Jela kwa kutoa tiba asili bila kibali

NA DIRAMAKINI

SALIM Amiri mwenye umri wa miaka 34 amehukumiwa kwenda jela miaka mitatu kwa kosa la kufanya shughuli za tiba za asili bila kuwa na kibali.

Amiri mkazi wa Kijiji cha Kangala Kata ya Loiborsiret wilayani Simanjiro mkoani Manyara alikuwa akifanya shughuli za uganga wa kienyeji kijijini humo

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Charles Uiso baada ya mshakiwa kukiri kosa hilo na kukutwa akiwa na zana za kazi yake.

Hakimu Uiso amesema, mshtakiwa huyo ambaye amekiri kosa hilo alikutwa na shanga, vibuyu na pembe akitoa tiba za jadi kwa watu bila kuwa na kibali kwenye Kijiji cha Kangala.

Hakimu huyo alitoa hukumu ya Amiri kutumikia kifungo cha miaka mitatu kwenda jela au kutozwa faini ya shilingi 200,000.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mosses Hamilton ameieleza mahakama kuwa, Salim Amiri hana taarifa za kufanya uhalifu na kutumikia kifungo hivyo itoe adhabu kulingana na sheria.

Aidha, mshtakiwa huyo aliiomba Mahakama hiyo imuonee huruma na kumpunguzia adhabu kwani ni kosa lake la kwanza na ana familia ya mke na watoto wanamtegemea.

Hata hivyo, mshtakiwa wa pili wa kesi hiyo ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kangala, Mohamed Kadangu (37) alikana shataka hilo alipoulizwa mahakamani hapo kama ni kweli alitenda kosa hilo.

Kesi hiyo itaendelea tena Mei 10, mwaka huu kwa mshtakiwa wa pili Kadangu ambaye yeye hakukubali kosa hivyo hakimu ameahirisha hadi itakapoendelea mahakamani hapo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news