote pamoja na Serikali kwa ujumla waendelee kutumia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 katika shughuli mbalimbali kama vile uwekezaji, biashara, tafiti na mipango mbalimbali ya maendeleo. Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ili kuongeza uelewa, uwazi na kupanua wigo wa matumizi ya matokeo ya sensa kwa Serikali, wananchi na wadau wote;
Tatu: Viongozi wote wa Serikali, dini, mila na vyama vya siasa wakemee kwa nguvu zote ushiriki wa sehemu yoyote ya jamii katika matendo yasiyoendana na mila, tamaduni na desturi za Watanzania. Hii ni pamoja na wazazi na walezi wote kushiriki kikamilifu katika makuzi na malezi bora ya watoto yatakayosaidia kuwaepusha na vitendo viovu;
Nne: Serikali na taasisi ziendelee kuhakikisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini yanaendelea kuimarishwa ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi;
Tano: Wizara na taasisi ziendelee kutenga fedha kwa ajili ya shughuli za ufuatiliaji na tathmini katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wanaotekeleza jukumu hilo. Lengo ni kuwezesha utendaji wenye matokeo na kufanikisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi; na
Sita: Viongozi wa siasa, dini na wadau wengine wahamasishe wananchi kushiriki kikamilifu katika maandalizi na uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024.
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2023/2024
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2023/2024, Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake inaliomba Bunge lako tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 173,733,110,000. Kati ya fedha hizo, shilingi 121,364,753,320 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 52,368,356,680 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, vilevile naliomba Bunge lako tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 165,627,897,000 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, shilingi 160,458,877,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 5,169,020,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.