NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Maendeleo ya Kiserikali katika Pembe ya Afrika (IGAD) imetoa wito wa kusitishwa mara moja kwa uhasama kati ya pande zinazozozana nchini Sudan.
Wito huo umetolewa hivi karibuni katika mkutano wa kawaida wa wakuu wa nchi kujadili mgogoro huo, ambapo Rais wa Jamhuri ya Kenya,Dkt.William Ruto aliungana na marais Salva Kiir wa Sudan Kusini, Yoweri Museveni wa Uganda, Ismail Omar Guelleh wa Djibouti na Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.
Mheshimiwa Rais Dkt.William Ruto aliwataka viongozi wa IGAD kuchukua msimamo thabiti kurejesha amani jijini Khartoum, Sudan.
Viongozi hao walitoa wito kwa Baraza la Mpito chini ya Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo kusitisha vita na kurejea kwenye mazungumzo.
IGAD iliazimia kuwatuma marais Kiir, Rais Ruto na Rais Guelleh haraka iwezekanavyo ili kupatanisha makundi hayo yanayozozana.Walisema utulivu nchini Sudan ni muhimu kwa utulivu wa kijamii na kiuchumi wa eneo hilo.
Mzozo huo, waliongeza, unadhoofisha maendeleo ya amani yaliyopatikana katika kipindi cha miezi minne iliyopita.
Viongozi hao pia waliyataka makundi hayo mawili kutoa njia salama kwa ajili ya usaidizi wa kibinadamu huko Khartoum na miji mingine iliyoathiriwa nchini Sudan.