JOWUTA,LHRC kuwasaidia wafanyakazi wa Sahara Media kulipwa madai yao Bilioni 3.5/-

NA DIRAMAKINI

CHAMA cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kimetangaza kushirikiana na Kituo Cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) kuwasaidia wafanyakazi 195 wa kampuni ya Sahara Media kudai kulipwa malimbikizo ya madai ya mishahara yao kiasi cha sh 3.5 bilioni.
Uamuzi huo,umetangazwa Jana na Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa,Mussa Juma na Mjumbe wa bodi ya udhamini wa JOWUTA,Mutta Robert katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ukumbi wa chama cha ushirika Nyanza.baada ya kukutana na pande zote katika mgogoro huo.

Juma amesema baada ya majadiliano baina ya wafanyakazi wa kampuni hiyo na ofisi ya Idara ya kazi mkoa wa Mwanza na LHRC wameazimia kupeleka mgogoro huo katika Tume ya Usuluhishi (CMA).

"Kwa kuwa mwajiri hajakaidi kulipa deni hili na kuwa ameshindwa kulipa licha ya kuahidi kufanya hivyo hali yake ya fedha itakapokuwa nzuri,tumeona njia bora ni kupeleka shauri hili CMA,"amesema.

Amesema, JOWUTA kama chama cha wafanyakazi itashirikiana na LHRC na wanasheria wengine ambao tayari wameonesha nia Ili kuhakikisha haki za wafanyakazi hao zinapatikana.

Juma amesema uamuzi huo,pia umefikia Ili kulinda heshma ya Tasnia ya Habari nchini,kwani kwa Sasa ni miongoni mwa sekta ambazo zinachangamoto kubwa ya malipo na stahiki za waandishi na watangazaji kwani wengi hawana mikataba licha ya kufanya kazi miaka mingi.

"JOWUTA tunaamini kesi hii ya Mwanza itakuwa ni mfano wa kesi nyingine ambazo zitafuata katika kulinda na kutetea maslahi ya wafanyakazi katika vyombo vya habari nchini,kwani hadi sasa kuna waandishi wanaolipwa shilingi 1000 kwa habari moja na wengi hawalipwi kabisa na kubaki kutegemea kulipwa na wanaowapa habari,"amesema.

Amesema, Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari wanastahiki kupata heshima na hadhi sawa na wafanyakazi wa sekta nyingine kwani licha ya serikali kutunga sheria za kazi na sheria za vyombo vya habari lakini bado wanahabari wanataabika.

"Wanahabari licha ya kufanya kazi kubwa bado asilimia 80 hawana ajira za kudumu wala mikataba tofauti na taaluma nyingine hali ambayo imekuwa ikiathiri utendaji wao wa kazi,"amesema.

Amesema, wakati wamiliki wa vyombo vya habari wakililia uhuru wa vyombo vya habari na kulipwa malimbikizo ya madeni ya matangazo wanapaswa kutambua kuwa uhuru huo hautakamilika kama wanahabari wakiendelea kuwa na maslahi duni, kufanya kazi bila mikataba na kutolipwa mishahara.

"Tunataka katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari mwaka huu suala la maslahi bora kwa wanahabari lipewe kipaumbele, kwani uhuru wa vyombo vya habari hauna maana kama hakuna maslahi bora kwa wanahabari, tunaiomba serikali kuchukuwa hatua kwa wamiliki ambao hawazingatii sheria licha ya kupata mapato katika vyombo vyao,"amesema.

Wakili Hamisi Mayomba wa LHRC amesema tayari taratibu za kufungua shauri hilo zimeanza na ambacho kinasubiriwa kukamilishwa kuna nyaraka mbalimbali ambazo zitasaidia katika shauri hilo.

Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini JOWUTA,Mutta Robert alisema watatumia sheria za kazi kufungua mashauri katika vyombo vyote vya habari ambavyo havilipi wanahabari.

"Sheria za kazi zipo tutahakikisha tunazitumia kulinda heshima ya taaluma hii kwani kuna wamiliki wa vyombo vya habari wanawatumia wanahabari kama vitega uchumi vyao,"amesema.

Robert ambaye pia ni Mwanasheria amesema sheria zipo wazi na lazima zifuatwe na wamiliki wa Vyombo vya Habari na kesi ya Mwanza itakuwa mfano kwa wamiliki wengine ambao hawazingatii sheria za kazi.

Awali Afisa kazi kiongozi mkoa wa Mwanza, Betty Mtega alisema ofisi yake imechoshwa na mashauri ya Wanahabari kushindwa kulipwa stahiki zao.

"Tumekuwa na kesi ya Sahara Media na vituo vingine vya radio hawataki kufuata sheria kuwalipa wafanyakazi wao licha ya kukiri kudaiwa,"amesema.

Hata hivyo, amesema serikali pia haijakaa kimya na shauri la Sahara media kwani hivi karibuni litafikishwa mahakamani na ofisi ya Mwanasheria Mkuu Kanda ya Ziwa.

"Kamishna wa Kazi nchini tayari amekamilisha taratibu zote za shauri hili kufikishwa vyombo vya sheria na kumbukumbu zetu hadi kufikia mwezi Mei mwaka 2021 wafanyakazi 152 walikuwa wanadai zaidi ya sh 2.5 bilioni na mwajiri amekiri kudaiwa,"amesema.

Hata hivyo amesema deni hilo limekuwa kubwa kutokana pia na wanahabari kutojua sheria za kazi kwani walipaswa kufungua mashauri mara tu wanaposhindwa kulipwa kwa miezi miwili.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza,Edwin Soko amewataka wamiliki wa vyombo vya habari kutuamini wafanyakazi wao kuhakikisha wanawaajiri na kuwapa mikataba bora.

"Mwanahabari bora ni yule ambaye pia uchumi wake upo vizuri, hivyo wamiliki wakiwalipa vizuri wafanyakazi wao wataweza kufanya kazi kwa weledi mkubwa,"amesema.

Hata hivyo, Soko amewataka wanahabari nchini kujiunga na JOWUTA kwani kisheria ndio chama pekee cha wafanyakazi ambacho kinadhamana ya kutetea maslahi yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Biashara inaweza kukuletea maisha bora kama ikifanikiwa. Ikifeli inaweza kukuua kwa mafikirio ya hasara au madeni. Namjua Mwalimu Mwenzangu (nilifanya kazi ya ualimu kwa miaka karibu 7) ambaye miaka miwili iliyopita kajiua kwa kanywa sumu baada ya kuzidiwa mafikirio yaliyoletwa na kudaiwa pande zote za maisha yake, madeni ambayo yalitokana na biashara zilizoenda vibaya.

    Nimeanza kwa maelezo hayo kujaribu kumsogeza yoyote kati yetu ambaye anao uhusiano na hawa wanaodai Shilingi Bilioni 3.5/- kwamba deni hili katika biashara ni kubwa sana. Siamini hata kidogo kama hili deni lilifikia kiwango hicho kwa kiburi cha Mwajiri. Hili deni linaweza kuwa lilifikia hapo kutokana na biashara kufeli. Uwezekano mkubwa hili ni deni ambalo lineletwa na ‘force majure’ na huwezi kulazimisha adhabu katika mazingira ya ‘force majure’.

    Internet ameharibu kabisa biashara za vyombo vya habari traditional kama Majarida, Magazeti, Television na Radio. Mitandao ya kijamii imepoka kipato cha vyombo hivi traditional kwa kuchukua sehemu kubwa ya matangazo. Mitandao ya kijamii msingi wake upo katika internet ambayo imerahisisha sana kusambaa kwa matangazo ya biashara.

    Ninachotaka kusema ni kwamba Mwandishi wa habari au mtu katika taaluma nyingine –labda pengine ni accounts, graphics dept, marketing ukiwa katika chombo cha habari traditional—nadhani ni hekima ukajua upo eneo lisilo kuwa na uwezo tena kupata fedha nyingi za kulipa wafanyakazi. Kama ukielewa hili nadhani ni busara ama kutoka, ama kuanza kujenga vyanzo vingine vya kipato.

    Hapa nataka nifananishe hivi: Kung’ang’ania malipo mahali ambapo kwa hakika unajua mazingira hayaruhusu Tsh. Bilioni 3.5/- kupatikana kesho ni kutafuta damu ya kisusio kwenye mti mkavu. Ushauri wangu ni kwamba wanaodai hizo fedha wajaribu kuangalia njia mbadala za kuishi. Hata kilimo ni njia mojawapo kama ajira mbadala haitapatikana.

    Ninazo taarifa kuna magazeti yaliyokuwa yanachapa nakala elf 10 leo yanachapa nakala 2000 na haziuzwi zikaisha. Watu wapo mitandaoni kutafuta taarifa na taarifa hizo zinapatina kwa bando la shilingi 500. Utanunua gazeti la shilingi 1000 la nini kama taarifa unazipata kwa jero.

    Nashauri hawa wanaodai hizo Bilioni 3.5/- wasiweke sana tumaini kwenye malipo ya hilo deni na sababu yangu si kiburi cha mwajiri, bali mazingira ya uchumi hayataruhusu mwajiri huyo kuwalipa. Mazingira ya kiuchumi kwa vyombo vya habari traditional si rafiki kabisa kwa sasa. Naamini mwajiri huyu ana ukata ambao umeletwa na force majure. Napendekezwa Itafutwe namna ya kumhurumia au hata kumsamehe kabisa madeni.

    Mtapata faida gani mkimuua huyu mfanyabiashara kwa mafikirio?

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news